Prime
Mambo matano yanayomtoa Fadlu Simba
TAARIFA mbaya kwa mashabiki wa Simba ambazo huenda hawatapenda kuzisikia ni kushika kasi kwa uvumi kwamba kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids anajiandaa kutimka Msimbazi.
Taarifa hizo zimewashtua wengi na ingawa klabu hiyo haijazitolea ufafanuzi, zina ukweli mkubwa ambapo kocha huyo kuna mambo hayafurahii ndani ya ajira aliyonayo klabuni hapo kwa msimu wa pili tangu alipotua akitokea Raja Casablanca ya Morocco.
Baada ya kuvuma kwa taarifa hiyo, Mwanaspoti limeingia chimbo na kubaini kuna mambo matano ambayo Fadlu hayafurahii ndani ya klabu yake na kuamua kufikiria kuachana nayo licha ya kwamba ndio kwanza msimu mpya umeanza.
HUJUMA
Jambo la kwanza ni kwamba kocha huyo anaona kama anahujumiwa, hasa baada ya kupoteza mechi ya nne mfululizo dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, huku timu yake ikishindwa kufunga bao hata moja.
Fadlu anaona wako viongozi, hawafurahii uwepo wake ndani ya klabu hiyo baada ya kuwazuia kuingilia mchakato wa usajili wa kikosi chake ambapo inaelezwa alishaonywa kwamba kama atapoteza dhidi ya Yanga presha itakuwa juu yake.
Fadlu alianza kuchapika mbele ya Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii msimu uliopita na kulala mechi zote mbili za Ligi Kuu Bara ikiwamo ile kuamua bingwa Juni 25 mwaka huu waliyofungwa 2-0, kisha msimu huu wakafungwa tena 1-0 katika Ngao ya Jamii.
MIUNDO MBINU
Jambo la pili ambalo limemtibua Fadlu ni kwamba wakati msimu uliopita unamalizika, alikubaliana na uongozi wa Simba kwamba kabla ya msimu ujao basi uwanja wa mazoezi uliopo kule MO Bunju Arena utafanyiwa maboresho makubwa ili kumrahisishia kazi kuiandaa timu kambini.
Eneo muhimu ambalo Fadlu alitaka liboreshwe ni lile la kuchezea, lakini hadi anarudi hakuna kitu ambacho kilifanyika na kuona kama mambo hayaendi kama wanavyokubaliana kwenye vikao na uongozi wake. Hivyo anaona ni vyema asepe zake ili maisha yawe mepesi kwake.
USAJILI
Kuna hili la usajili ambalo nalo limetibua amani ya Fadlu ndani ya Simba. Kocha huyo hakufurahishwa na namna alivyowakosa wachezaji muhimu ambao aliwataka wakati wa maboresho ya usajili.
Wako mastaa ambao Fadlu aliwataka akiwamo Celestin Ecua, Moussa Balla Conte, Lassine Kouma ambao wote wametua Yanga wakati awali walikuwa katika hesabu zake.
Kama haitoshi, Fadlu alitamani sana kuwa na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ msimu huu na alihakikishiwa kwamba staa huyo anaweza kuletwa, lakini haikuwa hivyo na mbaya zaidi akapata taarifa kwamba, changamoto za kumkosa ilitokana na makosa ya baadhi ya viongozi ambao walishindwa kusimamia vyema mazungumzo hayo.
Fadlu pia alitaka mshambuliaji wa maana kule mbele, lakini ikashindikana badala yake dakika za mwisho akapatikana Jonathan Sowah ambaye hata hivyo alitua katika kikosi chake akiwa na adhabu ya kusimamishwa.
Kwa changamoto hizo Fadlu anaona kwamba alishindwa kuwa imara mbele ya Yanga na kuingia katika mchezo huo akiwa na safu iliyopungua makali ya ushambuliaji ikimtegemea Steven Mukwala pekee kama chaguo la kwanza na kushindwa kumpa huduma aliyotaka.
Licha ya kuletwa kwa Seleman Mwalimu ‘Gomez’, naye alikuja kwa kuchelewa na akashindwa kuleta nguvu kubwa kwenye mchezo huo ambao ulimnyima raha alipofungwa kwa mara ya nne mfululizo.
UCHOVU BOTSWANA
Safari ya Simba kwenda Botswana nayo imetajwa katika mchafuko wa Fadlu ndani ya timu hiyo hasa baada ya kutumia zaidi ya saa 25 kufika jijini Francistown ambako ndiko mchezo dhidi ya Gaborone United ulichezwa.
Fadlu anayetoka Afrika Kusini anaona kutoka Tanzania kwenda Botswana haikutakiwa kutumia muda mrefu namna hiyo kama mambo yangenyooshwa vizuri hasa ukizingatia kwamba timu yake ilikuwa inatoka kwenye ratiba ngumu ya kucheza na kupoteza dhidi ya Yanga.
Uchovu wa safari hiyo Fadlu aliona mapema kwamba kikosi chake kinaweza kuwa na mchezo usiovutia na hivyo kuzidi kuingia nyongo na mabosi wake na kweli juzi usiku licha ya kushinda 1-0 mbele ya Gaborone United, timu haikucheza vile ilivyotarajiwa au kuzoeleka ikicheza CAF.
OFA YA WAARABU
Ofa kubwa iliyotibua kila kitu ni kurejea kwa Raja Athletic kutoka Morocco ambao walikuja na nguvu kubwa kutaka kumrudisha kocha huyo.
Kumbuka Fadlu aliwahi kuishi Morocco akiwa hapo Raja ambao aliwahudumia kama kocha msaidizi akiwaachia ubingwa wa Ligi Kuu na Waarabu hao waliwahi kutaka kumrudisha hapo msimu uliopita lakini hawakukubaliana.
Msimu huu Raja imeshuka na ofa nzito ikimpa mshahara mkubwa mara tatu ya ule anaolipwa Simba lakini kama haitoshi ikamwambia atakwenda na wasaidizi wake atakaowapendekeza.