Maprodyuza wanapokuja kuanzisha ligi na wasanii
Muktasari:
- Mabadiliko hayo yanaibua mjadala kuhusu nafasi ya prodyuza katika muziki wa sasa, huku baadhi yao wakiamua kutoka nyuma ya pazia na kuanza kujenga majina yao kama waimbaji wanaojitegemea
KATIKA muziki wa Bongofleva 2026, kuna sura mpya ya ushindani kwani watayarishaji wa muziki maarufu kama maptodyuza wanaongeza kasi ya kuingia kwenye uimbaji, tofauti na ilivyozoeleka miaka ya nyuma ambapo wengi wao walijikita zaidi katika kutengeneza midundo ya wanamuziki.
Mabadiliko hayo yanaibua mjadala kuhusu nafasi ya prodyuza katika muziki wa sasa, huku baadhi yao wakiamua kutoka nyuma ya pazia na kuanza kujenga majina yao kama waimbaji wanaojitegemea. Katika miaka ya nyuma, majina kama P-Funk Majani na Master J yalitambulika zaidi kwa ubora wa kazi zao za utayarishaji, huku mchango wao ukiwa mkubwa katika kukuza Bongofleva na kuwajenga wasanii mbalimbali.
Miongoni mwa mifano inayodhihirisha mabadiliko hayo ni Idd Mohamed Ngomba, maarufu Mocco Genius, ambaye mbali na kutengeneza nyimbo za wasanii wengine, amekuwa akitoa kazi zake kama mwimbaji.
Hatua yake ya hivi karibuni kuachia EP yake ya kwanza ya KANDA, Septemba 25, 2026, yenye jumla ya nyimbo sita imekuwa kama msisimko mpya katika gemu la muziki huo unaopendwa na vijana wengi hapa nchini. Ndani ya EP hiyo amewashirikisha Alikiba, Yammi, Christian Bella na Dogo Paten, huku ikiunganisha ladha ya muziki wa zamani na mitindo ya kisasa.
MOCCO AANZA SAFARI MPYA
Kwa upande wa Mocco Genius, kuingia kwenye uimbaji si jambo la ghafla, bali ni hatua mpya katika safari yake ya muziki iliyoanza akiwa na umri wa miaka 17.
Alisema mwanzoni alitembelea studio mbalimbali kujifunza namna ya kuchanganya sauti, kabla ya kuingia rasmi kwenye utayarishaji wa muziki mwaka 2017.
Kupitia kipaji hicho, Mocco alijijengea jina kama mtayarishaji aliyefanya kazi na wasanii mbalimbali wakubwa, wakiwamo Alikiba, Diamond Platnumz, Zuchu na Mbosso. Pia alianzisha studio ya Imagination Sound, inayojihusisha na utayarishaji na kukuza vipaji vya wanamuziki.
Hata hivyo, hakutaka kubaki nyuma ya mitambo ya muziki pekee. Mwaka 2022 aliamua kuanza rasmi safari ya uimbaji kupitia wimbo wake Napendwa, hatua iliyofuatwa na nyimbo nyingine zikiwamo Mchuchu, Mi Nawe na Yamenishika.
Akizungumzia safari yake ya kutoka kwenye utayarishaji wa muziki na kuingia kwenye uimbaji, Mocco alisema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wake wa kupanua utambulisho wake ndani ya tasnia ya muziki, baada ya kujijengea jina kama mtayarishaji.
“Kwa sasa ninajikita katika kukuza chapa yangu 'Brand' ili kukuza zaidi shughuli zangu za uimbaji na nimeanza na EP na mengine mengi mazuri yanafuata”. alisema Mocco
S2KIZZY NAYE KAINGIA
Prodyuza mwingine anayechukua hatua ya kujitanua kwenye muziki ni Salmin Maengo, maarufu S2Kizzy, ambaye sasa anajipanga kujitambulisha zaidi kama muimbaji kupitia albamu yake ya VIRUS, inayotarajiwa kuzinduliwa Novemba 12, 2026.
Kabla ya hatua hiyo, S2Kizzy amejijengea jina kubwa kupitia utayarishaji wa nyimbo zilizopata mafanikio ndani na nje ya Tanzania. Miongoni mwa kazi hizo ni Tetema ya Rayvanny akimshirikisha Diamond Platnumz. Pia alihusika katika utayarishaji wa Baba Lao na Jeje za Diamond Platnumz, ambazo zimevuka. Nyingine ni Komasava ya Diamond Platnumz, Khalil Harrison na Chley, aliyotayarisha kwa kushirikiana na DJ Awakening. Remix yake iliyomshirikisha Jason Derulo. Hatua yake ya kuingia kwenye uimbaji inaongeza sura mpya katika tasnia, ambapo watayarishaji hawabaki tena nyuma ya pazia pekee, bali wanapanua nafasi zao na kujenga utambulisho kama wasanii.
WASANII KATIKA USHINDANI MPYA
Mabadiliko haya yanaweza pia kuibua aina nyingine ya ushindani ndani ya Bongofleva. Zamani prodyuza alikuwa mtu ambaye msanii anamtafuta ili apate wimbo wenye ubora, lakini sasa prodyuza huyo anaweza kujikuta akiwa mshindani wake katika soko la muziki.
Ushindani huo si lazima uwe wa kugombania nafasi kwani unaweza pia kuongeza ubunifu na kuleta ushirikiano mpya, hasa pale ambapo mtayarishaji anakuwa na uwezo wa kuelewa pande zote mbili za muziki.
WANAKUJA KUWAPIKU WASANII?
Kuongezeka kwa watayarishaji wanaoingia kwenye uimbaji kunazidi kuibua mjadala kuhusu mwelekeo wa Bongofleva, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi yao tayari wamejijengea majina makubwa kupitia kazi za wasanii wengine.
Hatua hiyo inaweza kubadilisha uhusiano wa kawaida kati ya prodyuza na msanii, kwani mtu aliyekuwa akitengeneza nyimbo za wengine sasa anaanza kuwania nafasi hiyo hiyo katika soko la muziki. Je, huu ni mwanzo wa ushindani mpya wa kuwania mashabiki na nafasi kwenye muziki, au ni fursa ya kuongeza ubunifu wa Bongofleva?