Mayele amtisha Ibenge, Azam ikichanga karata zake
Muktasari:
- Ibenge amesema hilo leo Alhamisi Novemba 26, 2026 ikiwa ni siku moja kabla ya mechi yao ya kwanza ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli itakayopigwa kesho Ijumaa Novemba 27, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge, amekiri kuwa mshambuliaji wa Al Ahli Tripoli ya Libya, Fiston Mayele ni tishio kwa safu ya ulinzi ya timu yake, akisema nyota huyo ni miongoni mwa washambuliaji hatari Afrika ambaye hahitaji nafasi nyingi ili kufunga bao.
Ibenge amesema hilo leo Alhamisi Novemba 26, 2026 ikiwa ni siku moja kabla ya mechi yao ya kwanza ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli itakayopigwa kesho Ijumaa Novemba 27, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mayele, ambaye aliwahi kuichezea Yanga kuanzia 2021 hadi 2023 na kujijengea jina kubwa katika soka la Tanzania, sasa anarejea nchini akiwa na jezi ya Al Ahli Tripoli huku akitarajiwa kuwa miongoni mwa silaha muhimu za kikosi hicho dhidi ya Azam.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, Ibenge hakuficha heshima aliyonayo kwa uwezo wa Mayele, akisisitiza kuwa kumdhibiti kutahitaji umakini mkubwa kwa sababu si mchezaji anayehitaji nafasi nyingi ili kuwaadhibu wapinzani.
"Ni mmoja wa wachezaji bora Afrika kwa sasa. Kila mtu Tanzania anamfahamu, hahitaji nafasi nyingi ili kufunga bao. Itakuwa vigumu sana kukabiliana naye," amesema Ibenge.
Hata hivyo, Ibenge amesema kukutana tena na Mayele kutakuwa furaha kwake, akieleza kuwa anafurahia kuona namna mshambuliaji huyo alivyokua na kuendelea kupiga hatua katika maisha yake ya soka.
"Namfahamu vizuri sana na yeye pia ananifahamu vizuri. Kwanza itakuwa furaha kubwa kumuona tena na kuona namna alivyokua. Natumaini atafanya vizuri kesho, lakini mwisho wa mchezo nataka timu yangu iwe ndiyo iliyoshinda," amesema.
Pamoja na kumzungumzia Mayele, Ibenge amefichua kuwa anafahamu pia uwezo wa baadhi ya wachezaji wengine wa Al Ahli Tripoli, akiwamo Jean Claude Girumugisha ambaye amemwelezea kuwa mmoja wa mawinga bora Afrika kwa sasa.
Kocha huyo amesema aliwahi kufanya kazi na Girumugisha katika klabu ya Al Hilal, huku akimtaja pia Lamine Camara kuwa ni mchezaji anayemfahamu vizuri baada ya kushinda pamoja Kombe la Shirikisho walipokuwa RS Berkane.
Azam iliyopo kundi B katika Kombe la Shirikisho Afrika, inakabiliana na mtihani wa kusaka nafasi ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza itakapokutana na Al Ahli Tripoli ya Libya, AS FAR Rabat (Morocco) na Durban City (Afrika Kusini).