Mapacha wanaanza kurudi Uhuru taratibu
Muktasari:
- Kikubwa kinachofurahisha kwa mapacha ni jinsi wanavyofanya mambo kwa kuigana hasa upande mmoja ukiona mwingine unafanikiwa katika jambo fulani.
MAPACHA wanatuacha hoi sana hapa kijiweni ila hatuna tabu nao kwa sababu tumewazoea maisha yao katika namna wanavyoendesha mambo yao.
Kikubwa kinachofurahisha kwa mapacha ni jinsi wanavyofanya mambo kwa kuigana hasa upande mmoja ukiona mwingine unafanikiwa katika jambo fulani.
Hili jambo la Uwanja wa Uhuru msimu huu ni mfano mmojawapo wa jinsi mapacha wa kariakoo wanavyotazamana na kufuatiliana katika ufanyaji wa mambo yao.
Katika mechi za matamasha yao, zote mbili zilitumia Uwanja wa Uhuru na zikajikuta zikipokea vichapo ambapo pacha mmoja akifungwa na timu ya Kongo na mwingine akachapwa na Wakenya.
Wakaona uwanja una nuksi kwao wote wawili wakaukimbia pindi mechi za ligi zilipoanza wakaenda Kinondoni mmoja katika uwanja ule wa Manispaa na mwingine katika uwanja ule wa jeshi.
Zikaja mechi za kimataifa ambazo kikanuni wasingeweza kutumia viwanja vya kule Kinondoni wakajikuta mmoja anatumia uwanja wa kule Chamazi mwingine uwanja wa pale Chang’ombe.
Yule wa Chang’ombe akampiga mtu bao sita na aliyecheza Chamazi akashinda mabao mawili na wote wakafuzu hatua inayofuata kwenye mashindano wanayoshiriki.
Sasa yule wa Chamazi anaanza kurudi taratibu pale Uhuru muda mfupi baada ya mwenzake kumpiga mtu mabao sita na kwa kuanzia amepanga kucheza mechi ya kirafiki katika huo uwanja na timu kutoka nje ya nchi.
Inawezekana amehisi ule uwanja wa Uhuru una bahati kimataifa hivyo ameanza kutuandaa taratibu kisaikolojia kuwa anarejea hapo kubanana na mtani wake.