Lampard na saa ya bahati ya bilioni 3
Muktasari:
- Kocha huyo anayedaiwa kuwa na imani za ajabu amekuwa akibadilisha saa ikiwamo zenye thamani ya zaidi ya Pauni 1 milioni. Lakini kinachoulizwa kwa sasa ni je, hatimaye ameipata saa yake ya bahati zaidi?
CONVETRY, ENGLAND: UNAIJUA siri nyuma ya mafanikio ya kocha wa Coventry City, Frank Lampard, katika Ligi Kuu England? Mwamba anavaa saa ya bahati yenye thamani ya Pauni 879,490 (zaidi ya Sh3.35 bilioni), inayodaiwa kuwa ya bahati kwake katika shughuli za soka.
Kocha huyo anayedaiwa kuwa na imani za ajabu amekuwa akibadilisha saa ikiwamo zenye thamani ya zaidi ya Pauni 1 milioni. Lakini kinachoulizwa kwa sasa ni je, hatimaye ameipata saa yake ya bahati zaidi?
Lampard anadaiwa kuvaa saa zenye thamani kubwa wakati wa mechi tangu Coventry City iliporejea kwenye Ligi Kuu England. Hata hivyo, gwiji huyo wa zamani wa soka la England, ambaye anaamini katika mambo ya ajabu, huenda hatimaye amepata saa anayoiona kuwa ya bahati kwake.
Coventry ilipata ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Newcastle mwanzoni mwa wiki hii, na kuandika ushindi wake wa pili katika msimu huu chini ya Lampard. Kabla ya hapo, timu hiyo iliifunga Nottingham Forest bao 1-0 kwenye Uwanja wa City Ground kabla ya kuanza kwa mapumziko ya wiki tatu ya mechi za kimataifa yaliyopita hivi karibuni.
SIKIA HII
Kwa watu wanaoamini katika ishara za bahati na mikosi, kuimarika ghafla kwa kiwango cha Coventry kunahusishwa na mkusanyiko wa saa za kifahari ambazo Lampard amekuwa akionyesha tangu mwanzo wa msimu mpya. Katika mechi dhidi ya Nottingham Forest na Newcastle, Lampard alivaa saa mpya aina ya Patek Philippe Grand Complications yenye thamani ya Pauni 879,490 (zaidi ya Sh3.35 bilioni).
Saa hiyo yenye namba ya modeli 5316/50P-001 imetengenezwa kwa ustadi mkubwa na ina teknolojia mbalimbali za kupima na kuonyesha muda, huku ikiwa imefungwa kwenye mkanda wenye madini ya platinamu. Hiyo ndiyo saa ghali zaidi ambayo Lampard ameonekana kuivaa tangu Coventry irejee Ligi Kuu England, na inaungana na saa nyingine adimu za aina ya Grand Complications alizonazo katika mkusanyiko wake.
Mwanzoni mwa msimu, Lampard alikuwa akivaa saa aina ya Patek Philippe Nautilus Chronograph yenye namba ya modeli 5980/1R ambayo imetengenezwa kwa dhahabu yenye uzito wa gramu 3.6 na ina mfumo wa kioo cheusi kinachoweza kubadilika rangi kila mara.
Hata hivyo, kocha huyo alibadilisha saa hiyo ya dhahabu yenye thamani ya Pauni 196,560 (zaidi ya Sh692 milioni), baada ya Arsenal kuifunga Coventry mabao 3-0 katika siku ya ufunguzi wa msimu. Mabao ya Arsenal yalifungwa na Kai Havertz, Bukayo Saka na Martin Odegaard.
Katika mchezo uliofuata, Coventry ilipoteza dhidi ya Hull City katika wikiendi ya pili ya Ligi Kuu, ambapo kwenye mechi hiyo, Lampard alivaa saa aina ya Patek Philippe Aquanaut Chronograph yenye namba ya modeli 5968A iliyotengenezwa kwa chuma cha pua na kuunganishwa na mkanda wa mpira mweusi. Saa hiyo ina thamani ya Pauni 102,229 (zaidi ya Sh360 milioni), ikiwa ndiyo ya bei nafuu zaidi katika mkusanyiko wake wa saa za kifahari.
Katika mechi dhidi ya Manchester City na Brighton, ambazo Coventry ilipoteza kwa mabao 1-0 na 5-0 mtawalia, Lampard alivaa Patek Philippe Nautilus yenye namba ya modeli 5711/1A iliyotengenezwa kwa chuma cha pua na ina uso wa bluu unaong'ara kwa mtindo maalumu unaotambulisha modeli hiyo.
Ingawa bei hutofautiana kulingana na aina na nadra ya saa husika, saa hiyo inakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Pauni 113,000 (zaidi ya Sh398 milioni. Kwa ujumla, thamani ya saa nne za Lampard inakadiriwa kufikia Pauni 1.29 milioni (zaidi ya Sh4.5 bilioni).
LAMPARD NA IMANI ZAKE
Inaelezwa kwamba haijulikani kama kubadilisha saa kumekuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya Lampard maarufu pia kama Super Frank au Lamps siku za mechi, lakini kocha huyo wa Coventry amewahi kuzungumzia wazi tabia yake ya kuamini katika mambo ya bahati.
Alipokuwa akiifundisha Chelsea, Lampard alikuwa akifuata ratiba maalumu kila asubuhi, akihofia kwamba mabadiliko hata madogo katika utaratibu wake yangeweza kuathiri matokeo ya mechi.
Akizungumza na runinga ya Chelsea 2019, Lampard alisema: “Wakati mwingine inaweza kuwa jambo gumu kidogo. Namtembeza mbwa wangu katika muda maalumu wa siku fulani. Kabla ya mazoezi, humpeleka kwenye duka la kahawa lililo karibu, hununua kahawa ya kwenda nayo na kisha kumtembeza katika muda na njia ileile. Hakuna jambo la kusisimua sana!”
Aliongeza kuwa kutembea na mbwa wake humsaidia kutuliza mawazo na kuboresha akili, na pia hupenda kwenda mazoezini kama sehemu nyingine ya utaratibu wake. “Ninapenda kumtembeza mbwa wangu mara nyingi na nimegundua kuwa jambo hilo husaidia kuboresha akili. Pia napenda kwenda kwenye mazoezi ya viungo. Hiyo ni sehemu nyingine ya imani zangu.
“Ni lazima nitumie muda uleule kwenye baiskeli ya mazoezi, dakika 50, au nikimbie katika njia ileile. Nisipozingatia ratiba hizo, kwa namna ambayo hata mimi naiona kuwa ya kipuuzi, huhisi kana kwamba huenda ikaathiri matokeo ya mechi. Hata hivyo, wakati mwingine hushindwa kumtembeza mbwa wangu kwa sababu fulani.”
JE, ATAENDELEA KUVAA SAA MPYA?
Coventry sasa inajiandaa kusafiri kwenda kaskazini mwa London kukabiliana na Tottenham Hotspur kesho, Jumatatu, ambako Spurs inaingia katika mchezo huo ikiwa bado haijapata ushindi. Kwa kuzingatia ushindi wa hivi karibuni wa Coventry dhidi ya Nottingham Forest na Newcastle, Lampard huenda asiachane na saa yake mpya ya zaidi ya Sh3.35 bilioni, ambayo baadhi ya watu wanaichukulia kama 'kifaa' chake cha bahati.
Baada ya kuanza kwa msimu kwa matokeo yasiyoridhisha, ushindi mfululizo mara mbili uliopita unaweza kuwa umeongeza imani ya kocha huyo kwamba huenda hatimaye amepata saa inayomletea bahati.
Hata hivyo, kinachobaki wazi ni kwamba Lampard amekuwa na tabia ya kufuata ratiba maalumu na kuamini katika mambo yanayompa utulivu wa akili. Kama saa yake mpya itaendelea kuambatana na ushindi wa Coventry, huenda ikawa vigumu zaidi kuiweka mbali.