Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mastaa wanavyoshirikiana na wazazi wao kimuziki

Muktasari:

  • Mastaa kama Zuchu, Diamond Platnumz, Lulu Diva na Nandy, ni miongoni mwa wanamuziki wa Bongofleva waliowahi kushirikiana na wazazi wao katika kazi zao za muziki.

WANAMUZIKI wengi wamekuwa wakishirikiana wao kwao kwao katika nyimbo zao ili kupata matokeo bora zaidinlakini kwa muda wanashirikiana hadi na wazazi wao ili kufikisha ujumbe fulani maalum.

Mastaa kama Zuchu, Diamond Platnumz, Lulu Diva na Nandy, ni miongoni mwa wanamuziki wa Bongofleva waliowahi kushirikiana na wazazi wao katika kazi zao za muziki.

Zuchu, mwimbaji wa WCB Wasafi ambaye ni mtoto wa Malkia wa Taarabu nchini, Khadija Kopa, alimshirikisha mama yake katika wimbo wake unaokwenda kwa jina la Mauzauza, ambao katika video yake pia alionekana vizuri tu.

Wimbo huo unapatika kwenye Extended Playlist (EP) iliyomtambulisha, I Am Zuchu iliyotoka Aprili 15, 2020 ikiwa na nyimbo saba na kupata mapokezi makubwa upande wa mauzo mtandaoni huku akiweka rekodi nyingi katika chati mbalimbali za muziki.

Hiyo ndio ilikuwa kolabo ya kwanza kubwa kwa Zuchu kama msanii wa Bongofleva ndipo zikafuata nyingine alizofanya na wasanii kama Mbosso, Diamond, Rayvanny na Joeboy kutokea Nigeria.

Kwa kipindi hicho, ni wazi Zuchu alijua nguvu ya Mama yake katika muziki inaweza kusogeza talanta yake, na Khadija Kopa alijua huo utakuwa mwanzo mzuri kwa mtoto wake ambaye sasa amekuwa mwanamuziki mwenye ushawishi mkubwa.

Ni kitu ambacho anakijua pia mwanamuziki wa Pop na RnB kutokea Marekani, Beyonce Knowles ambaye anaendesha kumtengeneza mtoto wake wa kwanza wa kike, Blue Ivy Carter kuja kuwa mwimbaji mkubwa siku mbeleni.

Ikumbukwe Beyonce kwenye albamu yake iitwayo The Lion King: The Gift, amemshirikisha Blue Ivy ambaye amesikika katika wimbo 'Brown Skin Girl' ambao msanii wa Nigeria, Wizkid amesikika pia, na ni wimbo ulioshinda tuzo ya Grammy.

Tukiachana na hilo, pia kuna mtindo wa wasanii kushirikiana na wazazi wao katika video za nyimbo zao ili kuweza kufikisha ujumbe kwa uhalisia zaidi, ambapo Diamond, Lulu Diva na Nandy ni kati ya waliofanya hivyo.

Desemba 2015, Diamond alitoa video ya wimbo 'Utanipenda' ambayo ilifanyika Dar es Salaam, Tanzania na Johannesburg, nchini Afrika Kusini. Mama yake mzazi, Bi. Sandra maarufu kama Mama Dangote alicheza uhusika wa maisha atakayoishi siku ambayo msanii huyo atakapofilisika kimuziki na kiuchumi.

Pia katika video hiyo mrembo Zari The Bosslady ameonekana ambaye ni Mama wa Tiffah na Nillan, watoto aliyejaliwa na mwimbaji huyo kipindi cha mahusiano yao yaliyodumu kwa takribani miaka minne.

Mnamo Aprili 2021, Lulu Diva aliachia video ya wimbo wake 'Mama' ambao ulikuwa kwa ajili ya mama yake ambaye alikuwa akiugua kwa kipindi kirefu. Mama yake alifariki Desemba 2021 jijini Dar es Salaam.

"Mama yangu anatoa sapoti kubwa sana japo hawezi kufanya vitu vingi kwa sababu sasa hivi ni mgonjwa, anapenda kuniambia nisikate tamaa, nifanye kazi kwa bidii, na nipambane halafu ana neno lake moja ambalo anapenda kuniambia kwamba nisifananishe kifo na usingizi," alisema Lulu Diva kipindi mama yake akiwa hai.

Ikumbukwe kabla ya muziki, Lulu alianza upande wa uigizaji ambapo filamu yake ya kwanza kucheza inakwenda kwa jina la Nikabu (2016), baada ya kupewa fursa hiyo na mwigizaji maarufu, Kitale a.k.a Mkude Simba.

Baadaye Lulu Diva alikutana na Barnaba ambaye alimwandikia wimbo wake wa kwanza kumpatia mafanikio kama mwanamuziki, Milele (2016), mradi uliokuja baada ya wawili hao kukutanishwa na Belle 9. Na kipindi Nandy anaanza kupata umaarufu katika muziki, wimbo wake wa pili kuachia, katika video yake iliyotoka Februari 2017, baba yake Charles Mfinanga alitokea.

Baba mzazi wa Nandy alionekana katika video ya wimbo wa mwanamuziki huyo, One Day (2017), lakini wazazi wake wote walikuja kuonekana katika video ya kolabo yake na mumewe Billnass, Bye (2022) ambao ulikuwa maalum kwa ajili ya ndoa yao.

Utakumbuka kabla ya Nandy kusikika kimuziki hasa chini ya Tanzania House of Talent (THT), aliwahi kuwa mmoja wa waimbaji kwenye bendi ya Banana Zoro, B Band kwa kipindi fulani. Baadaye alikuja kuvuma kwa mara ya kwanza kupitia wimbo wake, Nagusagusa (2016) uliandikwa na mtayarishaji wa wimbo huo, Ima The Boy.