Kwaheri Maximo, hili halitasahaulika
Muktasari:
- Kocha huyo aliiongoza KMC katika mechi tisa tu za Ligi Kuu kabla ya kutangazwa kutemeshwa kibarua Desemba 6, ikiwa ni sawa na siku 131 au miezi minne na siku nane tangu alipoajiriwa.
ADIOS Amigo. Adios Maximo. Ndiyo, huu ni msemo wa kihispania wenye maana ya kuagana na rafiki na ndivyo mashabiki wa soka wanavyomuaga rafiki yao. Kocha Marcio Maximo. Kocha huyo raia wa Brazili, amekuja na kuondoka kabla hata hajamaliza msimu wa Ligi Kuu Bara kwa mara nyingine tena.
Ni kama utani. Hii ni mara ya pili, Maximo amekuja nchini na kuondoka kwa aibu bila kutarajiwa.
Maximo aliyejijengea jina na heshima kubwa kwa mashabiki wa soka katika timu ya taifa, Taifa Stars na amedumu katika Ligi Kuu msimu huu kwa muda wa siku 131 tu, akiinoa KMC kabla ya kusitishiwa mkataba kwa makubaliano ya pande mbili na mabosi wa Kino Boyz.
Maximo alitambulishwa na KMC mnamo Julai 28, mwaka huu kama kocha mkuu, ikiwa ni mara ya pili kuja nchini kufundisha klabu ya Ligi baada ya kufanya hivyo mwaka 2014 alipojiunga na Yanga.
Kocha huyo aliiongoza KMC katika mechi tisa tu za Ligi Kuu kabla ya kutangazwa kutemeshwa kibarua Desemba 6, ikiwa ni sawa na siku 131 au miezi minne na siku nane tangu alipoajiriwa.
Kama ilivyokuwa kwa Yanga, namba ndizo zilizomwangusha Maximo akiwa na KMC kwa kushindwa kupata matokeo mazuri na kufifisha tumaini la mabosi wa klabu na mashabiki waliokuwa nao wakati wakimpa ajira Mbrazili huyo aliyepokea mikoba kutoka kwa Kocha Kally Ongala.
Mwanaspoti limekuletea takwimu za Maximo katika siku 131 akiwa na KMC na kurejea kilichomkuta pia Jangwani mwaka 2014 alipopewa mkono wa kwaheri mara baada ya kipigo cha mabao 2-0 ilichopewa Yanga kutoka kwa wataniwao Simba katika pambano la Nani Mtaji Jembe mwaka 2014.
ALIANZA KIBABE
Mara baada ya kukaa na timu kwa karibu miezi miwili, Maximo alianza msimu mpya kibabe kwa kuingoza KMC kupata ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji.
Mechi hiyo iliyochezwa Septemba 17 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge ndio pekee kwa Maximo na jeshi hilo la Vijana wa Kino kutoka na ushindi uwanjani.
VIPIGO MFULULIZO
Mara baada ya mechi hiyo kwa kwanza ya Ligi Kuu, KMC chini ya Maximo haikuonja tena ushindi wowote zaidi ya vipigo sita mfululizo, kisha kujitutuma mbele ya Mtibwa Sugar kwa kutoka nao suluhu kabla ya kupasuka mechi ya tisa ikiwa ugenini jijini Mwanza na kuwa tiketi ya kocha huyo kusitishiwa mkataba, akiwa ameiacha timu mkiani mwa msimamo ikivuna pointi nne tu katika mechi tisa, ikishinda mechi moja, kupoteza saba na kutoka sare moja.
MABAO MAWILI TU
Huwezi kuamini, lakini ndiyo ukweli ulivyo. KMC ya Maximo katika mechi tisa ilizocheza, ilivuna mabao mawili tu, yote yakifungwa na mshambuliaji mzoefu wa ligi hiyo, Daruwesh Saliboko. Alifunga katika mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji na siku ilipofumuliwa mabao 4-1 na watetezi Yanga kwenye Uwanja wa KMC, washindi wakiwa wenyeji na kuifanya timu hiyo na wastani wa 0.2 kwa kila mechi.
UGENINI AIBU TUPU
KMC ya Maximo, imecheza mechi nne za ugenini na zote imepasuka, ikifunga bao moja tu na yenyewe kufungwa jumla ya mabao tisa.
Ilianza kucheza ugenini dhidi ya Maafande wa Tanzania Prisons na kulala 1-0 kabla ya kuifuata Fountain Gate mjini Babati na kulala pia 1-0.
Baada ya hapo ikavaana na Yanga, iliyowafumua mabao 4-1 kabla ya Pamba Jiji kuwanyoosha 3-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jiji Mwanza.
ANGALAU NYUMBANI
Licha ya kuanza na mguu mzuri kwa ushindi katika mechi ya kwanza ikiwa uwanja wa nyumbani, KMC ya Maximo ilionekana pia nyonge hata ikicheza Uwanja wa KMC, kwani ilipoteza mechi zote tatu zilizofuata kabla kuibana Mtibwa Sugar katika mechi ya mwisho ikiwa KMC Complex kwa kuambulia suluhu.
KMC ilianza gundu la nyumbani katika mechi ya pili tu ya msimu huu dhidi Singida Black Stars kwa kulala bao 1-0 kabla Mbeya City kuitia aibu kwa kipigo cha mabao 3-0. Mechi ya nne nyumbani ilikuwa ni dhidi ya Yanga na kugongwa 4-1 safi, ndipo ikaja ikatoka suluhu na Wakata Miwa wa Manungu.
Takwimu zinaonyesha katika mechi tano za nyumbani, KMC ya Maximo ilivuna pointi nne na bao moja na kufungwa matano na kuwa angalau kidogo kwa kulinganisha na mechi za ugenini ambazo haikupata hata pointi moja, lakini ilibahatika kufunga bao moja pia.
ILIVYOKUWA YANGA
Kama umesahau, Maximo alirejeshwa nchini na Yanga kwa mara ya kwanza Juni 26, 2014 baada ya kuacha alama akiwa Taifa Stars aliyoinoa kuanzia mwaka 2006 hadi 2010.
Yanga ilimleta Maximo kuchukua nafasi ya Hans Pluijm aliyeinoa kwa nusu msimu na kutimkia Arabuni akiwa na msaidizi wake, Charles Boniface Mkwasa.
Maximo alitua nchini Juni 26 na kuiongoza Yanga katika mechi tisa pia, ikiwamo moja ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC na kutoka na ushindi wa mabao 3-0, mawili yakiwekwa kimiani na straika Mbrazili aliyeletwa na kocha huyo, Genilson Santos 'Jaja'.
Pia alicheza mechi ya Nani Mtani Jembe iliyopigwa Desemba 13, 2014 ambayo ndio iliyokuiwa tiketi ya kocha huyo kurudishwa kwao kwa kupoteza 2-0 mbele ya Simba, ikiwa ni kipigo cha pili mfululizo kwa Vijana wa Jangwani mbele ya Simba katika michuano hiyo, kwani 2013 ilifumuliwa mabao 3-1.
AANZA LIGI VIBAYA
Tofauti na akiwa na KMC msimu huu, Maximo alipokuwa akiinoa Yanga alianza msimu wa Ligi Kuu vibaya kwa kupoteza ugenini kwa mabao 2-0 mbele ya Mtibwa Sugar.
Katika mechi hiyo kwa wanaokumbuka, ilipigwa Septemba 20, 2014 mabao ya Mtibwa yalifungwa na Mussa Hassan Mgosi na Ame Ali, huku Jaja akikosa penalti iliyotokana na beki Salim Mbonde kuunawa mpira na kipa Said Mohammed 'Nduda' kupangua shuti la Mbrazili huyo aliyeletwa na Maximo sambamba na Andriy Continho. Yanga ilifunga mabao mawili kupitia Simon Msuva na Mrisho Ngassa, lakini yote yalikataliwa na mwamuzi Dominick Nyamisana wa Dodoma, kwa madai ya kuwa wafungaji waliotea na dakika 90 kumalizika kw Maximo kuanza na gundu la kulala 2-0.
Hata hivyo, Yanga ya Maximo ilijitutumua na kushinda mechi mbili mfululizo za nyumbani dhidi ya maafande wa TZ Prisons na JKT Ruvu (sasa JKT Tanzania) kwa kuzifunga mabao 2-1 kila moja.
Baada ya hapo ikabanwa katika mechi ya tatu nyumbani kwa kutoka suluhu na Simba katika Dabi ya Kariakoo kabla kuifuata Stand United mjini Shinyanga na kushinda mabao 3-0.
TAMTAMU HAZIWEZI
Kama ilivyokuwa kwa Mtibwa Sugar iliyowafunga ugenini kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwa mabao 2-0, ndivyo Yanga ya Maximo ilivyoenda kuaibika mjini Bukoba mbele ya Kagera Sugar ilipolala kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Hilo lilikuwa pambano la pili kwa Yanga kupasuka msimu huo chini ya Maximo, zote zikiwa ni dhidi ya Wanatamtamu, timu zinazomilikiwa na viwanda vya kuzalisha sukari.
Maximo alimaliza mechi ya mwisho ya Ligi kabla ya kutimuliwa kupitia Nani Mtani Jembe, kwa kuwanyoa Mgambo JKT kwa mabao 2-0.
Takwimu zinaonyesha katika ligi ya msimu huo, Maximo aliiongoza Yanga katika mechi saba tu, ikishinda nne, kupoteza mbili na kutoka sare moja. Pia timu hiyo ilifunga jumla ya mabao tisa na kufungwa matano.
Ndipo mabao ya Awadh Juma 'Maniche' dakika 30 na lile la Elius Maguri dakika 41 zilihitimisha siku 172 za Maximo akiwa na Yanga katika pambano la Nani Mtani Jembe na baada ya miaka 10 baadae ndipo msimu huu alipokuja tena kuinoa KMC iliyotema Desemba 6 kutokana na matokeo mabaya.
MSIKIE MWENYEWE
Mara baada ya kutemeshwa kibarua, Maximo alizungumza na Mwanaspoti hivi karibuni na kusema, licha ya yaliyotokea lakini kwake ameyapokea kwa mkono mmoja, kwa sababu bado kwa taaluma suala la kuondoka sehemu moja kwenda nyingine ni la kawaida na yupo kiroho safi.
"Ni fahari kwangu kufanya kazi Tanzania kwa sababu ni nchi ninayoipenda, watu wake wanapenda mpira na kiukweli nimeona tangu mara ya kwanza nakuja hapa, Ligi Kuu imepiga hatua, ndiyo maana ni kivutio cha makocha wengi pia," alinukuliwa Maximo.
Maximo alisema kwa sasa ni mapema kuzungumzia kama ataamua kupumzika na masuala la ukocha au ataendelea akipata nafasi sehemu nyingine, licha ya baadhi ya klabu mbalimbali za Tanzania na nje ya nchi kuanza mazungumzo naye.
"Nahitaji muda kidogo wa kupumzika kisha baada ya hapo nitafanya uamuzi wa kujua hatima yangu, siwezi kusema sitafanya kazi tena Tanzania au sehemu nyingine, kwa sababu ninachoangalia ni mradi mzuri na mustakabali wangu kijumla," alisema.
Hii ni mara ya tatu kwa Maximo kuja Tanzania kufundisha soka, baada ya awali kuifundisha Taifa Stars kuanzia mwaka 2006 hadi 2010 na kuweka historia ya kuwa kocha wa kwanza kuipeleka fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizofanyika Ivory Coast mwaka 2009. Adios Maximo!
NAMBA AKIWA KMC
Mechi 9
Kushinda 1
Kupoteza 7
Droo 1
Mabao ya kufunga 14
Mabao ya kufungwa 2
MATOKEO
KMC 1-0 Dodoma Jiji
KMC 0-1 Singida BS
TZ Prisons 1-0 KMC
KMC 0-3 Mbeya City
Fountain 1-0 KMC
Yanga 4-1 KMC
KMC 0-1 JKT TZ
KMC 0-0 Mtibwa Sugar
Pamba 3-0 KMC
NAMBA AKIWA YANGA
Mechi 7
Kushinda 4
Kupoteza 2
Droo 1
Mabao ya kufunga 9
Mabao ya kufungwa 5
MATOKEO
Mtibwa 2-0 Yanga
Yanga 2-1 TZ Prisons
Yanga 2-1 JKT TZ
Yanga 0-0 Simba
Stand Utd 0-3 Yanga
Kagera Sugar 1-0 Yanga
Yanga 2-0 Mgambo