Prime
Kutumia video kuadhibu waamuzi ni uvivu
KATI ya mambo tunayotarajia kupokea wiki hii ni maamuzi dhidi ya marefa wawili na wasaidizi wao waliohusika katika mechi mbili zilizohusisha wababe wa Kariakoo katika Ligi Kuu Bara.
Umma unatarajia kuona yale mambo ya kawaida yatakayotolewa kwenye taarifa ya Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi (Kamati ya Saa 72), itakayojumuisha maneno “kwa kushindwa kutafsiri sheria” wakati wajumbe wa chombo hicho watakapojiridhisha uamuzi uliofanywa na marefa na wasaidizi wao kuhusu matukio kadhaa kwa kuangalia picha za marudio za mechi hizo.
Hakuna ambaye hatarajii kuwa waamuzi hao watapona mkono wa kamati hiyo. Ni kwamba watafungiwa mechi kuanzia tatu ambazo sasa zimekuwa kama mapumziko ya kawaida kwa waamuzi wetu maana nao wanachoka kusafiri umbali mrefu kila mwishoni mwa wiki kufuata mechi za Ligi Kuu.
Kwa wale watukutu wangediriki hata kukosea baadhi ya uamuzi muhimu ili wapate mapumziko hayo yanayoitwa ni adhabu kwa “kushindwa kutafsiri sheria za soka".
Watakaoadhibu watapata wasaa mwingi wa kurudia kuangalia matukio hayo na wakati mwingine kubishana kidogo kabla ya kufikia uamuzi kuwa refa ama alikosea au alikuwa sahihi kuchukua uamuzi fulani pale uwanjani.
Na baadaye watachora hata mistari bila ya kuwa na teknolojia sahihi kabla ya kuamua kuwa mwamuzi msaidizi alikosea kunyoosha au kutonyoosha kibendera cha kuotea.
Ndiyo utamaduni tuliojijengea wa kuwaadhibu waamuzi ambao hatujawawezesha kutumia teknolojia, ila sisi tunatumia teknolojia kufanya uamuzi dhidi yao na kuwaadhibu.
Mchezo wa mpira wa miguu umebadilika sana na kasi ya sasa si kama ile iliyokuwepo enzi za kina Edson Arantes de Naschimento au Pele, au enzi za kina Sunday Manara na Abdallah Kibaden. Ni kasi kubwa hasa katika eneo la mwisho ambalo makocha wametengeneza mbinu nyingi kujilinda na wakatengeneza mbinu nyingi kupenya ukuta.
Ukimwangalia mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa adhabu iliyoelekezwa langoni mwa Simba katika mechi dhidi ya Azam utamuona amesimama sambamba na ukuta wa Simba kabla ya Himid Mao kupiga mpira. Baada ya kiungo huyo kupiga shuti moja kwa moja golini na kipa kuutema, unamwona mwamuzi huyo msaidizi akikimbia kwa kasi kuelekea kwenye kibendera kuhakikisha kama mpira uliotemwa umevuka mstari.
Akiwa amebakiza hatua kama sita kufika mwisho wa mstari, unamuona akinyoosha kibendera kuonyesha kuwa mpira ulishatoka kabla ya kipa wa Simba kuunyaka tena. Ni kweli mpira ulishatoka na hata kipa wa Simba hakumbishia, lakini mwamuzi msaidizi aliwezaje kuhakikisha mpira ulivuka mstari wakati alikuwa hajafika katika kibendera?
Ni kweli kasi ya shuti la Mao isingeweza kwenda sambamba na kasi ya mwamuzi msaidizi, lakini hivyo ndivyo ilivyo kwa matukio mengine mengi yanayoweza kusababisha mwamuzi msaidizi akakimbia mbele, kurudi nyuma, kukimbia mbele na kurudi tena nyuma wakati timu ikijaribu kupenya ngome ya wapinzani na hivyo kusababisha asiweze kufanya uamuzi sahihi.
Ndiyo maana wasimamizi wa mpira duniani bado wanafanya kila liwezekanalo kubuni teknolojia itakayomsaidia zaidi mwamuzi wa kati kupata taarifa nyingi kabla ya kufanya uamuzi.
Waamuzi huongozwa na mambo mengi wakati wa kuchukua uamuzi, tofauti na watu waliokaa mezani, studio au mbele ya kompyuta na simu kumkosoa mtaalamu wa sheria za mpira anapokuwa uwanjani.
Wataalamu wanasema refa huzingatia sheria tofauti za soka, ari ya mchezo (jinsi mpira unavyotembea na haki) pamoja na mtazamo wao wa pale uwanjani wakati wanapofanya uamuzi wa tukio fulani.
Kwa tukio kama la wachezaji kugusana ndani ya eneo la penalti, refa huangalia asili ya tukio hilo kama kizembe (careless) au kutojali (reckless). Mara nyingi la kizembe ni lile dogo ambalo mchezaji kalifanya bila kuwa na nia mbaya na kwa tukio hili refa huwa hatoi penalti. Lakini tukio la kutojali ni lile ambalo mchezaji hulifanya bila kuangalia athari au hatari zake kwa mchezaji mwingine. Na hapa ni lazima refa atoe penalti.
Pia mwamuzi huangalia kama mchezaji ametumia nguvu kubwa (excessive force) na hapa ni lazima refa atoe penalti. Hili ni jambo ambalo mwamuzi pekee ndiye anaweza kulipima. Mambo mengine ni kama kitendo cha beki kuzuia mshambuliaji kutopata nafasi ya kufunga au kuharibu shambulio ambalo lingeweza kuzaa bao na kama beki aliugusa mpira kwanza kabla ya kumgusa adui, ingawa kugusa mpira kwanza hakuhalalishi rafu.
Sasa iweje watu waliokaa mezani na kuangalia marudio ya picha za video waone hiyo nia ya mchezaji? Iweje maoni ya refa pale uwanjani kuwa kulikuwa na dhamira ya kucheza vibaya au haikuwepo yaonekane kuwa ni tafsiri mbaya ya sheria? Hayo ni mambo machache tu ambayo mwamuzi hutumia sekunde chache kuyaweka pamoja kabla ya kupuliza filimbi na kuamua iwe adhabu.
Hata Ulaya ambako teknolojia ya televisheni na picha za marudio ilianza muda mrefu, bado hawakuthubutu kuadhibu waamuzi kwa kutumia teknolojia hiyo. Badala yake walikuna vichwa kutafuta njia gani za kuwawezesha wasimamizi wa haki uwanjani kufanya uamuzi sahihi.
Kuna mambo mengi walifanya, ikiwa ni pamoja na kutumia waamuzi watano yaani mmoja wa kati na wanne wasaidizi ili kufanya uamuzi sahihi katika mistari ya pembeni na kwenye magoli yote. Wameanzisha pia teknolojia ya mistari ya goli (goalline technology) ambayo inatoa jibu kama mpira umevuka mstari au haujavuka ndani ya sekunde nane.
Mbali na teknolojia ya Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R), ambayo huangalia zaidi matukio yanayotokea wakati wa kuelekea kufunga bao, pia wameanzisha mpira janja (smart ball) ambao hubaini mchezaji aliyeotea na sasa wanaenda kujaribu kwenye Ligi Kuu Canada tafsiri ya kuotea iliyopendekezwa na kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger kuwa ili mchezaji awe ameotea mwili wake wote uwe umempita mchezaji wa mwisho wa timu pinzani.
Hawa wanaelewa refa ni binadamu kama wengine na kuna makosa anayoweza kufanya bila kuwa na nia ovu wala uzembe na hivyo kumsaidia ni kumtafutia teknolojia itakayomuwezesha kufanya uamuzi sahihi na hivyo ile kanuni kuu ya mpira wa miguu kuwa maoni ya refa ndiyo yatatamalaki iweze kufanya kazi vizuri.
Bado hatujawa na teknolojia inayoweza kutupa taarifa sahihi za kubaini makosa au kasoro za uamuzi wa marefa. V.A.R ni teknolojia maalumu na si kila kamera au kompyuta inaweza kutumiwa kufanya uamuzi muhimu wa mpira na ndiyo maana haitolewi bure. Ni mali ya akili ya watu walioamua kupoteza muda kutafuta suluhisho.
Sasa watu wachache wanapokutana na kutumia picha za video zilizochukuliwa kwa kamera mbili, ni ishara tunatafuta suluhisho rahisi kwa matatizo makubwa. Ni ama tukubali kuingia gharama ili tuwezeshe matumizi ya teknolojia sahihi au tukubali kuingia gharama za kutumia waamuzi wengi zaidi ama tuwekeze katika mkakati wa kuboresha viwango vya waamuzi wetu. Lakini, kutumia picha za marudio zisizokuwa za teknolojia sahihi kuadhibu waamuzi ni uvivu wa kutafuta suluhisho la moja ya nguzo muhimu za soka na kutotenda haki.