Prime
Maswali tata tuzo za TFF 2023
GUMZO la tuzo za Ligi Kuu bado halijaisha kutokana na mambo mengi ambayo yalitokea pale mkoani Tanga.
Ni jambo zuri kuona tuzo zinatolewa na wachezaji kadhaa wanashinda tuzo hizo, pongezi kwa waandaaji kwa kuwa tofauti na miaka mingine mingi msimu huu tuzo zimefanyika kwa wakati mzuri.
Misimu kadhaa iliyopita ilikuwa ngumu kumuona mwenye tuzo anakwenda mwenyewe kuchukua, lakini kwa msimu huu mambo mengi yalionekana kuwa mazuri na wengi wanaohusika na tuzo walikwenda jukwaani kwa ajili ya kupokea.
Hata kama walikosekana basi kulikuwa na wawakilishi ambao waliokuwa familia ya wahusika, mfano tuzo ya Fiston Mayele alipokea mke wake jambo ambalo lilionekana kunogesha zaidi tuzo hizo.
Lakini pamoja na mazuri hayo, bado maswali yanaendelea kuwa mengi kuhusu tuzo hizo, kauli baadhi zinaleta ukakasi zaidi kuhusu mustakabali wa tuzo hizo kwa misimu kadhaa ijayo.
Kanuni
Kitendo cha kumalizika kwa ligi na kuwaacha na maswali mashabiki wa soka juu ya nani anastahili kuwa mfungaji bora baada ya Saido Ntibazonkiza na Fiston Mayele ni jambo ambalo lilileta ukakasi mkubwa kuhusu kamati na wengi kuona kuwa walikuwa hawajajipanga vizuri kuhusu jambo hilo.
Moja inawezekana kamati ilifanya jambo hilo ili kuwafanya mashabiki wa soka kuwa makini kusubiri kuhusu tuzo hizo, lakini ukweli ni kwamba kuna jambo la kujifuza hapa.
Kanuni za Ligi Kuu Bara ni jambo ambalo shabiki au ndau wa soka akitaka kulifahamu alipate kwa wakati, lisiwe jambo la siri ambalo watu wachache ndiyo wanalifahamu.
Kama inavyojulikana ni kwamba kila klabu inatakiwa kuwa na kanuni kabla ya mashindano, kama ni hivyo tukubaliane kwamba kulikuwa na shida kwenye suala la kanuni ya ufungaji bora, kwa kuwa Simba waliokuwa na mchezaji wao kwenye vita hivyo pamoja na Yanga wote walikuwa gizani nao walikuwa wanabishana kama mashabiki.
Hivyo hili liwe funzo, kwamba kanuni za msimu ujao zitengenezwe kwenye mazingira ya wazi ya kila mmoja kufahamu kitu flani kinasemaje na kwanini ili kuondoka hali hii.
Ukitaka kupata kanuni ya ligi yoyote kubwa duniani ni rahisi kuipata basi ni vizuri na kwetu hali hiyo itokee ili tubadilike na kwenda na wakati.
Kauli ya rais wa TFF Wallace Karia kuwa ni vyema kanuni zikabadilishwa kwa kuwa msimu huu kuna watu zimewanyima furaha nafikiri ni pamoja na hii ya mfungaji bora, lakini pia kitendo cha kusema matukio yanayotokea yanawafanya kurekebisha sheria na kanuni zao, basi ni pamoja na hii.
Tuzo za timu mbili
Katika msimu mzima wa Ligi Kuu Bara tumeona ushindani ukiendelea kila siku na kila timu ikijitahidi kupambana ili kutwaa ubingwa, kubaki kwenye ligi na wakati mwingine kuepuka kushuka daraja.
Kuna wachezaji walionekana kuwa na kiwango sahihi kwenye msimu mzima, ingawa kwenye tuzo hawakuingia na kuanzisha mjadala mkubwa.
Mfano kuna wengi wanahoji ilikuwaje likakosekana jina la kiungo wa Azam James Akamiko ambaye ameonekana kuwa kwenye ubora mkubwa msimu huu.
Kiungo huyo pamoja na timu yake kupata nafasi ya kufuzu kwa michuano ya kimataifa msimu ujao, bado binafsi alionekana kuwa bora kwenye kila mchezo ambao alicheza, lakini pia alikuwa na msaada mkubwa wa kuhakikisha kuwa timu yake inafika fainali ya Kombe ASFC ambalo walipoteza dhidi ya Yanga kwa bao 1-0 inaonekana kuwa alistahili kuwemo hapa, hata kama asingeshinda.
Maswali mchezaji bora
Imeonekana kuna maswali mengi yanaulizwa na hayana majibu, labda yanaweza kujibiwa na ile ishu ya kanuni kule juu.
Moja ambayo imekuwa na maswali mengi ni tuzo ya mchezaji bora ambayo ilikwenda na Fiston Mayele ambaye amehusika kwenye mabao 20 msimu huu, jambo zuri, lakini inaonekana kwa vigezo angetakiwa kushinda Saido Ntibazonkiza ambaye kwa uhalisia alishinda tuzo nne kwa mpigo.
Saido alichukua tuzo ya mchezaji muungwana, mfungaji bora, kiungo bora, lakini bado aliingia kwenye kikosi bora cha msimu, kutazama hili na mchango wake wa mabao 29 kwa msimu mzima anaweza kushawishi zaidi kupewa tuzo hiyo kuliko mchezaji mwingine kwa kuwa alionekana kufanya vizuri binafsi kuliko wengine.
Kocha bora safi
Hakuna anayeweza kukataa kuhusu Nasreddine Nabi kutwaa tuzo ya kocha bora kutokana na uwezo aliouonyesha, lakini nafikiri pia ndiye kati ya makocha wawili waliyoanza msimu na timu kwenye ligi na kumaliza nayo, timu nyingine nyingi zilibadilisha makocha katikati ya msimu, hapa lilifanyika jambo zuri pamoja na kushindwa kushinda tuzo nyingi za mwezi.
Manchester City ni moja ya timu iliyoshinda michezo mingi kwenye Ligi Kuu England, lakini FA hawajampa tuzo yoyote kocha wa timu hiyo, Pep Guardiola huku Mikel Arteta wa Arsenal akishinda mara nne.
Kauli ya Karia baada ya tuzo
Rais wa TFF ambaye amefanya kazi kubwa kwenye soka hapa nchini na kufanya makubwa ambayo huko nyuma yalishindikana ameweka msingi mzuri wa soka.
Swali moja ambalo limebaki ni linahitaji majibu kwa wadau ni kauli ya rais huyo baada ya tuzo kuwa msimu ujao hawataangalia idadi ya mabao bali wataangalia ubora wa mabao, hili linahitaji ufafanuzi zaidi kwa kuwa tuzo ya mfungaji bora ni ile ambayo inatolewa kwa yule aliyefunga mabao mengi siyo bao bora.
Alihojiwa na kusema hii ni mara ya mwisho kwa wafungaji wawili kupewa tuzo na wataangalia mfungaji bora siyo aliyefunga mabao mengi, basi ni wakati wa kanuni kuwa wazi kuepuka hili, lakini nafikiri kwa kuwa maboresho ya kanuni ni kazi ya wadau, hili linaonekana kuwa ameshalifanyia kazi.
Ubora wa tuzo
Huku hakuna shaka, pongezi kubwa kwa Shirikisho la Soka TFF kwa kuleta tuzo zenye maboresho makubwa, kila kimoja kilikuwa kinaonekana kwa ubora wake, hili linastahili pongezi kubwa.
Tuzo ya mfungaji bora, tuzo ya mwamuzi bora na tuzo nyingine zote zilionekana kuwa kwenye ubora wa hali ya juu, lakini pia mpangilio wa ukumbini nao uliendelea kuvutia, tunaamini msimu ujao kutakuwa na maboresho makubwa na tutashuhudia tuzo bora zaidi pia tuzo hizi zimegusa kwenye sehemu kubwa sana za soka hapa nchini.
Muda:
Inawezekana kutokana na ratiba ya Ligi Kuu Bara ilichangia jambo hili kufanyika baada ya fainali ya ASFC, lakini inaonekana kama kusingekuwa na ishu ya timu za taifa siku moja mbele ilikuwa siku nzuri zaidi kufanyika kwa tuzo hizo ili kuwapa nafasi wachezaji waliocheza fainali waweze kuhudhuria bila kukosa.
Ni ngumu kwa mchezaji aliyecheza fainali jioni kuhudhuria kwenye tuzo saa moja usiku sawa walikuwepo wachache kama Dickson Job, lakini kama angekuwa na muda wa kupumzika, kesho yake ilikuwa siku nzuri zaidi kwao.