Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mimba, kipingamizi ndoto za wachezaji wa kike

MIMBA Pict

Muktasari:

  • Ripoti ya FIFPRO ya mwaka 2017, kifungu cha 40 (9), ilieleza asilimia 61 ya wachezaji waliokuwa na watoto hawakupata msaada wa malezi, huku asilimia nane walipewa malipo ya likizo ya uzazi na klabu au mashirikisho ya kitaifa.

UCHUNGUZI unaonyesha baadhi ya wanasoka wa kike kushindwa kuendelea kuzipambania ndoto zao kutokana na kupata ujauzito na kutorejea baada ya kujifungua, imetajwa elimu ndogo, malezi na viongozi  wa timu kutowahitaji tena.

Ripoti ya FIFPRO ya mwaka 2017, kifungu cha 40 (9), ilieleza asilimia 61 ya wachezaji waliokuwa na watoto hawakupata msaada wa malezi, huku asilimia nane walipewa malipo ya likizo ya uzazi na klabu au mashirikisho ya kitaifa.

Hapa nchini, miongoni mwa hao ni kiungo mshambuliaji Sabahi Hashim Yusuff. Anasimulia baada ya kupata mimba mwaka 2019 akiwa na Kigoma Sisters viongozi wa timu hiyo walimfuta kwenye usajili hivyo akaamua kurejea kwao Zanzibar bila kuambulia kitu chochote.

Japokuwa wakati Sabahi anapata mimba ya kwanza ilikuwa bado haijapitishwa sheria ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) ya Ibara ya 18 (7) ya mwaka 2020 na kuanza kutumika Januari 1, 2021, inayompa mchezaji mwanamke haki ya likizo ya uzazi ya angalau wiki 14 pamoja na malipo ya theluthi mbili ya mshahara wake wa mkataba.

MIMB 01

Anasimulia "Niliolewa mwaka 2017, wakati timu inanisajili ilikuwa inajua mimi ni mke wa mtu, suala la familia siyo la upande mmoja, sikukaa na viongozi mezani ili angalau tujadiliane mkataba wa mwaka mmoja ambao ulikuwa umebakia, maana nilisaini mkataba wa miaka miwili, hivyo nikaamua kurudi nyumbani kwa mume wangu Zanzibar," anasema Sabahi.

"Nilipogundua nina mimba nilimwambia aliyekuwa kocha wa timu Lawrence Siang'a (marehemu), aliniambia wewe ni mke wa mtu suala la kuanzisha familia halikwepiki, ingawa alipowaambia viongozi walimwambia sitakuwa sehemu ya kikosi hicho, nifutwe kwenye mfumo wa usajili."

Anasema alisajiliwa na Magereza Queens ya Zanzibar kuanzia 2024-2027 baada ya kupata mimba akaondolewa katika timu hiyo bila kupata chochote na hapo sheria ya FIFA ilianza kutumika.

MIMB 02

"Nina watoto watatu, mtoto wangu wa pili nilizaa nikiwa sina timu, wakati uongozi wa Magereza Queens unakuja kuhitaji huduma yangu ulijua nina mume na watoto wawili, lakini baada ya kupata mimba nikiwa na timu yao, walinifuta kwenye usajili hadi sasa nimejikatia tamaa labda nisome ukocha ambao hautakuwa na vikwazo hivyo," anasema na kuongeza;

"Kuna wengine baada ya kupata mimba ya kwanza walikata tamaa wamerudi vijijini, maisha yao ni magumu na hawataki kusikia chochote kuhusu ulimwengu wa soka, lakini wapo wanaosema hawawezi kuzaa maana soka ndiyo sehemu yao ya kujipatia kipato cha kuzisaidia familia zao maana wanajua wakipata mimba inakuwa ndiyo mwisho wa ndoto zao."

Mwingine ni beki wa zamani wa Tanzanite Queens, Lilian Oswald Shirima mwenye umri wa miaka 26, anasema mwaka 2020 akiwa na timu hiyo, alipata changamoto ya kuuguliwa na mama yake mzazi, hivyo aliomba ruhusa ya kuondoka kambini ili akashughulikie hilo, lakini akajikuta anapata mimba akiwa mtaani.

MIMB 04

"Wakati naondoka kambini nilikuwa na mkataba wa miaka mitatu na nilikuwa sina mimba, ilinichukua muda mrefu kumuuguza mama, nikajikuta nabeba ujauzito na sikuona sababu ya kuitoa, baada ya kujifungua nilitaka nirejee kwenye timu ikawa imeuzwa, hivyo nikawa nimeendelea kusalia nyumbani hadi nikapata mtoto wa pili," anasema Lilian na kuongeza;

"Mbali na mimi nina marafiki zangu ambao baada ya kuzaa na waliowazalisha kukataa majukumu, wakajikuta wanaolewa na watu ambao hawakuwatarajia kisa wameamua kuwasaidia maisha, hilo jambo linaumiza na viongozi wa timu wajaribu kuangalia namna ya kulinda haki za msichana, maana hatuna elimu kubwa wengi wetu tumeishia kidato cha nne."

Winga wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya umri chini ya miaka 17 (U-17), Happy Nicco baada ya kuzaa ameshindwa kuendelea na soka, anawaza ni kitu gani anaweza akafanya kwa ajili ya kuendesha maisha yake.

MIMB 05

Happy amewahi kuzichezea Kigoma Sisters Panama Girls FC ya Iringa na JMK Queens anasimulia: "Septemba 2023 nilikuwa nimeenda kufanya majaribio Yanga Princess yalikuwa ya wiki tatu, nilifanya kwa wiki mbili nikajikuta najisikia kuchoka kusikokuwa kwa kawaida nikaenda hospitali kujua tatizo ni nini ndipo nilipoambiwa nina mimba.

Anaongeza: "Kwa sababu nilikuwa bado sijasaini mkataba na Yanga Princess ilinibidi nirudi nyumbani kwetu Chimala, Mkoa wa Mbeya na nilijifungua mwaka 2024, tangu hapo nipo mtaani ukizaa inakuwa ngumu timu kukupa nafasi ya kucheza."

Mchezaji mwingine ambaye hakutaka kuweka jina lake wazi anasema, baada ya kupata mimba timu aliyokuwa anaichezea jijini Dar es Salaam ilimfukuza kazi akiwa amebakiza mkataba wa miaka miwili, hivyo akarejea mkoani kwao Mwanza.

MIMB 06

"Baada ya kujifungua nilipitia hali ngumu ya kimaisha, wazazi wangu waliniambia ulikataa shule ulichagua soka na umerudi na mimba badala ya pesa ya kukujenga kimaisha tumekulea wewe unataka tena kutupa mzigo mwingine wa kulea mtoto wako, wakati napitia changamoto hiyo iliyofanya nijute kucheza soka nikakutana na mwanaume ambaye alinipenda na kuamua kubeba majukumu ya mtoto wangu, nimefunga naye ndoa ndiyo maana sitaki jina langu liwe wazi, asije akaona bado namuwaza mwanamume aliyenitelekeza."

Kiungo Zuwena Aziz 'Zizou' ambaye msimu uliopita wa 2025/26 aliichezea timu ya Mogbwemo Queens ya Ligi Kuu ya Wanawake Sierra Leone anazungumzia uzoefu wake wa kuwaona wachezaji wenye umri mdogo walipopata mimba hadi sasa wamepotea kwenye ramani ya soka.

Zizou aliyewahi kuzichezea Baobab Queens Uzuri Queens Evergreen Queens Ceasiaa Queens Tausi FC kwa timu za nje Thika ya Kenya Nahaj Souss ya Morocco Lady Doves FC ya Uganda na Mogbwemo Queens ya Sierra Leone anasema: "Binafsi nikitaka kuzaa inabidi niwe tayari kukaa nje ya kazi, kwani nimeona wasichana ambao waliingia kwenye soka wakiwa na umri wa miaka 19, 20 hadi 21 walipopata mimba ndoto zao zimekufa na wamerejea vijijini kwao, wengine baada ya hapo wameenda kuolewa na wazee ili mradi tu wapate hifadhi.

MIMB 07

Anaongeza: "Siyo Tanzania pekee nimeona hata Sierra Leone inavyokuwa ngumu kwa mwanamke kuendelea na majukumu akipata mimba, asilimia kubwa mikataba ambayo tulikuwa tunasaini na timu haina kipengele cha ulinzi wa kuendelea kusalia kwenye timu inapofika wakati huo.

"Hicho kipengele cha FIFA angalau kimetupa nguvu ya kuamini katika kujenga familia, kuliko kujiona ukiwa mchezaji unaweza ukafa bila kuacha mtoto duniani, kwani unaweza ukapata mtu ukipata mimba anakwambia sipo tayari kuoa mchezaji."

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Twiga Stars', Mwanahamis Omary 'Gaucho' anasema wachezaji wengi wa kike ambao wamepata mimba wamerejea vijijini na kuzima ndoto za kuwa wachezaji wakubwa, wachache ambao wamepata wenza waelewa ndio waliyorejea kazini.

MIMB 08

Staa huyo aliyeichezea Tausi FC msimu uliopita wa 2025/26 akitarajia kurejea uwanjani kupitia usajili wa dirisha dogo la 2026/27 anasema: "Wachezaji wa kike tunadharauliwa ukipata mimba wanakuchukuliwa kama veterani hufai kucheza tena, jambo ambalo linaloumiza akili zetu angalau wanahabari mnapotupa muda wa kuzungumza tunatoa vinyongo tulivyonavyo na huenda mamlaka za mpira wa miguu za ndani zikitusikia vilio vyetu, ili zitatunga sheria zinazoendana na za FIFA zitakazotupa haki za kuwa na familia.

Anaongeza: "Tofauti na Ulaya wenzetu wakiwa wajawazito unawaona wachezaji wanafanya mazoezi mepesi na timu, ila huku kwetu ikitokea mchezaji kapata mimba na aombe isiwe ya kiongozi basi huyo ataondolewa kabisa kwenye ramani ya mpira wa miguu.

"Changamoto, kuna wanaume wanaokuja kwenye maisha ya mchezaji wa kike kwa tamaa ya kulala naye, siyo kuanzisha familia ikitokea akapata mimba anajikuta timu haimtaki baba mtoto wake hayupo tayari kwa majukumu, hilo linatuogopesha wengi wetu, hivyo tunaamua kutafuta kwanza maisha hata ikitokea umepata mimba basi iwe rahisi kulea mtoto wako kuliko kuingia kwenye msongo wa mawazo".

MIMB 09

Mwanahamisi aliyewahi kuichezea Shabab Atlas ya ligi kuu ya Morocco na hapa nchini Simba Queens, Uzuri Queens anasema: "Kuna wachezaji ambao umri wao ni miaka 19, 20, 21 walipopata mimba walirejea vijijini kwao na kila kitu kiliishia hapo laiti wangepata uelewa wa mapema kuhusiana na sheria ya FIFA huenda kungekuwa na watu ambao wangewasimamia kupata haki zao."


KIMATAIFA

Siyo Tanzania pekee, taarifa iliyotolewa na FIFPro Juni 24, 2026 timu ya Lazio Women ya Italia, iliamuriwa  kulipa fidia kwa kiungo wao wa zamani Maja Gothberg kwa sababu kumfutia ajira yake kinyume cha sheria kutokana na ujauzito.

Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) iliamua kusimama upande wa mchezaji huyo wa Sweden, katika kesi ya uzazi ambayo umoja wa kimataifa wa wachezaji FIFPro uliiita 'ya kihistoria' pia iliamuru kuwa mchezaji huyo atapokea fidia ya madhara ya kimaadili, kutokana na klabu hiyo kufichua taarifa kuhusu ujauzito wake kwa wachezaji wenzake bila ridhaa yake.

"Kesi hiyo haikuhusu soka pekee, bali kutendewa kwa haki na kwa heshima katika wakati muhimu wa maisha yangu," anasema Gothberg na kuongeza;

"Uamuzi huu unatuma ujumbe ujauzito haupaswi kamwe kuchukuliwa kama tatizo au sababu ya kumnyima mchezaji fursa za ajira."

Mgogoro huo ulipelekwa CAS baada ya kesi ya Gothberg kukataliwa awali na Chumba cha Utatuzi wa Migogoro cha FIFA (DRC).

Baada ya maamuzi ya hukumu hiyo, uongozi wa Lazio, ulisema utaendelea kujitolea kwa dhati kulinda haki na ustawi wa wanamichezo wake na kuendeleza misingi ya ujumuishaji heshima usawa na kutobagua ambayo ni ya msingi kwa maendeleo endelevu ya soka la wanawake.

"Klabu itaendelea kupitia na kuimarisha taratibu zake za ndani ili kuhakikisha zinaendana kikamilifu na mfumo wa kanuni za kitaifa na kimataifa unaoendelea kubadilika unaosimamia michezo ya kitaaluma na mahusiano ya ajira."

Gothberg alikuwa na msimu mzuri wa 2023/24 akiwa na Lazio Women na beki huyo wa Sweden aliisaidia klabu kupata nafasi ya kupanda hadi ligi kuu ya Italia

Katika majira ya joto ya 2024 Gothberg na Lazio Women waliingia katika mazungumzo kuhusu mkataba mpya, ingawa hakuna makubaliano yaliyosainiwa pande zote mbili zilibadilishana mawasiliano mengi na kukubaliana kuhusu masharti muhimu ya mkataba mpya.

Kesi hiyo pia inaonyesha umuhimu wa ushahidi wa maandishi katika migogoro ya kisasa ya soka kwa kuwa hakukuwa na mkataba uliosainiwa, ujumbe wa WhatsApp ukawa muhimu katika kuthibitisha uwepo wa uhusiano wa ajira na ufahamu wa klabu kuhusu ujauzito wa Gothberg, ilitumika kama ushahidi kamili nia CAS.

Julai 23,2026, mwandishi wa BBC Sport Africa, Emmanuel Akindubuwa alimzungumza na mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Nigeria, Ngozi Okobi Okeoghene, aliyesema licha ya mashabiki kumkosoa mitandaoni baada ya kufunga ndoa na mfanyabiashara wa masuala ya nyumba na ardhi, Ahmed Okeoghene, Desemba 9, 2017 katika Jimbo la Delta, bado anaamini haiwezi kuwa kikwazo katika kazi yake.

Ngozi mwenye umri wa miaka 32 alibahatika kupata mtoto wake wa kwanza wa kiume 2024 katika mahojiano hayo anasema: "Mashabiki wengi wanaamini mwanamke anapoolewa anakuwa mzee, mwanamke akijifungua wanaona hana  nguvu ya kufanya kile alichokuwa akifanya.

Anaongeza: "Tatizo hilo limekuwa kubwa kiasi cha kuathiri hata maamuzi ya wachezaji wengine, wanatufanya tujisikie vibaya kuhusu sisi wenyewe, wasichana wengi wanaogopa kuolewa kwa sababu wanafikiri wakiolewa hawataitwa tena kwenye timu ya taifa."

Ngozi anayeitumikia Ottawa Rapid FC ya Ligi Kuu ya Wanawake Canada, kabla ya ligi hiyo aliwahi kukipiga Levante Badalona ya Hispania, Washington Spirit ya Marekani na klabu mbalimbali duniani: "Ni kitu kibaya kumuonyesha mwanasoka wa kike kuchagua kati ya familia na soka, tunapaswa kupewa sapoti kubwa na kuondoa uwoga waliyonao wanawake wengine kuolewa na kuzaa watoto."

Itaendelea kesho