Machotara wanahitajika sana Taifa Stars
Muktasari:
- Nadhani mnajionea wenyewe wale DR Congo sasa wanajivunia kufuzu Kombe la Dunia kwa kubebwa na mchango wa Diaspora wao 18 ambao walikuwa miongoni mwa wachezaji 26 wa kikosi kilichofuzu.
MPANGO wa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi kuzunguka maeneo mbalimbali duniani kusaka wachezaji wenye asili ya Tanzania una tija sana.
Hapa kijiweni tunaamini kwamba hadi Gamondi amepanga kitu kama hicho basi ana uhakika kwamba wapo wachezaji wa namna hiyo katika nchi tofauti hasa huko Ulaya.
Uwepo wa hawa wachezaji ambao mtaani tunawaita machotara ingawa kwa lugha sahihi ya kisomi wanajulikana kama Diaspora utakuwa na mchango mkubwa kwa Taifa Stars hivyo tunaunga mkono wakiwepo.
Kwanza aina hii ya wachezaji wanakuwa wamekulia katika misingi mizuri ya soka hivyo uwezo wao wa kutafsiri mbinu na mipango ya benchi la ufundi unakuwa wa hali ya juu kulinganisha na wachezaji wetu wengi waliozaliwa hapa nchini.
Nidhamu na kuishi kiweledi, ni jambo lingine ambalo linaweza kuwa faida chanya ya uwepo wa Diaspora wengi katika kikosi cha Taifa Stars. Hii ni hulka ambayo uwepo wao utaweza kuwaambukiza wengine.
Na jambo la tatu ni kuzidi kuipandisha thamani timu yetu ya taifa. Hawa wachezaji uwepo wao utaifanya Taifa Stars ifuatiliwe huko katika nchi zao, fursa ambayo inaweza kuwabeba na wachezaji wengine ambao bado hawajapata nafasi ya kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa.
Kama mataifa makubwa kisoka barani Afrika ambayo yana vituo vya kisasa vya soka vya kukuzia vipaji vya vijana, yanaamini katika kutoa fursa kubwa kwa Diaspora, kijiwe hakioni sababu kwa sisi Tanzania kutofanya hivyo.
Yaani haiwezekani hayo mataifa ambayo yana kila kitu kisoka yaone umuhimu wa kuwapa fursa kubwa Diaspora halafu kina sisi huku tushindwe kufanya hivyo.
Nadhani mnajionea wenyewe wale DR Congo sasa wanajivunia kufuzu Kombe la Dunia kwa kubebwa na mchango wa Diaspora wao 18 ambao walikuwa miongoni mwa wachezaji 26 wa kikosi kilichofuzu.