Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ni wakati wa Cecafa kuja na mikakati mipya

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ni kama vile limekwama kupata mwenyeji wa kuandaa fainali za Kombe la Kagame kwa mwaka 2016.

Mashindano hayo ya kila mwaka ambayo hushirikisha klabu za soka za Afrika Mashariki, ni kati ya mashindano muhimu ya kuzipima klabu za nchi wanachama wa Afrika Mashariki na Kati.

Ni mashindano yenye historia ndefu kama yalivyo yale ya Kombe la Chalenji ambayo hushirikisha timu za taifa za nchi wanachama wa Cecafa.

Awali habari ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ilipokelewa kwa mikono miwili na baadhi ya mashabiki wakiamini kwamba ni fursa nyingine ya Tanzania kulibakisha nchini kombe hilo ambalo Azam ni mabingwa watetezi.

Azam walifanikiwa kulibeba taji hilo mwaka jana katika mechi ya fainali dhidi ya Gor Mahia ya Kenya kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Wakati Rais wa TFF, Jamal Malinzi akitangaza Tanzania kujitoa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, wapo mashabiki wa soka nchini ambao wanaamini mashindano hayo yamepoteza mvuto wa zamani.

Hili ni jambo ambalo limekuwa likizungumzwa mara kadhaa na tunadhani imefika wakati sasa, Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye na rais wake, Dk Mutasim Gaffar kuja na mikakati mipya ya kuboresha mashindano hayo.

Kwa muda ambao mashindano haya yamekuwa yakifanyika tangu miaka ya 1960 mwishoni, yalitakiwa yawe na hadhi na kuzifanya nchi zipiganie kuwa mwenyeji badala ya hali ya sasa ya nchi kukimbia uenyeji.

Si mashindano haya tu ambayo kuanzia mwaka 2002 yalibatizwa jina la Kombe la Kagame, bali Cecafa kwa jumla yake inatakiwa kujipanga na kuja na mikakati mipya.

Hatua ya TFF kujitoa kuwa mwenyeji pamoja na mambo mengine huenda imechangiwa na kupungua kwa mvuto wa mashindano kwani kama yangekuwa ni mashindano yanayovutia wadhamini TFF kamwe wasingekubali kujitoa.

Tunaamini Cecafa bado ina uwezo wa kuyapa hadhi mashindano haya ili yawe ya mfano kwa kanda nyingine za Afrika.

Kwa hali ilivyo sasa ni dhahiri kwamba Cecafa wana kazi ya kubwa ya kufanya katika kuleta mapinduzi ya kweli kwenye mashindano yake.

Moja ya jambo linaloweza kufanywa na Cecafa ni kuja na nguvu mpya ya kupata wadhamini wengi ambao watafanikisha mashindano haya ili yawe kama yanazinduliwa kwa staili mpya. 

Musonye, mwandishi wa zamani wa habari za michezo, amekuwa ndani ya Cecafa tangu mwaka 2000, ni vyema akatambua kwamba anapitia katika kipindi cha aibu kwa mashindano hayo kushuka hadhi wakati yeye akiwa kiongozi mzoefu.

Mashindano hayo yamekuwa yakitumika kuinua soka la Afrika Mashariki na kati ambalo kwa mtazamo ni kwamba limekuwa likiburuzwa na maeneo mengine ya Afrika. Cha msingi ni kuongeza mashindano na wala si kuahirisha.

Vyovyote itakavyokuwa kwa sasa, Musonye hatoweza kujiweka kando na anguko la mashindano haya.