Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makocha watano upepo umebadilika Bara

WAMEBADILI Pict


MBINU na ushawishi wa benchi la ufundi ni jambo la kwanza la mafanikio ya timu uwanjani. Wakati wachezaji kama Allan Okello wa Yanga akionyesha maajabu yake kwa kuhusika kwenye mabao 14 katika Ligi Kuu Bara msimu huu akitua dirisha dogo la usajili Januari 2026 ambapo amefunga saba sawa na asisti, upepo wa matokeo kwa timu nzima huamuliwa na akili ya mtu anayesimama mstari wa mbele kuwaongoza wenzake ndani ya benchi la ufundi.


Msimu huu wa 2025-2026 umeshuhudia mapinduzi makubwa ya kiufundi yaliyofanywa na makocha wakuu watano ambao wamegeuza nyakati ngumu kuwa sherehe na kurejesha matumaini kwa klabu yao.

WAMEB 02

STEVE BARKER

Kurejesha utambulisho na ushindani wa kweli baada ya vipindi vya mtikisiko chini ya makocha waliopita kama Dimitar Pantev, kutua kwa Steve Barker pale Msimbazi mwezi Desemba 2025 kumeibua mapinduzi makubwa mno.

Pantev alitaka timu icheze soka la kukimbia muda wote jambo lililoharibu falsafa ya jadi ya Simba ya kumiliki mpira kwa pasi fupi na utulivu. Steve Barker amefanikiwa kuirudisha Simba kwenye misingi yake.

Amewapa uhuru viungo kama Clatous Chama na matokeo yake yanaonekana wazi uwanjani. Chini ya uongozi wake, Simba imeimarika sana na kujenga mfululizo wa mechi 19 bila kupoteza kwenye ligi kuu, huku ushindi wa hivi karibuni wa mabao 4-0 dhidi ya Tanzania Prisons ukithibitisha ukali wa safu yake ya ushambuliaji. Barker hajajenga tu timu inayoshinda, bali ametengeneza kikosi chenye nidhamu ya ulinzi inayompa kipa Djibrilla Kassali utulivu wa kutosha.

Kabla ya kucheza na Coastal Union, Simba ilikuwa na pointi 52 ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku ikiibua matumaini ya kubeba ubingwa baada ya awali kuwa mbali zaidi na tumaini hilo.

WAMEB 04

FLORENT IBENGE

Mfumo wa ushindani kutoka kwa Florent Ibenge ndani ya viunga vya Azam Complex kumeondoa ule unyonge wa matajiri wa lambalamba kuitwa “wasindikizaji wa dabi.”

Ibenge, akitumia mfumo wake unaoupenda wa 4-2-3-1, amejenga utulivu mkubwa kwenye eneo la kiungo na ulinzi.

Makocha wengi waliopita Azam walishindwa kuhimili presha ya mechi kubwa, lakini Ibenge ametumia uzoefu wake mkubwa wa soka la Afrika kuwajenga wachezaji kiakili. Azam kwa sasa inacheza soka la kueleweka, wakitawala michezo na kupunguza makosa.

Kupitia mbinu zake, Azam imejikita thabiti katika nafasi tatu za juu, ikizisogelea Simba na Yanga kwa ukaribu mkubwa, huku ikionyesha kandanda safi lenye usawa kati ya kuzuia na kushambulia ilipocheza na wakongwe hao msimu huu.

Azam Ijumaa hii inaikaribisha Tanzania Prisons na sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 46.

WAMEB 05

FREDY MINZIRO

Mfalme wa mbinu za ndani linapokuja suala la kuokoa timu na kuzifanya zicheze soka lenye matokeo chanya bila kutegemea bajeti kubwa ya usajili, jina la mzawa Minziro linasimama pekee.

Fountain Gate ilikuwa kwenye kipindi kigumu cha kupoteza mwelekeo na pointi mfululizo, jambo lililoweka rehani nafasi yao kwenye ligi. Minziro amebadili upepo kwa kutumia mbinu rahisi lakini zenye ufanisi wa hali ya juu.

Taratibu ameanza kuijenga timu hiyo kutoka eneo la chini kuja juu ambapo jana ilikuwa dimbani kucheza dhidi ya JKT Tanzania. Kabla ya mechi hiyo, Fountain Gate iliyokuwa ikinolewa na Mohamed Ismail ‘Laizer’ kabla ya ujio wa Minziro, ilikuwa nafasi ya 12 ikikusanya pointi 25, bado haipo salama sana kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, hivyo kazi bado anayo Minziro.

Kocha huyo tangu atue hapo, ameiongoza katika mechi sita za Ligi Kuu Bara, akishinda tatu na kupoteza tatu.

Ushindi wa mechi mbili mfululizo dhidi ya Coastal Union na KMC kwa matokeo ya kufanana mabao 3-2, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Fountain Gate kushinda mfululizo, kwani kabla ya hapo, watangulizi wake, Denis Kitambi na Laizer hawakufanikiwa.

WAMEB 01

JAMHURI KIHWELO

Mashujaa kutoka Kigoma imekuwa moja ya timu ngumu zaidi kufungika katika mzunguko huu wa pili hasa kuanzia Februari 2026 alipotua Jamhuri Kihwelo maarufu Julio.

Julio ameingiza utamaduni wa kupambana bila woga ndani ya kikosi chake. Mashujaa chini ya Julio haitazami jina la mpinzani, iwe inacheza dhidi ya Simba, Yanga au timu nyingine, nidhamu ya kupambana imekuwa silaha yao kuu.

Kocha huyo amebadili upepo wa matokeo kwani kabla ya kufungwa na Simba nyumbani 3-0 kwenye ligi, timu hiyo ilikuwa haijapoteza msimu huu ikiwa Lake Tanganyika. Baada ya hapo, ikafungwa tena 1-0 na Azam katika robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

Hata hivyo, Julio kabla ya hapo, alikuwa ameiongoza Mashujaa katika mechi tisa bila ya kupoteza, akishinda tatu na sare sita.

Mtihani alionao Julio ni kuhakikisha anaiweka salama Mashujaa iliyopo nafasi ya tisa na pointi 27, licha ya kuonekana ipo mbali zaidi na eneo la kushuka daraja, lakini kiuhalisia tofauti ya pointi dhidi ya timu iliyopo kwenye mstari wa kuepuka kushuka daraja kwa mechi za playoff, inaiweka hatarini.

WAMEB 03

MUHIBU KANU

Baada ya Singida Black Stars kufungwa 2-0 na TRA United, Aprili 5, 2026, benchi la ufundi la timu hiyo likavunjwa, ndipo Muhibu Kanu akakabidhiwa mikoba ya kuiongoza timu hiyo.

Aprili 8, 2026, Singida ikaanza na ushindi wa bao 1-0 na hadi sasa, kocha huyo ameiongoza katika mechi nane za mashindano tofauti, akishinda tano, sare moja na kupoteza mbili.

Singida inayoshika nafasi ya nne na pointi 38, imeondoshwa kwenye Kombe la Shirikisho la CRDB, hivyo Kanu ana kazi ya kufanya kuhakikisha timu hiyo inabaki ndani ya nne bora ikipambana kurudi tena kimataifa msimu ujao.

Hata hivyo, Kanu kwa kushirikiana na Papy Kimoto aliyepewa kazi ya kuwa meneja mkuu kikosini hapo, wanaweza kufanikisha hilo kwani mwelekeo unaonekana kutokana na mabadiliko yaliyopo.

Katika ushindi wa mechi tano, nne imeshuhudiwa Singida ikitoka bila ya kuruhusu bao, hii inaonyesha namna safu ya ulinzi ilivyojengwa kuwa imara.