Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mo Dewji amechafua hali ya hewa

Muktasari:

  • Mo Dewji amesema Sh20 bilioni alizitoa kwa ajili ya kununua asilimia 49 ya hisa za umiliki wa klabu hiyo baada ya kukamilika mchakato wa mabadiliko ya kimuundo na umiliki. Fedha hizo zilitokana na tathmini ya thamani ya Simba na mambo mengine ya kibiashara.


KWA mara nyingine mwekezaji wa Simba, Mohamed ‘MO’  Dewji ameibuka tena kuzungumzia ufadhili kwa klabu hiyo kongwe, akisema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017 ameshatoa zaidi ya Sh80 bilioni kwa ajili ya shughuli mbalimbali.


Mo Dewji amesema Sh20 bilioni alizitoa kwa ajili ya kununua asilimia 49 ya hisa za umiliki wa klabu hiyo baada ya kukamilika mchakato wa mabadiliko ya kimuundo na umiliki. Fedha hizo zilitokana na tathmini ya thamani ya Simba na mambo mengine ya kibiashara.


Zililenga kuiwezesha klabu hiyo kuwa na uwezo wa kifedha na kujiendesha kisasa. Pia amesema alitoa Sh22 bilioni kwa ajili ya mambo mengine mbalimbali ya dharura na changamoto zinapotokea.

Anasema kwa ujumla ameshatoa Sh87 bilioni, hivyo anashangazwa na kauli za watu wanaosema hatoi fedha, akisema ni za upotoshaji.

Ametoa kauli hiyo baada ya kumalizika kwa msimu ambao mabingwa hao wa zamani wametoka mikono mitupu hasa baada ya kukosa tena  taji la Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA) na Kombe la Shirikisho Afrika.

Amesema hayo katika kipindi ambacho mashabiki wanamlaumu mwenyekiti wa klabu, Murtaza Mangungu wakimhusisha na kutofanya vizuri kwa timu hiyo yenye makazi Mtaa wa Msimbazi.

Mtu anajiuliza, kwa nini Mo Dewji ameyasema hayo leo wakati klabu hiyo ina Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) anayetakiwa azungumzie masuala yote ya uendeshaji, ikiwa ni pamoja na michango, misaada na fedha za udhamini baada ya kumalizika kwa msimu?

Katikati ya hasira za kukosa mafanikio, mashabiki na wanachama ni lazima watachukulia kuwa tatizo kubwa kwa Simba ni viongozi, hasa wale wasio mabilionea au wasio na ukaribu naye, kwamba ndio wanamkwamisha mwekezaji.

Ukichanganya na usajili ambao haujafanya vizuri, ndio kabisa mashabiki na wanachama wataamini kuwa fedha hutolewa kwa ajili ya kununua wachezaji wenye ubora wa kuweza kupambana Afrika, lakini viongozi wanachukua asilimia na kununua wachezaji wasio na viwango.

Ni dhahiri kuwa kauli ya Mo Dewji inachongea viongozi wa Simba kuwa hawawajibiki ipasavyo, licha ya kutoa fedha kila wanapohitaji, iwe kwa maombi ya muda mrefu au kwa dharura.

Lakini swali ni kwanini anaendelea kutoa fedha baada ya kutoa Sh20 bilioni za kukuza mtaji wa Simba ili isimame imara kiuchumi naye abakie kusubiri faida?

Tumeona familia ya Glazer ambayo iliinunua Manchester United inavyopata faida kibiashara licha ya klabu hiyo kutopata mafanikio kwa muda mrefu na kukosa kushiriki mashindano kama Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ambayo yana fedha nyingi.

Kwa mujibu wa New York Times, familia hiyo imejipatia zaidi ya Pauni 128 milioni za Kiingereza za gawio linalotokana na faida ambayo klabu hiyo imekuwa ikipata. Fedha hizo hulipwa familia hiyo hata wakati ambao klabu imechukua mkopo. Familia hiyo pia imepata Pauni 1.2 bilioni zinazotokana na mauzo kwenye masoko ya hisa, wakati Pauni 27.4 milioni zilitokana na ada za menejimenti.

Pia familia hiyo hupandisha thamani ya klabu na hivyo hisa za Manchester United kuuzwa kwa bei kubwa kwenye masoko ya hisa, huku ikinufaika na uwezo wa kupata mikopo kama ilivyofanywa wakati wa kuinunua klabu hiyo.

Huu ndio uwekezaji unavyotakiwa kufanyika. Yaani mwekezaji aone thamani ya kuwekeza na kuweka mikakati ya jinsi ya kunufaika na uwekezaji wake na si kutwaa makombe.

Kwa maana nyingine ni kwamba tangu Dewji atoe Sh20 bilioni hakuna fedha ambayo imewahi kurudi kwake kama mwanahisa. Yaani hata wale wa vyama vya kuweka na kukopa (Saccos) huwa tunapata angalau Sh100,000 kama faida kutokana na hisa zetu. Iweje klabu kubwa kama Simba isiweze kurejesha faida baada ya mwekezaji kutumbukiza Sh20 bilioni?

Kwa kipindi cha miaka takribani minane, Simba imekuwa ikifanya vizuri ndani ya nchi na kimataifa.Licha ya kukosa ubingwa kwa misimu minne mfululizo, bado imekuwa ikiishia hatua za juu katika mashindano ya kimataifa na hivyo kukuza chapa (brand) yake kimataifa, jambo linaloongeza thamani ya klabu.

Inakuwaje basi klabu kama hiyo iendelee kutembeza bakuli kwa mwekezaji wakati ina kila kitu cha kuiwezesha kujitegemea? Imeingia mikataba mingi inayoonyesha itajipatia fedha nyingi kupitia mauzo ya bidhaa zake kama jezi na vitu vingine. Mikataba ya udhamini kama M-Bet, ambaye ni mdhamini mkuu, huku bidhaa za Mohamed Enterprises Limited (MeTL) zikitamalaki kwenye jezi za Wekundu hao.

Ukichanganya na haki za televisheni na vyanzo vingine kama mitandao ya kijamii, mapato ya mlangoni, zawadi za wadhamini wao na wa mashindano ya ndani na kimataifa na kodi za pango, huoni sehemu menejimenti ikilazimika kwenda kutembeza bakuli hadi zifikie Sh87 bilioni.

Kwa mujibu wa taarifa za klabu hiyo, Simba ilipanga kutumia Sh28 bilioni kwa msimu wa mwaka 2024/25. Fedha hizo zingetokana na udhamini wa Simba TV (Sh3.3 bilioni, haki za matangazo (Sh480 milioni), kodi ya pango (Sh500 milioni),  Kombe la Shirikisho (Sh508 milioni, ada za uanachama (Sh1.4 bilioni), Simba Day (Sh494 milioni), kuuza wachezaji (Sh500 milioni) na Sh400 milioni kutoka Simba App.

Pia Simba ilisema ilitarajia kupata Sh2.9 bilioni kutoka kwa mdhamini mkuu, wakati Sh1.5 bilioni zingetoka kwa mdhamini wa jezi, Sh155 milioni kutoka kwa mdhamini wa Ligi Kuu, Sh500 milioni kutoka kampuni ya Serengeti, Sh250 milioni kutoka kampuni ya A1 na Sh250milioni 250 kutoka vyanzo vingine.

Hiyo ni taarifa rasmi kutoka kwa uongozi wa Simba baada ya kuwasilisha bajeti yao kwenye mkutano mkuu. Ni wapi walifeli hadi wakalazimika kuomba fedha.

Pamoja na matarajio ya kuingiza fedha hizo, Mo Dewji aliwaambia wanachama kwenye mkutano huo kuwa tayari ameshatoa Sh7 bilioni ambazo zilianza kutumika kusajili wachezaji. Ndipo utata unapoanzia. Yaani msimu wa 2023/24 walimaliza bila fedha zozote hadi wakalazimika kuomba kwa mwekezaji ili wasajili?

Msimu wa 2022/23 Simba ilikuwa na bajeti ya kutumia Sh15 bilioni na msimu wa 2023/24 ilipanga kutumia Sh25 bilioni na vyanzo vya mapato havitofautiani sana, lakini mwishoni mwa msimu inakuwa kama klabu inamaliza bila ya hata senti tano. Unawezaje kuwa uwekezaji?

Hapo huoni kama klabu inaweza kuhitaji msaada wa zaidi ya Sh1 bilioni kwa msimu mmoja kama bajeti hizo na vyanzo, ambavyo vingi ni vya uhakika, vikawa na hivyo. Ninachoona labda kuna tatizo.

Tangu Simba ifanye mageuzi hakuna kitu kikubwa kinachoonekana katika muundo au utendaji wa shughuli za kila siku. Kilichoongezeka ni idadi ya viongozi wanaoweza kuzungumzia kila kitu, huku menejimenti ikionekana kuwa na kazi ya kurekodi matukio na si kuingiza ubunifu wa kuboresha vyanzo vya mapato na ufanisi katika utendaji.

Kama Mo Dewji ni mwekezaji, iweje awe ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu? Yaani awajibike kwake mwenyewe? Mwenye hisa nyingi, ambaye kwa utaratibu uliopo ni klabu, ndiye alitakiwa ateue Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kama ilivyo katika mashirika mengine makubwa.

Kwenye mkutano mkuu wa klabu, unategemea Mwenyekiti wa Bodi aende kutoa taarifa ya jinsi walivyoendesha klabu, kama kuna faida na hasara na kueleza matarajio yao ya msimu unaofuata. Hapo mwekezaji na klabu zinakuwa kama wanahisa ambao kazi yao ni kusikiliza kile kilichofanyika.

Na bodi ya wakurugenzi inakuwa imepata taarifa ya utendaji wa shughuli za kila siku kutoka kwa CEO, ambaye kwa kawaida huwa ndio kiongozi wa menejimenti.

Lakini mwekezaji anapokuwa mwenyekiti wa bodi halafu ndiye anayeongoza vikao vya bodi na wanahisa, kunakuwa hakuna utawala bora wala uwajibikaji. Na kwa maana hiyo hakuna wa kumlaumu mwingine.

Kwa kifupi, Mohamed Dewji ametuchanganya. Ni dhahiri kuwa hakuna atakayeweza kujitokeza na kupingana na alichosema labda yule CPA Issa Masoud ambaye aliwahi kuhoji fedha zinazotolewa na mwekezaji huyo.

Na wakikaa kimya maana yake watazua mijadala. Mo Dewji anaonekana anatoa fedha, lakini viongozi wanazitumia vibaya.

Ni vyema Simba ikawa na mfumo mzuri wa utoaji taarifa ambao unadhibiti viashiria vya kuvurugana. Kwa kifupi ni kwamba kwa kauli ya Mo Dewji ni kama amechafua hali ya hewa kwa sasa.

Mwandishi wa Makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa TFF na mchambuzi mkongwe wa soka.