LAZIMA KIELEWEKE! Makinda saba waliopandishwa kuokoa jahazi Manchester United
Muktasari:
- Hicho kilikuwa kipigo cha 12 kwenye mechi 25 ilizocheza kwenye Ligi Kuu England msimu huu na ipo pointi 12 tu juu ya timu zilizopo kwenye hatari ya kushuka daraja, ikiwa imeshika nafasi ya 15 kwenye msimamo.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United ya majanga ilikosa mastaa wake 12 wa kikosi cha kwanza kwenye mechi ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur, Jumapili iliyopita.
Hicho kilikuwa kipigo cha 12 kwenye mechi 25 ilizocheza kwenye Ligi Kuu England msimu huu na ipo pointi 12 tu juu ya timu zilizopo kwenye hatari ya kushuka daraja, ikiwa imeshika nafasi ya 15 kwenye msimamo.
Mara ya mwisho mambo kuwa mabaya kama hivi kwenye kikosi hicho cha Man United, miamba hiyo ya Old Trafford ilishuka daraja.
Kufanya mambo kuwa mabaya zaidi, mastaa ambao ni tegemeo lao kubwa, Amad Diallo na Lisandro Martinez ni majeruhi na watakuwa nje ya uwanja kwa sehemu yote ya msimu iliyobaki.
Jambo hilo lilimfanya kocha Ruben Amorim kuita makinda wanane, ikiwamo saba wa kutoka kwenye akademia ya klabu hiyo kukaa kwenye benchi kama wachezaji wa akiba katika mchezo wao huo wa ugenini dhidi ya Spurs.
Alifanya mabadiliko ya mchezaji mmoja tu, alipomwingiza kinda Chido Obi kwenye dakika za majeruhi – uamuzi ambao ulionyesha jinsi timu hiyo inavyopita kwenye wakati mgumu kwa kubaki na wachezaji walewale walioanza kwa mechi nzima licha ya baadhi kuonyesha kuchoka.
Wakati wengi wakishindwa kupata majibu juu ya mwelekeo wa msimu wa Man United, kocha Amorim alisema hivyo ndivyo mambo yanavyokuwa pindi kila kitu kinapokwenda kombo.
Sasa matumaini ya kocha huyo kwenda kuokoa msimu wa Man United yamebaki kwa makinda wa timu hiyo, wapandishwe kucheza kikosi cha kwanza kama ilivyo kwenye utamaduni wa miaka 87 wa klabu hiyo.
Man United imekuwa na kawaida ya kupandishwa walau mchezaji mmoja anayehitimu kutoka kwenye akademia yao tangu ilipoanza kufanya hivyo kuanzia kwa Tom Manley na Jack Wassall walipopandishwa Team A mwaka 1937.
Makinda hao waliofahamika kama The Busby Babes wakati huo walikwenda kutawala soka la Ulaya mwaka 1968 baada ya janga la ajali ya ndege ya Munich iliyoondoka na maisha ya watu wengi, wakiwamo wachezaji wao vijana ambao ilikuwa imewaibua miaka 10 iliyopita.
Hiyo ilikuwa kurudi nyuma mechi 4,279 – na kikosi kilikuwa na majina kama ya Bobby Charlton, George Best, Mark Hughes, Paul Scholes, David Beckham na Marcus Rashford miongoni mwa mazao yaliyozaliwa kutokea kwenye akademia ya miamba hiyo ya Old Trafford.
Historia ya kutengeneza makinda kwenye timu hiyo ilianzia kwenye uwanja wa Cliff na kisha baadaye Carrington na ilikuwa na mchango mkubwa wa kuibua wachezaji wa kuja kuisaidia Man United kwenye nyakati ngumu.
Shukrani kubwa kwa bosi wa akademia wa sasa, Nick Cox na timu yake matata kabisa, ambao wameendelea kufanya kazi kubwa walau ya kuwapa mashabiki kitu cha kujivunia kuhusu timu yao, kwamba bado inapika watu wa maana.
Amorim anafahamu wazi anapaswa kuwa makini kwenye usimamizi wa makinda hao, kwamba asiwaharakishe sana, lakini kutokana na klabu kuwa kwenye matatizo ya kifedha, kutokana na matumizi yasiyofaa kwenye usajili huko nyuma, jambo ambalo litaweka kwenye wakati mgumu wa kusajili wenye uwezo wa kufiti kwenye mfumo wao, hivyo, itahitaji akademia yao kufanya jambo.
Amorim aliamini sana makinda alipokuwa Sporting Lisbon, na safari hii bila ya shaka atalazimika kuliishi hilo Man United. Lakini, je ni makinda gani hao ambao Amorim atalazimika kuwategemea kuiokoa Man United msimu huu?
Jack Moorhouse – miaka 19
Jack Moorhouse alikuwa habari ya mjini wakati ilipotangazwa atakuwamo kwenye kikosi cha kwanza kilichosafiri kwenda kucheza na Tottenham baada ya viungo wanne wa kikosi cha kwanza cha timu hiyo wote kuwa majeruhi.
Moorhouse alifunga mara mbili kwenye mechi ambayo Amorim alikwenda kuitazama wakati kikosi cha Under-21 kilipoichapa Southampton 5-1 Desemba.
Akitumika kwenye kiungo ya juu, Moorhouse amekuwa kipenzi kutokana na upekee wake katika kuumiliki mpira na wengi wamekuwa wakimwita Paul Pogba II na analinganishwa pia na Morgan Rogers.
Kutokana na majeruhi katika kikosi cha Man United, Moorhouse anaweza kupewa nafasi ya kucheza kwenye mtindo wa kutumia Namba 10 wawili na akaleta matokeo.
Harry Amass – miaka 17
Ni mmoja wa makinda maarufu sana kwenye kikosi cha Man United, ambao mashabiki wamekuwa wakiwaamini kuna kitu wanaweza kufanya katika kuisaidia timu ya wakubwa.
Amass amekuwa akitazamwa kama staa wa Man United kwa miaka ya baadaye. Beki huyo wa kushoto amekuwa akilinganishwa na wachezaji wengi wa kiwango cha juu, akiwamo Luke Shaw na kitu ambacho kimekuwa kikielezwa mkali huyo, Amass ni mmoja wa makinda wanaovutia kuwatazama.
Alishawahi kuteuliwa kwenye kikosi cha kwanza huko nyuma, alipojumuishwa katika kikosi cha Europa League mwanzoni mwa msimu huu.
Kutokana na Tyrell Malacia kutolewa kwa mkopo, Amorim anaweza kumtumia sasa Ammas katika kubadilishana nafasi na beki mpya, Patrick Dorgu.
Jack Fletcher – miaka 17
Mtoto wa kiungo wa zamani wa Man United, Darren Fletcher na kinda huyo amefuata nyayo za baba yake kucheza nafasi ya kiungo. Alinaswa kutoka kwenye akademia ya Manchester City kwenye majira ya kiangazi 2023 pamoja na pacha wake, Tyler.
Amekuwa kwenye kiwango bora sana katika timu za watoto, akichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi wa PL2, huku mara yake ya kwanza kuitwa kwenye kikosi cha kwanz ilikuwa kwenye mechi dhidi ya Brentford.
Fletcher anatumia mguu wa kushoto na amekuwa na uwezo wa kucheza kiungo wa boksi moja hadi boksi nyingine. Amorim atakuwa na chaguo kubwa zaidi kwa kuwa naye kwenye kikosi.
Elyh Harrison – miaka 18
Idara ya makipa ni eneo ambalo lilikuwa la mwisho kabisa kwenye kichwa cha Amorim katika usajili wa Januari, lakini majeruhi ya Altay Bayindir na Tom Heaton yamemfanya Andre Onana kubaki kuwa kipa pekee mwenye uzoefu.
Harrison alikuwa kwa mkopo huko Chester hadi Januari, aliporudishwa Man United kuja kuokoa jahazi, licha ya kwamba hatatumika kwenye mechi za Kombe la FA, kwa kuwa alicheza michuano hiyo alipokuwa Chester.
Kiwango chake bora kwenye timu za watoto, kilimfanya ashinde Tuzo ya Wachezaji Bora wa timu ya risevu.
Kocha wa Chester, Calum McIntyre alisema kipa huyo kinda ni wa aina yake.
Tyler Fredricson – miaka 19
Tyler Fredricson si maarufu sana kwa kulinganisha na makinda wenzake. Lakini, ukweli ni mabeki wa kati wachache sana wenye ubora kama wake wa kuwa na akili kubwa ya kushambulia kama wachezaji wa safu hiyo.
Mkataba wake wa kwanza kwenye klabu hiyo alisajili mwaka 2022 na amekuwa akitua hatua kwa hatua kwenye vikosi vya vijana wa miamba hiyo ya Old Trafford.
Fredricson panga pangua amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha timu ya taifa ya England aliifikisha timu fainali ya FA Youth Cup kwa timu za chini ya miaka 18, licha alikosa mechi hiyo ya fainali kutokana na kuumwa. Fredricson anaweza kuwa msaidizi wa makinda wengine Leny Yoro na Ayden Heaven kwenye beki ya Man United hasa kwa kipindi hiki ambacho Martinez ni majeruhi.
Sekou Kone – miaka 19
Sekou Kone alinaswa na Man United kwa ada ya Pauni 1 milioni kutoka klabu ya Guidars ya huko Mali dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana na ameshapandishwa kikosi cha wakubwa.
Kiungo huyo mkabaji alitamba kwenye fainali za Kombe la Dunia 2023 kwa timu za Under-17, alipoisaidia Mali kumaliza fainali hizo kwenye nafasi ya tatu na alitamba pia na kikosi cha Under-18, Aprili 2024.
Amepachikwa jina la Yaya Toure mpya na wengi wanamtazama kama suluhisho la siku la baadaye kwa Man United kwenye sehemu ya kiungo ya kukaba.
Kocha wa Under-21, Travis Binnion alisifu ubora wa kiungo Kone na kusema ni mchezaji wa aina yake, Man United imepata No.6.
Ayden Heaven – miaka 18
Heaven alinaswa kutoka Arsenal kwenye dirisha lililopita la majira ya baridi kwa ada ya Pauni 1.5 milioni na sasa ameingia moja kwa moja kwenye kikosi cha wakubwa. Beki wa kati huyo alikuwa staa kwenye akademia ya Arsenal na alipewa nafasi ya kucheza kikosi cha wakubwa na kocha Mikel Arteta kwenye mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Preston.
Akitumia mguu wa kushoto na kimo cha futi 6 na inchi 2, anatazamwa kama mrithi wa kudumu wa Martinez kwenye upande wa kushoto wa safu ya mabeki ya Man United.
Ana uwezo pia wa kucheza kwenye kiungo na anapokuwa kwenye eheo hilo amekuwa akilinganisha na Patrick Vieira.
Chido Obi – miaka 17
Obi ni kinda ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao kama anavyotaka, tangu alipokuwa kwenye timu ya watoto ya Arsenal na sasa kwenye kikosi cha Man United.
Obi amefunga mabao 12 kwenye mechi tisa za FA Youth Cup na ligi ya Under-18 tangu alipojiunga na Man United, akiongeza mabao yake kwenye kuwa kinara wa mabao wa muda wote akiwa amefunga mara 41 katika michuano ya Ligi Kuu England kwa timu za U18, ikiwamo mabao 10 aliyofunga kwenye mechi moja dhidi ya Liverpool, kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 15 tu.
Alifunga hat-trick ya dakika 15 katika mechi yake ya kwanza Man United na kabla ya kupewa nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha wakubwa dhidi ya Tottenham, alitokea kufunga hat-trick kwenye FA Youth Cup dhidi ya Chelsea. Amorim alisema Obi ni mjanja sana.
Makinda wengine
Kwenye kikosi cha Man United kuna makinda wengi sana, ambao wanaweza kupata nafasi za kucheza kikosi cha wakubwa ndani yam waka huu, ambao ni pamoja na James Scanlon, Shea Lacey, Gabriele Biancheri na Godwill Kukonki. Man United ilimnasa pia beki wa Uruguay, Diego Leon, lakini atajiunga na timu wakati wa dirisha la majira ya kiangazi la mwisho wa msimu.