Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kichapo dhidi ya Singida BS chamshtua Ibenge

Muktasari:

  • Azam ilianza kwa kasi mechi hiyo, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, baada ya Feisal Salum na Zidane Sereri kufunga mabao ndani ya dakika mbili na kuifanya timu hiyo kuongoza kwa mabao 2-0.

KOCHA wa Azam FC, Florent Ibenge amesema kipigo cha mabao 4-2 kutoka kwa Singida Black Stars ni matokeo yaliyowashtua kutokana na makosa mengi yaliyofanywa na kikosi chake katika eneo la beki, licha ya kuanza mechi vizuri na kupata mabao mawili ya mapema.

Azam ilianza kwa kasi mechi hiyo, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, baada ya Feisal Salum na Zidane Sereri kufunga mabao ndani ya dakika mbili na kuifanya timu hiyo kuongoza kwa mabao 2-0.

Hata hivyo, Singida ilirejea mchezoni na kufanikiwa kugeuza matokeo kupitia Emmanuel Keyekeh, James Mwashinga na Jonathan Sowah aliyefunga mabao mawili na kuipa timu yake ushindi wa 4-2.

Akizungumza na Mwanaspoti Ibenge alisema hakutarajia timu yake ipoteze mechi kwa namna hiyo, hasa baada ya kupata mwanzo mzuri na kujijengea faida ya mabao mawili.

“Ni matokeo ambayo yametushtua. Tulikuwa tumeanza vizuri sana na kupata mabao mawili, lakini tulishindwa kuendeleza kiwango hicho. Tulifanya makosa mengi ambayo hayakupaswa kutokea katika mchezo wa aina hii.

Alisema, tatizo kubwa lilikuwa namna walivyoshindwa kudhibiti eneo la ulinzi baada ya kupata uongozi, jambo lililowapa Singida nafasi ya kurejea na kujiamini zaidi. “Tulikuwa na nafasi nzuri ya kuudhibiti mechi, lakini makosa yetu ndiyo yaliyowarudisha Singida. Tulipaswa kuwa makini zaidi, hasa baada ya kupata mabao mawili ya kuongoza.”

Kocha huyo aliongeza si jambo la kawaida kwa timu kuongoza kwa mabao mawili halafu ikaruhusu mabao manne, hivyo lazima wafanye tathimini ya kina kubaini walipokosea.

“Unapokuwa mbele kwa mabao mawili, unatakiwa kucheza kwa nidhamu na kuhakikisha unailinda faida uliyoipata. Tulishindwa kufanya hivyo na tukawapa wapinzani nafasi ya kutuadhibu. Hilo ni jambo ambalo tunapaswa kulifanyia kazi.

“Haya ni matokeo ambayo tunapaswa kujifunza kutoka kwake. Hatupaswi kuendelea kuyawaza kwa huzuni pekee, bali tuangalie makosa tuliyoyafanya na namna ya kuyarekebisha. Tunakwenda kwenye michezo ya Afrika na tunajua huko makosa kama haya yanaweza kutugharimu zaidi.

“Tunatakiwa kurejea kwenye maandalizi, kufanya kazi zaidi na kuhakikisha tunakuwa na nidhamu ya kiufundi. Hatuwezi kwenda kwenye mashindano ya Afrika tukirudia makosa yaleyale,” alisema Ibenge.

Azam inatarajiwa kucheza mechi za kundi B la Kombe la Shirikisho Afrika Novemba 27 itakapokutana na Al Ahli Tripoli ya Libya, kabla ya kuvaana na Durban City ya Afrika Kusini Desemba 4, 2026 huku Desemba 5, 2026 ikiwa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga na Desemba 12, 2026 ikitarajiwa kucheza na Dodoma Jiji.

Baadaye itarejea kwenye michuano ya CAF Desemba 19, 2026 kuvaana na AS FAR Rabat ya Morocco, kabla ya kuanza michezo ya marudiano Januari 9, 2027 dhidi ya AS FAR, Januari 16, 2026 dhidi ya Al Ahli Tripoli na Januari 27, 2026 dhidi ya Durban City.