Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Manyasi: Kiungo msomi anayeng'aa Coastal Union

Kiungo wa Coastal Union, Geofrey Manyasi

Safari ya maisha ni ujasiri, uthubutu na uamuzi. Ndicho alichofanya kiungo wa Coastal Union, Geofrey Manyasi kuachana na taaluma aliyosomea na kuamua kuendeleza kipaji chake.

Manyasi ni mwalimu kitaaluma wa masomo ya Historia na Lugha kwa kiwango cha Shahada aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Jordan kilichopo mkoani Morogoro, akihitimu 2018.

Hata hivyo matarajio yake huko mbeleni ni kujiendeleza hadi kupata shahada ya uzamili ili kutimiza azma ya wazazi wake waliotamani kuona anafikia kiwango hicho kisha kuendelea na mambo mengine.

“Kipindi Mbeya City ikiwa moto wakati imepanda Ligi Kuu chini ya Juma Mwambusi, walinihitaji kufanya nao kazi. Lakini kutokana na msukumo wa wazazi kuwa na kipaumbele chao, nilishindwa kwenda,"anasema Manyasi.

Kiungo wa Coastal Union, Geofrey Manyasi


Mgogoro na wazazi

Manyasi anasema haikuwa rahisi kuwashawishi wazazi wake wamruhusu acheze Ligi Kuu huku akiwa anasoma na hasa baba yake mzazi.

“Ilikuwa ni vita kali sana, mimi nawaza, nafikiria na kupenda mpira lakini wazazi wakawa wanakazia elimu. Ikawa ni mgogoro mzito hasa na baba ambaye aliamini kitu ni elimu.

“Nashukuru walimu walinipenda kama sehemu ya alama ya chuo, wakaamini kupitia mpira natangaza taasisi. Hivyo baadhi ya mitihani nikawa nafanya mwenyewe baada ya kumaliza mechi,” amesema Manyasi.


Aibukia Ihefu

Baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu, Manyasi aliibukia Ihefu (kwa sasa Singida Black Stars), ambako ndiko nyota ilianza kung’ara, akionesha kiwango bora kisha kutimkia kwingine.

Hata hivyo baada ya Ihefu kuuzwa, nyota huyo alitua Geita Gold ambapo kiwango chake kilizidi kuonekana hasa baada ya kusaidia kuipandisha Ligi Kuu timu hiyo na kutimkia Kagera Sugar.

“Baada ya Kagera Sugar simu iliita kutoka Coastal Union, ambapo tulikubaliana nikaamua kusaini na kwa sasa nashukuru maisha na mazingira ya kazi ni mazuri kazi inaendelea,” amesema.

Kiungo wa Coastal Union, Geofrey Manyasi


Ataka namba Simba na Yanga

Kiungo huyo fundi wa mpira anasema kuwa malengo yake ni kuona anavuka mafanikio aliyonayo kwa sasa akicheza moja ya timu kubwa nchini, Yanga, Simba na Azam akieleza kuwa namba ni uhakika.

Anasema anachoamini ni uwezo wake wa mguu aliopewa na Mungu kupitia kipaji cha mpira, hivyo popote atakapopata nafasi, kupata namba ni uhakika na atafanya makubwa kufikia ndoto zake.

“Malengo yangu ni kuona navuka hapa nilipo, nicheze moja ya timu za Simba, Yanga na Azam na Taifa Stars. Naamini kila kitu kina wakati wake, siwezi kukata tamaa kwakuwa bado ni mapema.

“Lolote linawezekana kwa kuwa naamini kwenye uwezo na kipaji. Mungu atakapoamua nicheze wapi, binafsi nipo tayari na ndoto zangu ni hizo. Wapo wanaofanya vizuri ila mimi pia naweza,” amesema.


Amtaja Boban

Staa huyo anakiri kuwa wachezaji aliowaona uwanjani ni wengi na walifanya makubwa sana, lakini nyota wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars Haruna Moshi ‘Boban’ ndiye alikuwa mbabe wa wote.

Anasema akiwa na umri mdogo, Manyasi alikuwa akivaa jezi yenye jina la Boban akiiandika namba tatu mgogongo kuashiria mapenzi yake kwa kiungo huyo wa zamani na nyota.

“Niliwaona viungo wengi wakifanya makubwa uwanjani lakini nilimkubali sana Boban. Hadi nguo zangu niliziandika jina lake na baadhi ya mashabiki nyumbani wananiita Boban.

“Pale eneo la katikati alilitawala wakati wake bila kujali timu gani aliyocheza nayo. Mara kadhaa nikiangalia video zake sichoki. Najifunza vingi kwake natamani nizidi pale,” amesema nyota huyo.


Coastal Union sio kinyonge

Nyota huyo anasema msimu huu hawakuwa na mwanzo mzuri lakini kwa sasa Coastal Union iko kwenye malengo yake na matokeo waliyoanza kupata yanawapa matumaini mapya.

Anasema kama walivyoazimia kusaka nafasi nzuri kwenye msimamo, wanao uwezo wa kubadili upepo na kumaliza ligi kibabe akieleza kuwa ari, nguvu na morali kwa wachezaji na nje ya uwanja ni kubwa.

“Bado tupo kwenye malengo. Hatujapoteana japokuwa ratiba tuliyokutana nayo haikuwa nzuri ila kwa sasa tumeanza upya kurejea taratibu na matarajio ni kumaliza nafasi nzuri,” amesema kiungo huyo.