Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matano usiyoyajua kuhusu Kombe la Dunia U-17

U-17 Pict

Muktasari:

  • Kuanzia mafanikio ya Ronaldinho akiwa kijana hadi ubabe wa Nigeria katika mashindano hayo, historia ya Kombe la Dunia U-17 imejaa matukio ya kuvutia na rekodi zilizodumu kwa miaka mingi.

Mashindano ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17 (U-17) yamekuwa chimbuko la baadhi ya nyota wakubwa wa soka duniani, yakizalisha vipaji vilivyokuja kutamba katika medani ya kimataifa na kuweka rekodi za kipekee tangu yalipoanzishwa mwaka 1985.

Kuanzia mafanikio ya Ronaldinho akiwa kijana hadi ubabe wa Nigeria katika mashindano hayo, historia ya Kombe la Dunia U-17 imejaa matukio ya kuvutia na rekodi zilizodumu kwa miaka mingi.

Mwaka huu, mashindano hayo yanafanyika nchini Qatar kwa mara ya pili mfululizo, ikiwa ni sehemu ya mfumo mpya wa uendeshaji wa michuano hiyo. Haya hapa ni mambo matano ya kuvutia ambayo huenda hukuyafahamu kuhusu mashindano hayo.


U- 01

REKODI YA VICTOR OSIMHEN

Kabla ya kujitengenezea jina kubwa kama mmoja wa washambuliaji wanaotambulika duniani, Victor Osimhen aliweka historia ya kipekee katika Kombe la Dunia U-17 mwaka 2015.

Mshambuliaji huyo wa Nigeria alifunga mabao 10 katika michezo saba, akiiongoza nchi yake kutwaa ubingwa wa tano katika mashindano hayo.

Miongoni mwa mabao hayo ni lile alilofunga katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mali kwenye mchezo wa fainali.

Mafanikio hayo yalimfanya avunje rekodi ya mabao tisa iliyokuwa ikishikiliwa kwa pamoja na Florent Sinama Pongolle na Souleymane Coulibaly.

Jambo la kuvutia ni kwamba, zaidi ya miaka 10 baadaye, rekodi hiyo ya Osimhen bado haijavunjwa.


U- 02 (1)

MOROCCO YAWEKA REKODI

Moja ya matokeo yaliyovutia zaidi katika historia ya mashindano ya FIFA yalitokea kwenye Kombe la Dunia U-17 mwaka 2025 nchini Qatar.

Morocco iliichakaza New Caledonia kwa mabao 16-0 katika mchezo wake wa mwisho wa hatua ya makundi, ikiweka rekodi ya ushindi mkubwa zaidi katika historia ya mashindano yote ya Kombe la Dunia yanayoandaliwa na FIFA.

Morocco ilifunga mabao saba katika kipindi cha kwanza na kuongeza mengine tisa baada ya mapumziko, huku New Caledonia ikimaliza mchezo ikiwa na wachezaji tisa uwanjani.

Matokeo hayo yalivunja rekodi ya ushindi wa mabao 13-0 iliyowekwa na Hispania dhidi ya New Zealand katika Kombe la Dunia U-17 mwaka 1997, ambayo baadaye ililinganishwa na Marekani ilipoifunga Thailand katika Kombe la Dunia la Wanawake mwaka 2019.


U- 04

RONALDINHO ALIKUWA BINGWA KABLA YA UMAARUFU

Muda mrefu kabla ya kutwaa tuzo ya Ballon d'Or na kubeba Kombe la Dunia la wakubwa, Ronaldinho alikuwa tayari amekuwa bingwa wa dunia akiwa na Brazil katika ngazi ya vijana.

Nyota huyo wa Brazil alisaidia nchi yake kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia U-17 mwaka 1997 nchini Misri, akifunga mabao mawili katika mashindano hayo, huku Brazil ikiifunga Ghana mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali.

Ronaldinho si nyota pekee aliyepitia mashindano hayo kabla ya kujipatia umaarufu mkubwa duniani. Wengine ni Neymar, Toni Kroos, Cesc Fabregas, Xavi na Gianluigi Buffon.


U- 02

NIGERIA YATWAA MATAJI MENGI KULIKO BRAZIL

Ingawa Brazil ndiyo nchi iliyofanikiwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia la wakubwa kwa wanaume, Nigeria ndiyo inayoongoza kwa idadi ya mataji katika mashindano ya vijana chini ya miaka 17.

Kikosi cha Nigeria kinachofahamika kwa jina la Golden Eaglets kimetwaa ubingwa mara tano, katika miaka ya 1985, 1993, 2007, 2013 na 2015.

Cha kuvutia zaidi, Nigeria ndiyo iliyokuwa bingwa wa kwanza wa mashindano hayo mwaka 1985 nchini China, baada ya kuifunga Ujerumani Magharibi mabao 2-0 katika fainali iliyohudhuriwa na takribani watazamaji 80,000.

Brazil inashika nafasi ya pili ikiwa na mataji manne, huku Ghana na Mexico zikifuata zikiwa na mataji mawili kila moja.


U- 05

QATAR MWENYEJI WA MIAKA MITANO

Tofauti na Kombe la Dunia la wakubwa ambalo hufanyika kila baada ya miaka minne katika nchi tofauti, mashindano ya U-17 yameingia katika mfumo mpya wa uendeshaji.

Qatar imepewa haki ya kuandaa matoleo matano mfululizo ya mashindano hayo kuanzia mwaka 2025 hadi 2029, ikiwa nchi ya kwanza kupewa jukumu hilo chini ya mfumo mpya wa michuano hiyo kufanyika kila mwaka.

Aidha, idadi ya timu zinazoshiriki imeongezwa kutoka 24 hadi 48 kuanzia mwaka 2025, huku kila toleo likipangwa kuwa na jumla ya michezo 104.

Mfumo huo mpya unaifanya Qatar kuingia katika historia ya mashindano hayo kwa kuwa mwenyeji wa matoleo matano mfululizo, kuanzia 2025 hadi 2029.