Kocha Singida Black Stars aanza na tahadhari
Muktasari:
- Timu hiyo iliondoka juzi baada ya kuweka kambi fupi jijini Dar es Salaam, ikiwa sasa inatafuta rekodi nyingine mpya baada ya kufanya maajabu msimu uliopita kwa kufika hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo.
SINGIDA Black Stars ipo tayari kuandika historia mpya kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika huku kocha mkuu, Papy Kimoto akisisitiza lengo lao ni kuvuka hatua ya kwanza.
Timu hiyo iliondoka juzi baada ya kuweka kambi fupi jijini Dar es Salaam, ikiwa sasa inatafuta rekodi nyingine mpya baada ya kufanya maajabu msimu uliopita kwa kufika hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia ya timu hiyo.
Singida wanatarajia kuanza kampeni yao ya kimataifa kwa mara ya kwanza kesho, watakapokutana na Al-Ghazal FC ya Sudan Kusini, katika mchezo ambao utakuwa mtihani wa kwanza kwa kikosi hicho kwenye mashindano ya Afrika.
Singida Black Stars imeweka wazi dhamira ya kufanya vizuri zaidi msimu huu baada ya msimu uliopita kuishia hatua ya makundi, huku Kimoto ambaye ni mmoja kati ya makocha wakubwa Afrika akieleza maandalizi yamefanyika kwa umakini mkubwa kuhakikisha timu inaingia kwenye mchezo huo ikiwa tayari kupambana kwa dakika zote tisini uwanjani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kimoto alisema benchi lake la ufundi limekuwa likitumia muda uliopo kurekebisha upungufu uliojitokeza kwenye mechi za ligi.
“Tunajiandaa kwa uzito mkubwa sana kwa sababu tunahitaji kwenda hatua ya pili, tuna kikosi bora cha kuweza kufanya hivyo, lakini faida kwetu ni kwamba tayari tumeshaona makosa yetu kwenye michezo ambayo tumecheza msimu huu,” alisema Kimoto akieleza kuwa lengo siyo kushiriki tu, bali kupata matokeo mazuri ili yatakayowaweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Kimoto alisema mbali na hilo bado wana kazi kubwa ya kujenga uimara wa kikosi, hasa katika suala la mwendelezo wa kiwango cha uchezaji.
Kocha huyo ambaye ameiongoza Singida kwenye michezo mitano ya ligi na kushinda mitatu, wametoka sare mmoja na kupoteza mmoja, amekiri kuwa Singida imekuwa ikionyesha viwango vinavyobadilika kutoka mchezo mmoja kwenda mwingine, jambo ambalo analiona kama eneo muhimu la kulifanyia kazi.
“Hatuna mwendelezo mzuri wa uchezaji wakati mwingine tunafanya vizuri sana, wakati mwingine tunafanya vibaya uwanjani, kitu ambacho si kizuri hasa kwenye mashindano ya kimataifa, lazima tfanye kazi kubwa kuhakikisha kuwa tunafanya vizuri kwenye michezo yetu miwili inayokuja, vinginevyo hatutaweza kuvuka hatua hii, kila mmoja anatakiwa kujitoa kwa nguvu kubwa,” alisema.
Huu utakuwa msimu wa pili kwa Singida kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho endapo timu hiyo itafanikiwa kufika hatua ya makundi, basi itakuwa moja ya timu changa ambazo zimefanya vizuri zaidi kwenye michuano ya CAF kwa miaka ya hivi karibuni.
Hata hivyo kuvuka na kwenda hatua ya makundi ni mtihani kwa Singida kutokana na kuwepo kwa timu kubwa nyingi kwenye michuano ya Shirikisho tofauti na hali ilivyokuwa misimu kadhaa nyuma.
Kwa msimu huu vingingi vikubwa kwenye michuano hiyo ni Al Ahly ambayo ni timu bora ya pili Afrika, Al Ahly Tripoli, Jwaneng Galaxy pamoja Raja Casablanca zikiwa ni baadhi ya timu ambazo zimekuwa na uchu mkubwa wa kulihitaji kombe hilo baada ya kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.