Prime
Lamine alipozaliwa mwaka wa Ballon d’Or kuwa ya magwiji watupu
Muktasari:
- Yamal, alizaliwa 2007, mwaka ambao ulishuhudia tano bora ya tuzo ya Ballon d’Or ilihusisha masupastaa watupu kwenye soka, ambao kwa sasa wanahesabika kama magwiji kwenye mchezo huo.
BARCELONA, HISPANIA: KINDA wa Barcelona, Lamine Yamal hakika ndiye mchezaji kijana anayevutia zaidi kumtazama kwa sasa tangu alipoibuka Kylian Mbappe na kabla ya hapo masupastaa wawili, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Yamal, alizaliwa 2007, mwaka ambao ulishuhudia tano bora ya tuzo ya Ballon d’Or ilihusisha masupastaa watupu kwenye soka, ambao kwa sasa wanahesabika kama magwiji kwenye mchezo huo.
Kinda, Yamal kwa kiwango chake cha soka kinavyokwenda, pengine anaweza kwenda kushinda tuzo hiyo kwa miaka ya baadaye na kufuata nyayo za wakali kadhaa, akiwamo Mbrazili, Ricardo Kaka, ambaye alishinda Ballon d’Or kwenye mwaka ambao winga huyo wa Barcelona alizaliwa.
Kutokana na hilo, makala haya yanahusu mahali walipo na wanachofanya masupastaa waliokuwamo kwenye tano bora kwenye tuzo ya Ballon d’Or wakati staa wa Barcelona na Hispania, Yamal anazaliwa mwaka 2007.
5. Andrea Pirlo
Alikuwa kwenye kikosi cha AC Milan sambamba na Kaka, ambaye aliibuka mshindi kwenye tuzo hiyo mwaka huo. Kiungo huyo fundi wa mpira, alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka huu, kabla ya kwenda kujiunga na Juventus ilimpa mafanikio makubwa, akichaguliwa kwenye Timu Bora ya Mwaka kwenye Serie A kwa miaka minne kuanzia mwaka 2011 na kuendelea.
Baada ya kustaafu soka aliingia kwenye ukocha, akipata nafasi ya kuinoa klabu yake ya zamani ya Juventus, mahali ambako hakuwa na mafanikio makubwa sana kama kocha licha ya kushinda makombe mawili. Baadaye alikwenda Uturuki kuinoa klabu ya Fatih Karagümrük, ambayo aliongoza kwenye mechi 34, huku akiwa amepoteza mechi nyingi kuliko alizoshinda. Alienda Sampdoria, lakini baada ya msimu mmoja aliondoka kwenye timu hiyo Agosti 2024 na sasa hana kazi, akivuta muda kutafuta kibarua.
4. Didier Drogba
Fowadi huyo wa Chelsea, Drogba alikuwa kwenye kiwango bora sana mwaka huo, ambapo aliweka rekodi safu ya kufunga mabao katika michuano yote aliyocheza. Alifunga mabao 33 na kuasisti mara 11 katika mechi 60 alizotumikia Chelsea kwa msimu huu na timu yake ilimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, lakini ilifika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya huku akifunga mabao kwenye fainali zote za Kombe la FA na Kombe la Ligi. Baadaye aliondoka Stamford Bridge na kwenda soka huko China, Uturuki na Marekani kabla ya kustaafu na sasa amekuwa akionekana kwenye matukio mbalimbali ya masuala ya soka na kuonekana pia kwenye mechi za hisani. Kwa kiasi kikubwa kitu ambacho Drogba amekuwa akifanya kwa sasa ni kujihusisha na suala la mambo ya hisasi licha ya kuwa kimya kwa kiasi kikubwa katika masuala ya kimpira.
3. Lionel Messi
Licha ya kwamba Barcelona ilishinda Super Cup tu mwaka huo, Lionel Messi alikuwamo kwenye tatu bora ya Ballon d’Or mwaka huo, kama ilivyokuwa kwa mpinzani wake wa miaka mingi, Cristiano Ronaldo, ambaye hakuwa na mafanikio makubwa sana kwa mwaka huo, ambapo ulikuwa mwanzo wao wa kwenda kuchuana jino kwa jino kwenye soka na tuzo hiyo. Kwa upande Messi, alifunga mabao 17 na kuasisti mara tatu katika mechi 36 alizocheza kwenye mechi huo, huku balaa la majeruhi lilimzonga baada ya kupata tatizo kwenye mfupa wa uvungu wa mguu katikati ya msimu. Baada ya hapo, Messi alikuwa moto wa kuotea mbali uwanjani, akishinda mataji ya kutosha ikiwamo mataji matatu makubwa ndani ya msimu mmoja, Kombe la Dunia na tizo saba za Ballon d’Or.
Aliondoka Barcelona kwenda PSG na hakudumu kwa miaka mingi, akatimkia zake MLS anakokipiga kwenye kikosi cha Inter Miami kinachomilikiwa David Beckham. Kwenye kikosi cha Inter Miami, Messi amekutana na wachezaji wenzake wa zamani wa Barcelona, Jordi Alba, Sergio Busquets na Luis Suarez.
2. Cristiano Ronaldo
Supastaa huyu alishika namba mbili kwenye Ballon d’Or mwaka huo, lakini alisubiri kwa mwaka mmoja tu kabla ya kunyakua tuzo hiyo maarufu duniani. Baada ya hapo, alikwenda kunyakua tuzo nyingine na kufikia tano, lakini akiwa mchezaji aliyeshika namba mbili mara nyingi zaidi nyuma ya mpinzani wake wa muda mrefu, Messi.
Ronaldo alifunga mabao 23 na kuasisti mara 14 katika mechi 53 alizocheza mwaka huo na timu yake ya Manchester United ilinyakua ubingwa wa Ligi Kuu England na alichaguliwa kuwa mchezaji bora na alikuwamo kwenye kikosi cha World XI.
Baada ya hapo alikwenda Real Madrid, kisha Juventus kabla ya kurudi Man United na kutimkia zake Saudi Arabia kukipiga kikosi cha Al Nassr. Umri wake wa sasa ni miaka 40 na Ronaldo bado anaendelea kuwatesa makipa uwanjani huko kwenye Saudi Pro League.
1. Kaka
Mshindi wa Ballon d’Or 2007 alikuwa kwenye kiwango bora sana mwaka huo na alishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya, Super Cup na Klabu Bingwa Dunia, huku akiwa amefunga mabao 10 na kuasisti mara tatu katika mechi 13 alizocheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kumbukumbu matata kabisa ya Kaka ni lile bao lake alilofunga uwanjani Old Trafford, ambapo aliwagonganisha mabeki wa Man United kabla ya kufunga kirahisi kabisa katika mechi ya marudiano ya mtoano ya hatua ya 16 bora.
Baadaye aliondoka AC Milan kwenda kujiunga na Real Madrid, ambako alikutana na magwiji kwelikweli wa soka akiwamo supastaa Cristiano Ronaldo. Los Blancos mambo hayakuwa matamu sana, akarudi Milan kabla ya kwenda zake MLS kujiunga na Orlando City na baadaye alienda kumalizia maisha yake ya soka huko Sao Paulo.
Alistaafu soka 2017 na aliweka wazi dhamira yake ya kutaka kwenda kuwa mkurugenzi wa Milan. Kwa sasa amekuwa kimya sana kwenye masuala ya kimpira, akiwekeza guvu zake kwenye biashara na shughuli za kijamii.