Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makocha maarufu wanaonogesha soka la kimataifa

MAKOCHA Pict

Muktasari:

  • Achana na timu hizo za taifa kukusanya wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa kutoka kwenye timu za klabu mbalimbali, lakini jambo kubwa ni kuhusu makocha wanaozinoa timu hizo kwa sasa, wengi maarufu.

LONDON, ENGLAND: KUNA sababu kibao tamu zinazofanya soka la mechi za timu za taifa kuwa na mvuto mkubwa kwa mashabiki wa mchezo huo duniani.

Achana na timu hizo za taifa kukusanya wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa kutoka kwenye timu za klabu mbalimbali, lakini jambo kubwa ni kuhusu makocha wanaozinoa timu hizo kwa sasa, wengi maarufu.

Soka la timu za taifa sasa limekuwa na mvuto kama lilivyo tu la klabu kutokana na makocha waliopewa dili za kuzinoa timu hizo. Ni makocha maarufu, mafundi na wenye majina makubwa.

Mataifa makubwa kwenye soka kama Brazil, England na Ujerumani yameingia dili za kuajiri makocha wenye uzoefu, mashuhuri na maarufu ili kuzifanya timu zao kuwa na ubora na yamekuwa yakiwalipa pesa nyingi kufanya kazi kwenye timu zao na kuachana na klabu.

Hii hapa orodha ya makocha 10 maarufu waliopo kwenye timu za soka za taifa ambao wanaongeza mvuto katika kandanda la kimataifa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026.

MAKO 10

10. Ralf Rangnick (Austria)

Austria ilionyesha kiwango bora sana katika michuano ya Euro 2024, ambapo ilikuwa ikicheza staili ya soka la klabu, kukabia juu na kuzipa timu ngumu kama Ufaransa na Uholanzi wakati mgumu zilipokutana.

Kipigo walichokutana nacho kwenye 16 bora dhidi ya Uturuki ilikuwa bahati mbaya, kwa sababu Austria ilicheza kwa kiwango bora, huku nyuma ya jambo hilo yupo kocha mashuhuri, Ralf Rangnick.

Kocha huyo mwenye uzoefu wa kuibua vipaji vingi, anajiandaa kuipeleka Austria kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998.

MAKO 09

9. Ronald Koeman (Uholanzi)

Ronald Koeman ni kocha mwingine mashuhuri anayefanya kazi kwenye soka la timu ya taifa akiwa na kikosi cha Uholanzi, ambacho kilifika nusu fainali ya Euro 2024.

Kwenye kikosi chake kuna mastaa mahiri kama Virgil van Dijk, Xavi Simons na Cody Gakpo, ambao wamekuwa na kiwango bora kabisa sambamba na Tijani Reijnders, Frenkie de Jong na Ryan Gravenberch.

Koeman anatarajia kuiongoza Uholanzi kwenye mchakamchaka wa kufuzu gainali za Kombe la Dunia 2026.

MAKO 08

8. Roberto Martinez (Ureno)

Baada ya kushindwa kukika ubingwa wa taji lolote kikosi cha dhahabu cha Ubelgiji, kocha maarufu Roberto Martinez, alibamba ajira ya kwenda kuinoa Ureno tangu 2023.

Kwenye kikosi cha Ureno alifika nacho robo fainali ya Euro 2024, lakini aliisaidia kushinda ubingwa wa Nations League 2025.

Kama alivyo maarufu, kocha huyo kikosi chake kimejaa wachezaji maarufu pia akiwamo Cristiano Ronaldo, ambaye amekuwa kwenye kiwango bora akipambana akacheze Kombe la Dunia 2026. Kocha Martinez analipwa mshahara wake Pauni 3.5 milioni kwa mwaka.

MAKO 07

7. Marcelo Biesla (Uruguay)

Akiwa tayari mwenye uzoefu mkubwa kwenye soka la timu za taifa alipokinoa kikosi cha Argentina, kocha fundi wa boli, Marcelo Bielsa kwa sasa ni kocha wa Uruguay, ambako amekuwa akifanya kazi tangu 2023.

Huko Leeds United, kocha huyo bado anapendwa kwelikweli kutokana na staili yake ya soka alilokwenda kufundisha mahali hapo, pasi nyingi na mpira wa kutandaza ardhini.

Bielsa ni miongoni mwa makocha maarufu kwenye soka la dunia, ambao ameoondoka kwenye klabu na sasa anafanya kazi katika timu ya taifa.

MAKO 06

6. Luis de la Fuente (Hispania)

Luis de la Fuente ni kocha mwingine maarufu, ambaye mashabiki wangetarajia kuwaona kwenye soka la klabu, lakini anapiga mzigo katika timu ya taifa ya Hispania.

Uzuri wa kikosi chake kuna mastaa wenye vipaji vya hali ya juu kama Lamine Yamal na Nico Williams kwa kuwataja kwa uchache, ambao wanaweza kwenda kuisaidia Hispania kufanya vizuri kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kubeba ubingwa wa Euro 2024 kwa staili ya soka la kibabe.

Mataifa mengi makubwa ikiwamo Ujerumani, Italia, Ufaransa na England zote zinashindwa namna ya kuikabili Hispania ya De la Fuente.

MAKO 05

5. Didier Deschamps (Ufaransa)

Didier Deschamps amekuwa kocha wa kikosi cha Les Bleus tangu 2012, akiandaa kikosi hicho kuwa cha kibabe Ulaya na duniani.

Ni mmoja wa makocha wa timu za taifa waliodumu kwenye timu moja kwa muda mrefu, akishinda Kombe la Dunia na UEFA Nations League, huku akifika pia kwenye fainali ya michuano mikubwa na kupoteza.

Kinachokosolewa kwa Deschamps ni staili yake ya uchezaji ya kikosi cha Ufaransa, ambacho kina mastaa wengi wa viwango bora kabisa, ambao mashabiki wa soka wanaamini, timu ingepaswa kuwa tishio zaidi.

MAKO 04

4. Lionel Scaloni (Argentina)

Argentina ilikuwa kwenye hali mbaya wakati Lionel Scaloni anachukua mikoba mwaka 2018, ambapo ilitokea kufanya hovyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Russia licha ya kuwa na huduma ya mchezaji wa soka mwenye kipaji kikubwa zaidi, Lionel Messi kwenye timu yao.

Mataji mawili ya Copa America na moja la Kombe la Dunia alilokuja kubeba baadaye, yamemfanya kocha huyo kuwa mashuhuri huku ufundi wake ulitazamiwa kuonekana kwenye timu za klabu, lakini anapiga mzigo katika soka la timu za taifa.

MAKO 03

3. Julian Nagelsmann (Ujerumani)

Baada ya kufutwa kazi Bayern Munich mwaka 2023, Julian Nagelsmann alirudi kufanya kazi kwenye timu ya taifa ya Ujerumani, akichukua mikoba ya kuinoa miamba hiyo.

Alioongoza Ujerumani kufika robo fainali kwenye Euro 2024 na sasa ana majukumu mazito ya kuhakikisha anaondoa bahati mbaya ya Ujerumani ya kukomea kwenye hatua ya makundi katika fainali mbili mfululizo zilizopita za Kombe la Dunia.

Ujerumani ipo kwenye msako wa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2026, ambapo imepangwa kundi moja na timu za Northern Ireland na Slovakia.

MAKO 02

2. Thomas Tuchel (England)

Thomas Tuchel ni kocha wa kwanza wa kigeni kuwahi kuinoa England tangu Fabio Capello alipoachana na timu hiyo na amekuwa akilipwa mshahara mkubwa kuhakikisha timu hiyo inabeba taji jingine kubwa baada ya kunyakua Kombe la Dunia 1966.

Kwenye soka la klabu, Tuchel aliwahi kuzinoa Chelsea, PSG na Bayern Munich kwa mafanikio makubwa na hilo ndilo lililoifanya England kuamini anaweza kwenda kuhamishia mafanikio hayo kwenye kikosi cha Three Lions baada ya kuona Gareth Southgate kushindwa mara kadhaa licha ya kuifikisha fainali ya michuano ya Ulaya timu hiyo.

Tuchel ameonyesha jeuri ya kutokuwa na woga wa kuwapiga chini mastaa wenye majina makubwa kama Jude Bellingham, Phil Foden na Jack Grealish.

MAKO 01

1. Carlo Ancelotti (Brazil)

Carlo Ancelotti alichukua mikoba ya kuinoa timu ya taifa ya Brazil mwaka huu baada ya kuachana na Real Madrid mkataba wake ulipofika tamati mwishoni mwa msimu uliopita.

Kwa muda mrefu Brazil ilikuwa ikimfukuzia kocha huyo, ambaye amejitengenezea umaarufu mkubwa kwenye soka la klabu akibeba mataji kibao ikiwamo makubwa kabisa kama ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na timu tofauti.

Mara ya mwisho Brazil kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia 2002, hivyo imempa ajira Ancelotti na kumpa mshahara mkubwa wakitaka akafanye jambo kubwa kwenye fainali zijazo za Kombe la Dunia 2026 huko Marekani.