Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipigo kilivyompa Isa Bodi ukocha wa ngumi

BODI Pict

Muktasari:

  • Huyu ni Isa Bodi, kocha wa ngumi za kulipwa, ambaye anasema aligundua kuwa moyo wake haukuwa kwenye kupigana, bali kuwafundisha wengine namna ya kuingia ulingoni, kupambana na kuendeleza vipaji vyao.

KIPIGO alichokipata ulingoni kilimfanya abadili ndoto zake kutoka kuwa bondia na kuamua kujikita katika ukocha, kazi ambayo sasa inamuwezesha kuwafundisha baadhi ya mabondia wanaotambulika nchini, akiwamo Hassan Mwakinyo na Ibra Classic.

Huyu ni Isa Bodi, kocha wa ngumi za kulipwa, ambaye anasema aligundua kuwa moyo wake haukuwa kwenye kupigana, bali kuwafundisha wengine namna ya kuingia ulingoni, kupambana na kuendeleza vipaji vyao.


BID 01

ALIVYOANZA

Isa anasema alianza safari yake ya ngumi akifundishwa na kocha wake Babu Jonas, aliyemwingiza kwenye mchezo huo na kumpeleka kwenye mapambano ya ridhaa kabla ya kuanza kupigana ngumi za kulipwa.

“Nilikuwa nafundishwa boxing na kocha wangu mmoja anaitwa Babu Jonas. Alinifundisha uboxing, akanipeleka hizi amateur. Nikapigana amateur, baada ya hapo akaniingiza kwenye pro,” anasema Isa.


UBONDIA UNGEMCHELEWESHA

Anasema alipigana mapambano kadhaa katika maeneo ya Manyara, Magomeni na Tandale, lakini kadri alivyokuwa akiendelea na mchezo huo ndivyo alivyogundua kuwa anapenda zaidi kuwa kocha kuliko bondia.

“Mimi mwenyewe tu nikamwambia kocha natamani sana niwe kocha, siyo bondia. Naona ubondia nachelewa kwa sababu natumia muda mwingi kukata mwili, naona bora niwe kocha” anasema Isa.

Anasema kocha wake alishangazwa na uamuzi huo kwa kuwa alikuwa akipigana vizuri, lakini Isa alisisitiza kuwa alitaka kufundisha wengine badala ya kuendelea kupanda ulingoni.

“Akaniambia sasa itakuwaje uwe kocha na unacheza vizuri? Nikamwambia acha tu niwe kocha, nifundishe. Akaanza kunifundisha ukocha, ufanye hivi na hivi. Basi ndiyo hapo nikaanza hivyo hivyo mpaka sasa hivi.”


KILICHOMFUNGUA

Isa anasema pambano dhidi ya bondia aliyemtaja kwa jina la Hamisi ndilo lililobadilisha mtazamo wake kuhusu mchezo huo na kumfanya aupende zaidi ukocha.

“Ngumu nilicheza na mshikaji mmoja hivi anaitwa Hamisi. Ndiyo imenifanya niache ngumi na niupende ukocha. Yaani yeye ndiyo akanifanya mimi niupende ukocha,” anasema.

Anaeleza kuwa baada ya pambano hilo alipata maumivu makubwa, jicho lake likashindwa kuona vizuri kwa wiki nzima na mwili mzima ukawa unauma, hali iliyomfanya akae ndani kwa takribani wiki mbili.

“Ukiona ngumi ni mchezo mmoja hatari sana, nikisema hivyo maana yake ukienda kimungu-mungu unaweza ukafa ulingoni. Ukipigwa ngumi moja, yaani hili jicho sijaona wiki nzima, halafu mwili mzima unauma. Nilikuwa sitoki ndani kama wiki mbili.

“Na mama akaniambia, ulivyovimba hivyo, achana mwanangu na ngumi, fanya kitu kingine,” anasema.


BID 02

USHIRIKINA NA NGUMI

Akizungumzia imani za kishirikina katika mchezo wa ngumi, Isa anasema anaamini kuwa mchezo huo una mambo mengi ambayo mabondia wanapaswa kuyazingatia nje ya ulingo.

“Hamna mchezo ambao una ushirikina kama boxing, kuliko mpira wa miguu. Boxing ni mchezo wa hatari sana, usipokuwa makini unaweza ukapoteza maisha,” anasema.

Anakumbuka pia kusikia taarifa za mabondia waliopoteza maisha au kupata madhara makubwa baada ya mapambano, akitaja tukio alilosikia kuhusu bondia aliyepigwa ngumi ya koromeo katika eneo la Tandale.


BID 03

UKOCHA UNALIPA

Kwa Isa, tofauti kubwa kati ya bondia na kocha ni kwamba bondia ndiye anayeonekana zaidi ulingoni na kupata sifa nyingi, hata pale kocha anapokuwa amechangia kwa kiasi kikubwa ushindi wake.

“Naweza nikakuambia huu ubondia unalipa sana kwa sababu yanayoonekana kwenye ringi ni bondia, na sifa zote anapewa bondia, haipewi kocha. Ila kuna zile zawadi zawadi ambavyo bwana njoo na kocha yako,” anasema.

Anaongeza kuwa mara nyingi bondia ndiye anayenufaika zaidi na matokeo ya pambano, lakini makocha wengi wanaendelea kufanya kazi kwa sababu ya mapenzi yao kwa mchezo huo na dhamira ya kuendeleza vipaji.

“Siyo mara nyingi, ila anafaidika nani? Bondia. Sasa huwa mara nyingi sana sisi makocha hatuangalii kufaidika kwa bondia, tunaangalia ile fani yetu tuiendeleze,” anasema.


KUHUSU MWAKINYO

Miongoni mwa mabondia ambao Isa amepata nafasi ya kufanya nao kazi ni Hassan Mwakinyo, bondia mwenye uzoefu mkubwa katika ngumi za kulipwa. Anasema amekuwa akifanya kazi na Mwakinyo mara kwa mara, hasa pale bondia huyo anapokuwa anajiandaa na pambano na kumhitaji kwa mazoezi maalumu.

“Nilikutana naye kupitia Slim, aliyeniambia nimpigishe pad Mwakinyo ukimwangalia nje anajiamini na haogopi mtu, lakini ukikaa naye ni mtu mzuri, ana roho safi na hana mashauzi kama watu wanavyodhani,” anasema.

Isa anasema anatamani siku moja awe kocha wa kudumu wa Mwakinyo kwa makubaliano rasmi, jambo analoliona kama hatua muhimu katika safari yake ya kitaaluma.

“Napenda sana nije niwe mwalimu wa Mwakinyo kabisa, tusaini mkataba. Ukitaka kuwa maarufu tembea nyayo za Mwakinyo,” anasema.


BID 04

IBRA CLASSIC, MPOLE

Mbali na Mwakinyo, Isa anasema pia amekuwa akifanya kazi na Ibra Classic kwa takribani miezi mitatu.

Anamwelezea Ibra kama mtu mwenye utulivu katika maisha ya kawaida, lakini anayebadilika anapoingia ulingoni na kuanza kupambana na mpinzani wake.

“Ibra ni mpole sana uraiani, lakini ulingoni ni mkali,” anasema.

Isa anakumbuka pambano la Ibra Classic lililofanyika Super Dome dhidi ya bondia kutoka Thailand kuwa miongoni mwa mapambano yaliyompa changamoto akiwa kocha.

Anasema changamoto kubwa ilikuwa kubadilishiwa mpinzani dakika za mwisho, hali iliyowalazimu kufanya marekebisho ya maandalizi yao kwa muda mfupi.

“Pambano la Super Dome dhidi ya Mthailand, kwa sababu tulibadilishiwa mpinzani dakika za mwisho, lakini namshukuru Mungu tulishinda.”


WANAWAKE WANA FURSA KUBWA

Isa anaamini mchezo wa ngumi una fursa za kiuchumi ambazo bado wanawake wengi hawajazichangamkia kutokana na hofu ya madhara yanayoweza kusababishwa na kupigwa ngumi.

“Watu wanauogopa huo mchezo. Wanaogopa kuwa una hatari au unaweza ukawa na matatizo ya kichwa baadaye kutokana na ngumi. Ila si mchezo mbaya, ni mchezo mzuri, unapata pesa. Sasa hivi mchezo wa ngumi una hela hasa kwa wanawake.

“Wana-wake wanaogopa, ila kwa wana-wake ni njia nyepesi sana kupata hela. Akicheza mechi tatu nne tayari zinaingia kwenye BoxRec, ni hela,” anasema.


UJEURI NI ISHU

Kwa Isa, mojawapo ya changamoto zinazokwamisha maendeleo ya ngumi nchini ni tabia ya baadhi ya mabondia kutokuwa na nidhamu baada ya kuanza kutambulika.

“Kwa Tanzania changamoto kwa mabondia ni ujeuri. Akishajulikana anakuwa jeuri na anataka kujiongoza mwenyewe,” anasema.