Prime
Kwa Yanga hili wala sio la kwanza

Muktasari:
- Pia wakasema endapo Bodi ya Ligi na TFF watawakata pointi 15 kama kanuni zinavyotaka, basi watasusia ligi kwa michezo iliyobaki.
ALHAMISI iliyopita, Juni 5, waliojitambulisha kama wazee wa Yanga, walijitokeza na kusisitiza timu yao haitocheza mechi ya Juni 15 dhidi ya Simba hadi baadhi ya viongozi wa Bodi ya Ligi Kuu Bara na TFF wajiuzulu.
Pia wakasema endapo Bodi ya Ligi na TFF watawakata pointi 15 kama kanuni zinavyotaka, basi watasusia ligi kwa michezo iliyobaki.
Hiki kinachoendelea sasa kati ya Yanga na mamlaka za soka, Bodi ya Ligi na TFF, siyo kitu kipya hata kidogo.
Hata hivyo, jana Jumatatu kimeitishwa kikao cha pamoja baina ya pande hizo mbili kwa nia ya kujadili pambano hilo la Ligi Kuu lililoshindwa kupigwa Machi 8, mwaka huu, ili kufanya maandalizi kabla ya Jumapili kupigwa pale Kwa Mkapa. Kilichoamuliwa huko, huenda utakuwa umeshakisikia.
Kadhalika hii siyo mara ya kwanza kwa Yanga na mamlaka za soka kuzozana,
Historia inaonyesha klabu hiyo imewahi kuingia katika migogoro kadhaa na mamlaka za soka hapa nchini na mara zote waliishia kushindwa.
Makala haya yanakuletea matukio kama haya yaliyowahi kutokea huko nyuma na hatua zilizochukuliwa baada ya hapo.
MKASA WA 1965
Yanga na Simba (wakati ile bado ikiwa Sunderland) zilipangwa kukutana Juni 7, 1965 kwenye Uwanja wa Ilala (sasa Karume).
Siku ikafika na zote zikaja uwanjani, lakini Yanga ikagoma kucheza ikipinga uwepo wa mchezaji mmoja wa Sunderland.
FAT ikasema huyo mchezaji hakuwa na tatizo la kumfanya asicheze.
Yanga baada ya kushindwa hoja hiyo, ikaja na hoja nyingine ya kumkataa mwamuzi.
Rais wa FAT, Balozi J. Maggid, akamteua kocha wa timu ya taifa, Milan Celebic, achezeshe mechi hiyo. Yanga ikakubali kuingia uwanjani, lakini Sunderland nayo ikagoma ikitaka wachezaji wawili wa Yanga wasichezea kwa sababu walifungiwa.
Mwenyekiti wa Ligi (Bodi ya Ligi), Abdu Hussein, akasema wao kama waendeshaji wa ligi, hawajawafungia wachezaji hao. Mzozo ukaisha na timu zote zikaingia uwanjani. Dakika ya 15 Yanga ikapata bao lililofungwa na Mawazo Shomvi.
Hata hivyo, mchezo ukashindwa kumalizika kwa muda sahihi kutokana na giza kwa sababu ulichelewa kuanza kwake kwa mizozo iliyojitokeza mapema kabla ya timu hizo kuingia uwanjani.
Mwamuzi akauvunja, FAT ikapanga mchezo urudiwe lakini Yanga ikagoma na kujitoa katika ligi. Sunderland ikapewa ushindi na ligi ikaendelea...mwisho wa msimu Sunderland ikawa bingwa.
MKASA 1966
Yanga na Sunderland zilikutana Novemba 5, 1966 kwenye Uwanja wa Ilala (Karume) katika mchezo wa raundi ya pili wa Ligi ya Taifa (sasa Ligi Kuu Bara). Yanga ikiongoza 2-0, mchezaji wao mmoja akatolewa baada ya kufanya madhambi hatarishi.
Wakati huo kadi nyekundu zilikuwa hazijaanza kutumika duniani...mchezaji akifanya madhambi mabaya, mwamuzi anamtoa tu kwa kumwonyesha aelekee nje.
Viongozi wa Yanga wakagoma mchezaji wao kutolewa...wakavunja mechi.
FAT ikapanga mechi irudiwe, yule mchezaji afungiwe mechi tatu na nahodha wa Yanga afungiwe mwaka mzima kwa kuhamasisha kuvunjika kwa mechi.
Zaidi ya hapo, Yanga ikaamuliwa inyimwe mgao wao wa mapato ya mlangoni ya mchezo huo.
Hiki kilikuwa kisu kikali sana kwa Yanga kwani mapato ya mlangoni ndiyo yalikuwa chanzo pekee cha mapato kipindi hicho.
Wakakataa kucheza mechi ya marudio, FAT ikawapa Sunderland ushindi wa mezani na Yanga ikajitoa katika ligi. Ligi ikaendelea na Sunderland ikawa bingwa.

MKASA WA 1967
Ligi ya mwaka 1967 ilitakiwa itoe mwakilishi wa kwanza wa Tanzania katika mashindano mapya wa klabu bingwa Afrika. Mwaka huo FAT ilipanga ligi ichezwe kikanda na iligawa nchi katika kanda sita.
Lengo lilikuwa mabingwa wa kila kanda waje Dar es Salaam kutafuta bingwa wa Taifa. Lakini bahati, kanda zenyewe hazikuwa na uwezo wa kuandaa mashindano makubwa kama hayo.
Ligi ikachelewa kuanza na kuonyesha dalili ya kuchelewa kuisha. Ili kuwahi tarehe ya mwisho ya CAF ya kupokea majina ya wawakilishi, FAT iliamua kuachana na ligi ile ya kanda na kuanzisha ligi nyingine ya haraka haraka.
Sunderland na Yanga zikaigomea ligi hii.
Sunderland ikasema haitocheza na inataka itambuliwe kama mabingwa kwa sababu ilishinda ubingwa msimu uliopita hivyo jina lao lipelekwe CAF.
Yanga ilikataa kucheza ligi hii kwa sababu wachezaji wao wengi walisafiri na timu ya Taifa kwenda Kinshasa Zaire (sasa DRC) kwa mechi ya kufuzu AFCON, na baada ya hapo itaenda Nairobi Kenya kwa Kombe la Gossage (baadaye CECAFA Senior Challenge Cup).
FAT ikaachana na Sunderland na Yanga...ikaendesha ligi yao na Cosmopolitan kuwa bingwa.

MKASA WA 2003
Kuanzia 1982 hadi 2003 kulikuwa na mashindano yaliyoitwa Ligi Kuu ya Muungano (sasa Kombe la Muungano).
Hii ndiyo ilikuwa ligi kuu ya Tanzania na ndiyo iliyotoa wawakilishi wa taifa katika mashindano ya kimataifa ya Afrika kwa ngazi za klabu.
Bingwa alishiriki Klabu Bingwa Afrika ambayo kuanzia 1997 ikawa Ligi ya Mabingwa Afrika na mshindi wa pili alishiriki Kombe la CAF.
Tanzania Bara na Zanzibar kulikuwa na ligi zao.
Timu kadhaa za juu (kulingana na mwaka) ndizo zilifuzu kushiriki Ligi Kuu ya Muungano. Mwaka 1982 zilifuzu timu mbili kutoka kila upande...na baadaye zikaongezeka na kuwa tatu tatu. Mwaka 2003 ligi ya Bara ilichelewa kumalizika hivyo kusababisha Ligi ya Muungano kuchelewa kuanza.
Kwa kawaida ligi za Bara na Zanzibar ziliisha Agosti au Septemba mwanzoni.
Na Septemba katikati au mwishoni Ligi Kuu ya Muungano ilianza na kuisha Novemba.
Lakini mwaka huo, hadi Novemba Ligi ya Bara ilikuwa haijaisha...iliisha Novemba 26. CAF ilipanga mwisho wa kupokea majina ya wawakilishi ni Desemba 24, 2003. Kwa hiyo Ligi Kuu ya muungano ingechezwa kama kawaida kwa nyumbani na ugenini, ingechelewa kuisha na Tanzania kushindwa kuiwahi tarehe ya mwisho ya CAF.
Hivyo Chama cha Soka cha Tanzania (FAT, sasa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF) na kile cha Zanzibar, ZFA (sasa Shirikisho la Sokla Zanzibar, ZFF), kama waandaaji wa Ligi Kuu ya Muungano, wakakubaliana kuongeza timu moja kila upande ili ziwe nne nne na kufanya jumla ya timu nane. Timu hizi zicheze kwa mtoano badala ya nyumbani na ugenini.
Yanga ilikuwa ya nne Bara hivyo ikapata nafasi hiyo ya bahati na kwa Zanzibar nafasi ikachukuliwa na Ujamaa. Yanga ikapangwa kucheza na Jamhuri ya Pemba, Desemba 10...na wakatoka Dar es Salaam hadi Unguja ili waende Pemba. Kufika Unguja, ikagoma kwenda Pemba, ikisema imegundua hakuna Ligi ya Mtoano duniani...inataka icheze Ligi ya nyumbani na ugenini.
Ikaambiwa ligi za mtoano zipo na hata hiyo Ligi Kuu ya Muungano ilichezwa hivyo mwaka 1992 na fainali kuwa Yanga na Simba kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar...Yanga ikafungwa 1-0 kwa bao la tiktak la Damian Kimti. Lakini Yanga ikagoma kwenda Pemba.
FAT ambayo ilikuwa chini ya Kamati ya Muda iliyoongozwa na Mwina Kaduguda kama Katibu Mkuu na Yahya Mhata kama Mwenyekiti, ikaamua kuiondoa Yanga na kuipa ushindi wa mezani Jamhuri.
Yanga ikapinga na kwenda kufungua kesi mahakamani kuzuia ligi.
Mahakama ikasimamisha ligi hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa...na ikapanga kusikiliza kesi hiyo Februari 2004.
FAT na ZFA zikatii amri ya mahakama na kusimamisha ligi.
Lakini zikateua mabingwa wa kila upande kushiriki mashindano ya Afrika.
Simba kama bingwa wa Bara ikapewa nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa na Mlandege kama Mabingwa wa Zanzibar ikapewa nafasi ya kushiriki mashindano mapya ya Kombe la Shirikisho (iliyozaliwa kwa kuunganishwa kwa Kombe la CAF na lile la Kombe la Washindi Afrika).
Lakini Mlandege ikasema haina uwezo wa kifedha wa kushiriki mashindano ya Afrika. ZFA ikaiteua Mtibwa Sugar kuchukua nafasi ya Mlandege...na ndipo Mtibwa Sugar ikaitwa mtoto wa kambo wa Zanzibar.
MKASA WA 2013
Mwaka 2013 kampuni mpya ya runinga, Azam Media Ltd, ilisaini mkataba na Kamati ya ligi (mwanzilishi wa Bodi ya Ligi) kwa ajili ya kuonyesha Ligi Kuu. Yanga iliupinga mkataba huu kwa nguvu zote.
Mechi yao ya kwanza kuonyeshwa ilikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar, Oktoba 6, 2013 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Mkapa).
Viongozi wa Yanga walikataa mechi hii kuonyeshwa kiasi cha kuita mashabiki majukwaani wavunje kamera za Azam TV. Azam TV wakaondoa kamera zao kuepusha shari.
Taarifa zikafika polisi, Kamanda Suleiman Kova wakati ule akiwa kamanda wa polisi Dar es Salaam, akatuma kikosi kuja kulinda kamera.
Mechi ikaanza kuonyeshwa kipindi cha pili.
Hata hivyo, Yanga haikuishia hapo, iliendelea kuipinga Azam TV kiasi cha kufungua kesi mahakama ya ushindani wa kibiashara.
Baada ya kupinga kwa miaka mingi, hatimaye mwaka 2017 ikaenda kuifuta kesi na maisha yakaendelea.

MKASA WA MORRISON
Yanga ilimsaini Bernard Morrison kama mchezaji huru, Januari 2020 na kumpa mkataba wa miezi sita. Baadaye ikatoa taarifa Morrison amesaini mkataba mpya wa miaka miwili. Lakini mwezi wa saba, Morrison akatimkia Simba.
Yanga ikasema imedhulumiwa na Simba...kesi ikaenda TFF, ikashindwa.
Haikuridhika, ikaenda CAS, ikashindwa...ikaishia kumtambulisha kwenye siku ya mwananchi...lakini ikamkosa.

MKASA WA FEI TOTO
Desemba 22, 2022 nyota wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto' aliwasilisha barua ya kuununua mkataba wake na klabu hiyo ili awe huru.
Mkataba wake ulikuwa na kipengele kilichosema akitaka kuununua mkataba wake ili awe huru, basi alipe pesa aliyopewa siku anasaini mkataba pamoja na mshahara wa miezi mitatu.
Siku anasaini mkataba alipewa Sh100 milioni.
Na mshahara wake wa mwezi ulikuwa Sh4 milioni...kwa miezi mitatu ni Sh12 milioni. Hivyo, akailipa Yanga Sh112 milioni, lakini Yanga ikakataa kupokea pesa hiyo.
Wazee wa Yanga wakajitokeza na kusema wanajua nani yuko nyuma ya sakata la mchezaji wao, hivyo watasusia bidhaa zake endapo atamchukua. Lakini mwishowe Feisal hakubaki Yanga...akaondoka. Kwa hiyo hata haya ya sasa, mwishowe Yanga itashindwa na maisha yataendelea.
Yanga haitoshinda!