Massanza: Sikuwahi kuwa shabiki wa soka
Muktasari:
- Hiyo ndiyo safari ya meneja wa habari na mawasiliano wa Singida Black Stars Hussein Masanza, ambaye kabla ya kuingia kwenye soka alikuwa mwajiriwa wa serikali na hakuwa na ndoto ya kufanya kazi katika tasnia hiyo, ingawa kwa sasa ni mtu maarufu sana.
SAFARI ya kuingia kwenye soka si lazima ianze kwa kuwa shabiki wa mpira au kuota siku moja utakuwa sehemu ya mchezo huo. Wakati mwingine, taaluma uliyoisomea ndiyo inaweza kukufungulia mlango wa kuingia kwenye ulimwengu ambao hukuwahi kufikiria ungekuwa sehemu yake.
Hiyo ndiyo safari ya meneja wa habari na mawasiliano wa Singida Black Stars Hussein Masanza, ambaye kabla ya kuingia kwenye soka alikuwa mwajiriwa wa serikali na hakuwa na ndoto ya kufanya kazi katika tasnia hiyo, ingawa kwa sasa ni mtu maarufu sana.
Leo hii, amekuwa sehemu ya safari ya klabu hiyo kutoka Singida Big Stars ya zamani hadi Singida Black Stars, huku akiendelea kupewa imani na uongozi wa timu hiyo katika majukumu ya habari na mawasiliano.
Akizungumzia mwanzo wa safari yake Masanza anasema Singida ndiyo mahali alipoanzia safari yake ya soka na bado anaendelea kuitumikia klabu hiyo.
“Safari yangu kwenye mpira wa miguu ilianzia Singida na mpaka sasa bado inaendelea. Kabla ya kuingia kwenye mpira nilikuwa mwajiriwa wa serikali, lakini kutokana na taaluma yangu ya habari na mawasiliano nilipata nafasi ya kuingia kwenye soka.”
HAKUWAHI KUOTA
Kabla ya kupewa nafasi hiyo, hakuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatilia kwa karibu soka. Hata hivyo, taaluma yake ya habari na mawasiliano ndiyo iliyokuwa sababu ya bosi wake kumfikiria kwa nafasi hiyo.
Anasema alipopata taarifa kuwa anateuliwa kuwa afisa habari, jambo la kwanza lililomjia akilini ni kushangaa, kwa sababu hakuwahi kufikiria kufanya kazi kwenye mpira wa miguu.
“Kwa kweli haikuwa ndoto yangu kufanya kazi kwenye mpira wa miguu. Hata kuwa shabiki wa mpira sikuwa, kwa hiyo nilipoambiwa kuwa nitakuwa afisa habari nilishangaa na nilidhani bosi wangu anatania.
“Nilikuwa mtu mpole kwa asili. Ukiwaangalia maofisa habari wa kipindi kile kama Haji Manara, unajiuliza kama utaweza kuhimili mazingira ya soka, kwa sababu kuna kelele nyingi, majibizano na wakati mwingine tashtiti.”
ZAKA NI MLEZI
Anasema Ali Kamwe alikuwa miongoni mwa watu waliompa moyo na kumtia hamasa nyuma ya pazia. Hata hivyo, mtu aliyemsaidia kuingia vizuri kwenye mazingira ya soka na kumtambulisha kwenye aina ya mawasiliano yaliyokuwa yakitumiwa na maofisa habari alikuwa Zakaria Thabit, maarufu Zaka Zakazi wa Azam FC.
Anakumbuka kuwa moja ya stori zilizomuingiza kwenye mazingira hayo ilihusisha mechi dhidi ya Azam FC na majibizano kuhusu wachezaji wa klabu hiyo kutoka Brazil, akiwamo Bruno Gomez.
“Ali Kamwe alinipa morali sana nyuma ya pazia, lakini mtu aliyenipeleka mjini na kunitambulisha vizuri kwenye soka alikuwa Zaka za Kazi.
“Stori yangu ya kwanza iliyofanya watu waanze kunifuatilia kwenye mitandao ilitokana na majibizano na Zaka kuhusu wachezaji wao wa Kibrasil, akiwamo Bruno Gomez. Baada ya hapo nikaanza kuelewa namna ambavyo unaweza kutumia matukio ya mechi na utani wa kikazi kuwavutia watu.”
ALIJIFUNZA
Anasema mwanzoni baadhi ya watu na waandishi wa habari walikuwa wakimwona kama mtu aliyepoa, huku wakiamini kwamba timu yake ilikuwa na wachezaji wakubwa lakini mawasiliano yake hayakuwa na uchangamfu unaotarajiwa.
“Changamoto yangu ya kwanza ilikuwa kujichangamsha na kujichetua, kwa sababu mimi ni mpole kwa asili. Mwanzoni watu walikuwa wakiniambia nimepoa, wakati timu yangu ina wachezaji wakubwa.
Hata hivyo, kadiri alivyoendelea kufanya kazi, alianza kuelewa kile ambacho soko la soka lilikuwa linahitaji kutoka kwa afisa habari. Akajifunza namna ya kuongeza uchangamfu bila kuingia kwenye migogoro au kuvuka mipaka ya heshima.
“Baadaye nilielewa soko linataka nini. Nikajua ninaweza kuchangamka na kufanya kazi yangu vizuri bila kuvunja heshima yangu wala kugombana na mtu.”
KIZAZI KILICHOBADILISHA LUGHA YA SOKA
Akizungumzia uhusiano wake na maofisa habari wa klabu nyingine, anasema kizazi kilichoingia kwenye majukumu hayo katika kipindi cha msimu wa 2022/2023 kilileta namna mpya ya kuwasiliana na kushirikiana.
“Tumepokea kijiti katika kipindi kinachokaribiana. Kizazi chetu kimebadilisha namna maofisa habari wanavyohusiana. Tunaweza kutaniana kwa sababu ya kazi, lakini nje ya kamera tunashirikiana na tunaelewana.”
ALLY KAMWE, AHMED ALLY
Kuhusu Ali Kamwe, anasema ni mtu anayependa kuona wengine wakifanikiwa na si mwenye tabia ya kujitenga na wenzake. Anasema walikuwa na ukaribu hata kabla Ali hajaingia kikamilifu kwenye majukumu yake ya sasa, alipokuwa mchambuzi wa mpira.
Anakumbuka pia namna Ali alivyokuwa miongoni mwa watu wa kwanza kumpigia simu na kufika wakati wa msiba wa baba yake, Masanza.
“Ali ni mtu wa ushirikiano, si mbinafsi. Anapenda kuona wengine wakifanikiwa. Wakati wa msiba wa baba yangu Masanza alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kunipigia simu na kufika kunipa pole.”
Anasema jambo analolipenda kwa Ahmed ni namna anavyoweza kuzungumza na mtu kwa faragha badala ya kugeuza kila tofauti kuwa mjadala wa hadharani.
“Ahmed ni muungwana sana. Kuna wakati mtu unaweza kufanya jambo ambalo halina taswira nzuri, lakini yeye anaweza kukushauri kwa faragha. Alikuja pia kwenye msiba wa baba yangu na kunipa moyo, kwa sababu naye amewahi kupoteza mzazi.”
SIRI YA UTULIVU WA SINGIDA BLACK STARS
Akizungumzia Singida Black Stars, anasema taswira inayoonekana kwa watu wa nje inaendana na mazingira yaliyopo ndani ya klabu hiyo. Anahusisha utulivu na maendeleo ya timu na namna uongozi unavyowekeza katika klabu na kuhakikisha wachezaji pamoja na benchi la ufundi wanapata mazingira mazuri ya kufanya kazi.
“Kinachoonekana nje ndicho kilichopo ndani. Utulivu unaouona unatokana na uongozi ulio makini, unaowekeza na kuhakikisha wachezaji pamoja na benchi la ufundi wanakuwa na utulivu wa kufanya kazi.”
UWANJA WAKO, UHURU WAKO
Moja ya mambo anayoyataja kuwa faida kubwa kwa Singida Black Stars ni kumiliki uwanja wake. Anasema tofauti kati ya klabu yenye uwanja wake na ile inayotegemea kukodi viwanja ni kubwa, hasa katika kupanga ratiba za mazoezi.
“Utofauti ni mkubwa sana. Ukiwa na uwanja wako unaweza kupanga mazoezi asubuhi, mchana au usiku kulingana na programu ya timu. Lakini kwenye uwanja wa kukodi, kama Gymkhana, wakati mwingine unalazimika kufuata muda uliopangiwa.”
MICHUANO YA KIMATAIFA
Kuwa sehemu ya klabu inayoshiriki michuano ya kimataifa ni hatua nyingine anayoieleza kuwa na maana kubwa katika safari yake ya kazi. Anasema jukumu la afisa habari linakuwa nyeti zaidi kwa sababu timu inapokuwa nje ya nchi, mawasiliano yake yanakuwa sehemu ya namna klabu na Tanzania vinavyowakilishwa.
“Ni fahari kubwa kuwa sehemu ya timu inayoshiriki michuano ya kimataifa, lakini pia kuna presha. Unakuwa kitovu cha taarifa za timu inayowakilisha nchi, kwa hiyo unatakiwa kuwa makini katika namna unavyowasilisha taarifa.”
Akizungumzia malengo ya klabu katika mashindano hayo, anasema hatua ya kwanza ni kufuzu hatua ya makundi kupitia mechi dhidi ya Tusker. Iwapo watafanikiwa kufikia hatua hiyo, wanataka kujiwekea lengo kubwa zaidi la kusonga hadi robo fainali.
“Lengo letu ni kufuzu hatua ya makundi. Tukifanikiwa kufanya hivyo, hatutaki kuishia hapo; tutataka kuthubutu na kupambana ili kufika robo fainali,” anaeleza.
SOKA LA TANZANIA
Anapongeza mchango wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi, vyombo vya habari na Azam Media, akisema namna mechi zinavyorushwa na kufikishwa kwa mashabiki imeongeza nafasi ya soka la Tanzania kuonekana kwa ubora mkubwa zaidi.
“Soka la Tanzania linakua kwa kasi sana. Ligi imekuwa ngumu na ushindani umeongezeka. Hata wachezaji wengi wa kigeni wanaokuja hapa wanapaswa kupambana ili kuendana na kiwango kilichopo.”
KIMOTO MSHINDANI
Anasema Kimoto ni kocha anayechukulia kwa uzito kazi yake ya mazoezi na ana wasifu unaoonesha kuwa amewahi kufika hatua za juu katika mashindano ya Afrika, ikiwamo robo fainali.
“Kimoto ni kocha mtaalamu, analifahamu soka la Afrika na ni mshindani. Ana wasifu unaoonesha kuwa amewahi kufika hatua za robo fainali za mashindano ya Afrika. Pia ni mtu anayechukulia mazoezi kwa uzito.”
USAJILI ULIOWASHANGAZA WENGI
Akizungumzia usajili wa msimu huu, anataja kurejea kwa Jonathan Sowah, kuwa miongoni mwa hatua zilizovuta hisia za watu wengi. Anasema baadhi ya watu walikuwa na mtazamo kwamba mchezaji huyo hakufanikiwa alipokuwa Simba, hivyo kurejea kwake kulizua mjadala.
“Sowah nje ya uwanja ni kama malaika. Ni mpole, anapenda amani na anaishi vizuri na kila mtu. Lakini ukiwa uwanjani, kuna wakati hasira zinaweza kupanda kutokana na matukio ya mchezo.”
OFA NYINGI
Hata hivyo, anasema wakati fursa hizo zilipojitokeza tayari alikuwa ameshasaini mkataba na Singida, kipindi ambacho klabu hiyo ilikuwa bado inajulikana kama Ihefu.
“Nilipata maombi kutoka kwa klabu mbalimbali wakati wa mabadiliko yaliyokuwa yakitokea. Hata kocha mmoja aliyeenda kufundisha Ujerumani alitaka kunijumuisha kwenye timu yake, lakini tayari nilikuwa nimeshasaini mkataba na Singida.”
SIMBA NA YANGA
Anasema hata hivyo, maandalizi ya Singida Black Stars yanahusisha kuwa na wachezaji wenye uzoefu wa mechi kubwa, jambo linaloweza kusaidia timu kukabiliana na mazingira ya ushindani.
“Mechi za Simba na Yanga zina presha kubwa sana kwa sababu zina mashabiki wengi kila kona ya nchi. Lakini sisi pia tuna wachezaji wenye uzoefu wa kucheza mechi kubwa, kwa hiyo tunatakiwa kujiandaa vizuri na kuingia uwanjani kupambana.
“Malengo yetu ni kupambana ili kupata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao. Tunajua si jambo rahisi, lakini tunatakiwa kuendelea kufanya kazi na kupambana.”