Mapito!! Nyuma ya Mwasika kuna maumivu katika soka
Muktasari:
- Mwasika anasema kumbukumbu alizosalia nazo katika mpira wa miguu ni nne, ambazo zimejaa uchungu kutokana na kupitia vitu vigumu, akivikumbuka vinamuumiza kutokana na kuvuja jasho ambalo halijamlipa.
SIMULIZI ya maisha ya soka ya beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Stephano Mwasika, inafunua upande mwingine ambao mashabiki hawakuwahi kumsikia.
Mahojiano baina yake na Mwanaspoti, beki huyo anaeleza ingawa amesomea ukocha ngazi ya Diploma C ya CAF hataki kujishughulisha na mambo ya soka kabisa na uamuzi huo unaweza ukachukua muda mrefu.
“Nimeamua kuendelea na biashara zangu za kuuza vifaa vya michezo, inaweza ikanichukua miaka 10 au nikaachana na mambo ya mpira wa miguu moja kwa moja, kitu nachofanya kwa sasa ni mazoezi na maveterani wenzangu kwa ajili ya kutunza afya,” anasema.
ALAMA NNE ZA SOKA
Mwasika anasema kumbukumbu alizosalia nazo katika mpira wa miguu ni nne, ambazo zimejaa uchungu kutokana na kupitia vitu vigumu, akivikumbuka vinamuumiza kutokana na kuvuja jasho ambalo halijamlipa.
“Nakumbuka mkataba wangu na Moro United ulitakiwa kumalizika 2009 maana nilisaini 2008/09 nikitokea Tanzania Prisons, baada ya kumalizika kwa mkataba huo, timu ya African Lyon ikiwa chini ya Mohammed Dewji ilihitaji huduma yangu ambapo dau lake la usajili lilikuwa kubwa,” anasema Mwasika na kuongeza:
“Wakati nataka kwenda kusaini nilishangaa viongozi wa timu ya Moro United wananiambia nina mkataba wa mwaka mmoja mbele, sikuwa na la kufanya nikalazimika kutumika mwaka mmoja bure, ingawa nilijua wamenifanyia uhuni, sikuacha kufanya bidii ya mazoezi na kujituma uwanjani wakati wa mechi, hivyo ofa ya Lyon ikashindikana maana nilitafutwa moja kwa moja Mo Dewji mwenyewe.”
Anasema bahati nzuri baada ya kuutumikia mwaka mmoja wa bure Moro United, alionekana na timu ya Yanga, kiongozi ambaye alikuwa amehusika katika kumdhurumu alimkuta tena Jangwani akiwa na ushawishi mkubwa ndani ya timu na kusimamia usajili. “Maisha ndani ya Yanga yaliendelea, baadaye nikapata majeraha ya goti ilitakiwa nikatibiwe India nikamtafuta Uhuru Seleman aliyekuwa anacheza Simba maana alikuwa ameshawahi kwenda huko kutibiwa na akawa anataka kurejea tena mara ya pili, akaniunganisha na daktari ambaye aliniambia gharama, nikarudi kwa viongozi wa Yanga kuwaambia kila kitu,” anasema beki huyo na kuongeza:
“Kumbuka kiongozi ambaye nilikuwa namwambia hayo yote ni yule aliyekuwa amehusika kunidhurumu Moro United, akawa amenijibu nenda tu India huko nina biashara zangu nitakuunganisha na watu wangu ambao wanasimamia vitu vyangu kila kitu kitaenda sawa, basi nikampigia Uhuru tukaenda hadi India, baada ya kufika huko nilipiga simu wiki nzima akawa hapokei, nikamwambia daktari anifanyie upasuaji timu italipa.
“Baada ya kunifanyia upasuaji nikawa napiga simu hawapokei, nilitembea na kadi ya benki ya Visa, nikampa Uhuru ili akatoe pesa abadilishe kwa dola kisha tulipe, maana walikuwa hawakubali kulipa kwa pesa yao ilikuwa chini, nilikuwa na Sh20 milioni kwenye akaunti ambayo ililipwa yote hospitali na bado nikawa nadaiwa mambo mengine madogomadogo.
“Kwa upasuaji na sindano ambayo nilichomwa ilitakiwa nikae wiki mbili hadi tatu bila kufanya ‘movement’ ya aina yoyote, lakini mimi baada ya siku mbili nilimwambia Uhuru tuondoke tutajua tutasaidiwaje kwenye uwanja wa ndege au tukapotelee huko, hadi nafika Tanzania sikujua nimefikaje.
“Nilipofika Tanzania sikuwataarifu viongozi wa Yanga nilikaa kama miezi mitatu maana hawakuwahi kuniulizia, mechi ambayo Simba iliifunga Yanga mabao 5-0 nilienda uwanjani ndipo waliponiona kwamba nipo Tanzania, baadaye nikapigiwa simu na watu waliokuwa wanafanya kazi na aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga Yusuf Manji (marehemu), ili nikachukue cheki ambayo ilikuwa ya Sh500,000 na ikumbukwe nilifanyiwa upasuaji hadi kukamilika ilikuwa zaidi ya Sh20 milioni, nikanyamaza kimya sikutaka mambo mengi.”
Anasema baada ya kupona alirejea klabuni kuendelea na majukumu yake kama kawaida, lakini akiwa na msongo wa mawazo kutokana na hali anayopitia.
“Ujue kuna wakati viongozi walikuwa wananitafsiri kama mtu mwenye kiburi, kwani nilikuwa sina kawaida ya kuombaomba kama ilivyokuwa kwa baadhi ya wachezaji wenye uchawa wa kupeleka maneno ya uchonganishi, mimi nilikuwa nasubiri mshahara wangu wa mwisho wa mwezi, niliamini niliuvujia jasho, ambao niliamini niliacha usingizi na kwenda kurukaruka na mazoezi,” anasema Mwasika.
Baada ya kumalizika mkataba wake wa kwanza, anasema hakutaka kuendelea na Yanga ili kuepusha migongano na kiongozi aliyekuwa anamwekea ugumu katika vitu vingi, lakini aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Tom Saintfiet alipojua changamoto hiyo alimpigia simu moja kwa moja Manji kwamba ananihitaji, hivyo ahusike mwenyewe kumbakiza.
“Manji alinipigia simu moja kwa moja, nikamwelezea akasema mimi ndiye natoa pesa za usajili, tukakubaliana dau ninalolitaka akanielekeza kwa kiongozi huyo huyo ili nikasaini mkataba, nikakaza moyo kwenda ofisini kwake, nikamwambia kiasi cha pesa ambacho nimekubaliana na Manji, akasema hiyo pesa ni nyingi, akawa anataja ya kwake nikasema kama sitapewa hiyo sitasaini akasema niondoke, nikaondoka,” anasema Mwasika.
“Nilipofika karibu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akapiga simu nirudi kusaini, baada ya kurudi akanipa mikataba miwili, mmoja ulikuwa mkataba wa mwaka mmoja na mwingine wa miaka miwili, halafu akasema niisaini, halafu atanikata pesa ya adhabu ambayo niliadhibiwa kwa kumpiga ngumi mwamuzi Israel Nkongo, ilikuwa mechi dhidi ya Azam na pesa ilikuwa tayari imelipwa na klabu ilikuwa Sh3 milioni, ili kuepusha mengi nilimwambia aikate.
“Baada ya kusaini mkataba nilimrudishia wa miaka miwili, nikabakia na wa mwaka mmoja, baada ya msimu kumalizika viongozi wa timu walikaa na wachezaji wakasema mchezaji aliyemaliza mkataba wake apite mbele, mimi nikapita kila mtu akabakia anashangaa, nikaulizwa wewe una mkataba wa miaka miwili kwa nini unapita mbele, nikawajibu nilisaini mkataba wa mwaka mmoja, akadakia yeye kwamba nipeleke ushahidi kesho yake katika ofisi za Yanga pale Jangwani.
“Ilipofika kesho yake nikaenda na mkataba wakawa ule wa mwaka mmoja, wakawa wanataka niwape mkononi, nikawaambia naushika mwenyewe angalia kwa mbali, walipoona ni kweli akabakia yeye na aibu yake, hivyo huo ukawa mwanzo wangu wa kuondoka Yanga na pesa yangu niliyokuwa nawadai ya usajili maana sikupata yote nikalipwa baada ya kuwashitaki TFF.
“Sikuwahi kuwa na shida na Yanga wala viongozi wengine wa timu, alikuwa ni huyo mmoja tu, ukiniuliza soka limekupa nini nitakujibu limenipa watu ila kiuchumi hapa, sijafaidika nalo kabisa, kuna wachezaji wanapitia mazito hawana pa kusemea, kila mtu anawahukumu anavyoona bila kujua nyuma ya pazia wanapitia kitu gani.”
Alipoulizwa na Mwanaspoti ni sababu zipi zilizomfanya ampige ngumi Nkongo, Mwasika anasema hukumu dhidi yake ingeamriwa vizuri zaidi iwapo kungekuwa na teknolojia bora kama sasa.
“Laiti kama Tanzania kungekuwa na vifaa kama Ulaya, mchezaji anaposemezana na mwamuzi vinakuwa vinavuta na kuonyesha alikuwa anasema nini, basi waamuzi wengi wasingechezesha mpira wa miguu, unakuta mtu anakutukania mama yako inaumiza, ukiwa na moyo mdogo unajikuta unachukua uamuzi mbaya,” anasema.
“Ingawa kuna waamuzi walikuwa na hekima sana, mchezaji ukimfuata na kumwambia mbona hiki kimefanyika hivi anakujibu ni makosa ya kibinadamu tuendelee, mtu kama huyo huwezi kuendelea kubishana naye mfano walikuwepo kama Victor Mwandike, Kennedy Mapunda walikuwa na busara kubwa, mchezaji ukijua wanachezesha unakuwa na amani, hao ni miongoni mwa wema na wanapaswa kuigwa. Soka ni mchezo wa uungwana na siyo mmoja kuonekana hana akili wakati anategemewa kama baba.”
KMC VIWANJA
Anasema baada ya kujiunga na KMC alikabidhiwa unahodha wakati inapambana kupanda Ligi Kuu, aliitwa katikati ya madiwani wa Kinondoni na kuambiwa anapaswa kuahidi jambo moja, kwamba ataisaidia timu kupanda.
“Walisema timu ikipanda daraja, kila mchezaji watampatia kiwanjani, mechi ya mwisho dhidi ya Mlale FC katika hoteli ambayo tulikuwepo alikuja Meya akatuambia kama timu ikipanda zawadi imeongezeka, tutapewa viwanja na matofali, baada ya kufanikiwa kuipandisha, wakaishia kutupa Sh100,000 kila mchezaji,” anasema Mwasika.
“Kitendo cha KMC msimu wa 2025/26 kushuka daraja huwezi kuamini wachezaji ambao tulidhurumiwa pamoja wanapiga simu bado wana vinyongo, hawana maumivu na timu hiyo kushuka, kiukweli wakati mwingine vilio vya kweli vya watu siyo vizuri. “Wachezaji wengi tumetokea familia za kimaskini kiongozi ikitokea anakudhurumu ajue hakukomoi mchezaji peke yako ajue kuna watu nyuma yako anawaumiza, wale wakiomba mwisho wao unakuwa mbaya.
“Washikaji wangu wengi wameachana na wanawake zao wa mwanzo mambo ni hayo hayo, muda mwingi upo bize na timu halafu haoni pesa unayopeleka nyumbani, laiti viongozi wangejua hilo wasingelifanya hata kwa bahati kula pesa za wachezaji kwa makusudi, binafsi namshukuru Mungu nimedumu na mke wangu kwa hekima na neema yake.”
MPANGO WA PILI
Anasema mkoa wa Mbeya aliyozaliwa jambo la kwanza, mtu anapokuwa anakua anakuwa anawaona wazazi wake, wakishika majembe na kwenda kulima, hivyo lazima itamjenga kichwani kuona ndiyo kama anatakiwa kuifanya.
“Nilikuwa nalima kwa mkono baadaye kuna watu walikuwa wanasimamia wakati nipo bize na kazi ya soka, ingawa kwa sasa nalima mwenyewe mazao kwa ajili ya chakula, ikitokea yamezidi nafanya biashara, binafsi najivunia kilimo siyo cha kunifanya nikajisikia vibaya,” anasema.
“Ukiachana na hilo naendelea kufanya biashara za vifaa vya michezo, duka langu lipo Karume tangu nacheza Yanga, wanunuzi ni hao hao wachezaji wanaocheza kwa sasa.”
SOKA LA SASA
Akizungumzia soka la miaka ya sasa, nyota huyo mkongwe anasema hujisikia vibaya anapogundua mchezaji anaidai timu ilhali aliitumikia kwa upendo na kujituma.
“Ligi Kuu inazidi kuwa bora msimu hadi msimu, ila jambo la msingi viongozi wa soka, wajitahidi kulipa haki za wachezaji, ninajisikia vibaya ninapoona mchezaji fulani anaidai timu na ameishitaki timu yake, ni asilimia chache unamkuta mchezaji aliyetoka familia za kitajiri anacheza mpira wa miguu, hao kina Cristiano Ronaldo ukubwa wa jina lake, nyuma kuna historia ya maumivu ya umaskini,” anasema.
WANASAIKOLOJIA
Anasema mchezaji anapofanya tukio lisilo la kawaida uwanjani asihukumiwe bila kujua anapitia tatizo gani. “Kuna haja wanasaikolojia kuwepo kwenye timu, ikishindikana liwe jukumu la viongozi mnapoona mchezaji basi mtafutie mtu wa kumjenga, nilikuwa mchezaji kuna mambo mengi wanapitia, ambayo inakuwa siri ya mioyo yao,” anasema.