Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dada, usikurupuke saluni bila kujua siri hizi za kucha

Muktasari:

  • Lakini ukweli ni kwamba kucha nzuri si lazima ziwe ndefu kama sindano wala kupakwa rangi inayong’ara kutoka mbali. Muhimu ni kuchagua urefu unaokufaa, rangi inayokupendeza na mtindo unaoweza kuutunza bila usumbufu.

DADA kabla hujakaa kwenye kiti cha mtaalamu wa kucha wikiendi hii jiulize swali moja; hivi unataka kucha zinazokupa urembo au zinazokufanya ushindwe hata kufungua pochi yako? Wapo wanaopenda kucha ndefu zenye rangi kali, wengine wanapenda fupi zenye mwonekano wa kawaida, huku wengine wakibadili rangi kila waendapo saluni.

Lakini ukweli ni kwamba kucha nzuri si lazima ziwe ndefu kama sindano wala kupakwa rangi inayong’ara kutoka mbali. Muhimu ni kuchagua urefu unaokufaa, rangi inayokupendeza na mtindo unaoweza kuutunza bila usumbufu.


UREFU SAHIHI WA KUCHA NI UPI?

Kucha za asili zinaweza kuwa fupi au ndefu, lakini kwa matumizi ya kila siku, kucha zinazopita kidogo ncha za vidole huwa rahisi kutunza. Urefu huu unakupa nafasi ya kupaka rangi na kupata mwonekano nadhifu bila kukuzuia kufanya kazi za kawaida kama kuandika, kupika au kufungua vitu.

Ikiwa unapenda kubandika kucha, unaweza kuchagua urefu mfupi au wa wastani unaolingana na vidole vyako. Kucha ndefu zinaweza kuvutia, lakini zinahitaji uangalizi zaidi na zinaweza kuvunjika au kukwama kwenye nguo. Hakikisha pia zimebandikwa vizuri na haziumi, hazibani wala kuharibu kucha zako za asili.


RANGI ZINAZOPENDEZA NGOZI NYEUSI

Kwa dada mwenye ngozi nyeusi, rangi kama nyekundu iliyokolea, zambarau, kahawia ya chokoleti, dhahabu na rangi ya maziwa zinaweza kuleta mwonekano mzuri. Rangi ya waridi iliyopauka pia inaweza kupendeza, hasa ikiwa unataka mwonekano mpole unaofaa kuonekana kokote bila kushtua.


RANGI ZINAZOPENDEZA NGOZI NYEUPE

Kwa dada mwenye ngozi nyeupe, rangi kama nyekundu, zambarau, kahawia na  ya maziwa zinaweza kutoa mwonekano wa kuvutia. Rangi nyekundu inaweza kuleta mwonekano wenye kuvutia Zaidi kuliko zingine.

Rangi za kahawia laini na rangi zinazofanana na ngozi pia zinaweza kufanya kucha zionekane nadhifu, unaweza kuchagua dhahabu au rangi yenye mng’ao. Hata hivyo, hakuna rangi inayomilikiwa na ngozi nyeupe pekee ingawa nyingi zinawakubali.


WASIKIE WAREMBO

Jesca Lunyali anasema: “Mimi napenda rangi zinazojitokeza kama nyekundu iliyokolea na zinanikaa vizuri, mikono yangu huonekana nadhifu na kucha zinavutia. Lakini sipendi kucha ndefu sana kwa sababu zinanisumbua ninapofanya kazi zangu.”

Witness Monyo anasema: “Napenda rangi ya maziwa kwa sababu zinanipa mwonekano wa kawaida. Nikitaka kwenda kwenye sherehe, huwa nachagua rangi nyekundu au yenye mng’ao. Kwangu, muhimu ni rangi kuendana na mavazi yangu.”

Mama John anasema: “Urembo wa kucha ni mzuri, lakini wasichana wasisahau usafi. Kucha ziwe safi, zisiumize vidole na zisiwe ndefu kiasi cha kuwazuia kufanya kazi. Hata kucha fupi zinaweza kupendeza sana.”

Robert Laurent anawakilisha vijana wa kiume anasema: “Mimi napenda kucha zilizopangwa vizuri na rangi inayomfaa msichana. Si lazima ziwe ndefu sana au ziwe na mambo mengi. Kucha safi na zenye mwonekano mzuri zinavutia zaidi.”


USHAURI

Dada, kabla ya kubandika kucha au kupaka rangi, hakikisha mikono na vifaa vinavyotumika ni safi. Usibandike kucha kwenye ngozi iliyojeruhiwa, na ukiona maumivu, wekundu au uvimbe, acha kutumia bidhaa hiyo na tafuta ushauri wa mtaalamu wa afya.

Chagua urefu unaokuruhusu kufanya shughuli zako bila shida, na usilazimishe kucha zako ziwe ndefu kwa sababu tu unaona wengine wako hivyo. Kumbuka, rangi nzuri ni ile unayoipenda na inayokupa kujiamini; ngozi nyeusi au nyeupe haikuzuii kujaribu rangi yoyote inayokuvutia.