Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kizazi kipya gofu chasukwa

Muktasari:

  • Kwa mara ya tatu mfululizo, mashindano hayo hayakuwa tu ya kusaka mabingwa wa vikombe na pointi, bali pia yaligeuka kuwa jukwaa la kuunganisha michezo, biashara, burudani na ukuzaji wa kizazi kipya cha wachezaji wa gofu.

GOFU imepiga hatua nyingine katika kukuza mchezo huo baada ya mashindano ya Vodacom Corporate Masters 2026 yaliyofanyika Septemba 5, 2026 katika viwanja vya TPDF Lugalo Golf Club jijini Dar es Salaam, yakishirikisha takribani wachezaji 150 kutoka Tanzania na nchi jirani.

Kwa mara ya tatu mfululizo, mashindano hayo hayakuwa tu ya kusaka mabingwa wa vikombe na pointi, bali pia yaligeuka kuwa jukwaa la kuunganisha michezo, biashara, burudani na ukuzaji wa kizazi kipya cha wachezaji wa gofu.

Wakati Khalid Shemndolwa na Yvonne Ondari wakitwaa mataji ya jumla kwa wanaume na wanawake baada ya kila mmoja kukusanya pointi 42, jambo lingine lililovuta hisia lilikuwa darasa maalumu la gofu lililowakutanisha watoto, vijana na watu wazima.

Washiriki hao walipata nafasi ya kujifunza misingi ya mchezo huo na kuboresha ujuzi wao chini ya wataalamu wa gofu, Pro Daudi Helela na Pro Iddi Mzaki.

Darasa hilo lililoendeshwa kwa siku nzima, lilifanya Corporate Masters kuwa zaidi ya mashindano ya siku moja, likiwa daraja linalounganisha gofu ya sasa na kizazi kinachotarajiwa kuingia uwanjani miaka ijayo.

Mratibu wa mashindano hayo, Kelly Simon alisema falsafa ya Corporate Masters si kutafuta washindi pekee, bali pia kushiriki katika kujenga msingi wa maendeleo ya mchezo huo.

“Mbali ya kupata washindi kwa wachezaji kushindana, pia tunaangalia maendeleo ya mchezo kwa ujumla. Ni wazi kuwa hata michezo mingine ina malengo ya kuzalisha wachezaji kwa ajili ya maendeleo. Sisi katika gofu tumekwenda mbali zaidi kwa kufikiria vijana na watu wazima pia,”  alisema Simon.

Alisema kinachofanya gofu kuwa mchezo wa kipekee ni uwezo wake wa kuwaunganisha watu wa rika tofauti, huku umri ukiwa si kikwazo cha ushindani. “Gofu ni tofauti na michezo mingine kwa sababu hata wazee wanaweza kushindana na vijana na kushinda. Hivyo, umri kwetu si kikwazo. Ndiyo maana mafundisho haya yamekuwa kwa watu wa rika tofauti na tunafurahi kwa mwitikio mkubwa,”€  alisema. Kwa mtazamo huo, mtoto aliyeshikiriki kwa mara ya kwanza katika tukio hilo anaweza kuwa mchezaji wa mashindano makubwa siku zijazo.

Kijana aliyepata nafasi ya kufundishwa misingi ya mchezo anaweza kuwa sehemu ya timu ya taifa baadaye, huku mtu mzima aliyeanza kujifunza gofu akawa balozi wa mchezo huo katika familia, kampuni au jamii yake. Ndiyo maana darasa hilo halikuwa shughuli ya pembeni, bali lilikuwa sehemu ya uwekezaji katika mustakabali wa gofu.


SHEMNDOLWA, ONDARI WATAWALA

Katika uwanja wa ushindani, Shemndolwa na Ondari walionyesha makali yao na kumaliza siku wakiwa mabingwa wa jumla wa mashindano hayo. Wote walikusanya pointi 42 katika mashimo 18, wakionyesha ushindani mkubwa katika toleo hilo la tatu la Corporate

Katika Division A kwa wanaume, Godfrey Abel alitwaa ubingwa baada ya kukusanya pointi 42, akifuatiwa na Likuli Juma aliyepata pointi 41. Division B nayo ilitoa ushindani wa karibu, ambapo Sigfrid Urassa alitwaa taji kwa pointi 40, sawa na Godfrey Kilenga, lakini Urassa akaibuka mshindi kwa kanuni ya countback.

Boniface Japhet alikuwa kinara wa Division C baada ya kukusanya pointi 39, huku Abdallah Singano akimaliza nafasi ya pili kwa pointi 37.

Kwa upande wa wanawake, Neema Job alitwaa taji kwa pointi 42, akifuatiwa na Leticia Kapalia aliyepata pointi 40.

Katika mashindano ya timu za kampuni, KQ iliibuka mshindi baada ya kushindana na timu nyingine tisa.

Katika tuzo maalumu, Michael Norbert alitwaa Longest Drive kwa wanaume, huku Kapalia akishinda kipengele hicho kwa wanawake.

Harshid Barmeda alitwaa tuzo ya Nearest to the Pin kwa wanaume, wakati Vaileth James akishinda tuzo hiyo kwa wanawake.

GOFU, BIASHARA, FAMILIA ZAKUTANA

Corporate Masters 2026 haikuwa suala la klabu na mipira pekee. Kulikuwa na eneo la Corporate Village lililobadilisha mandhari ya mashindano hayo na kuwa sehemu ya kukutana kwa wafanyabiashara, viongozi wa kampuni, wachezaji na familia zao.

Kulikuwa na burudani, maonesho ya biashara na eneo maalumu la watoto, huku washiriki wakipata nafasi ya kujenga mahusiano mapya nje ya mazingira yao ya kawaida ya kikazi.

Kwa kufanya hivyo, gofu ilitumika kama daraja la kuunganisha michezo na biashara.

Mkurugenzi wa Vodacom Business wa Vodacom Tanzania, Nguvu Kamando, alisema mashindano hayo yameonyesha namna michezo inavyoweza kuwa chombo cha kujenga mahusiano ya kibiashara na kijamii.

“Vodacom Corporate Masters 2026 imeonyesha tena kwamba michezo ni jukwaa lenye nguvu la kujenga mahusiano ya kudumu ya kibiashara. Tumefurahishwa na ushiriki mkubwa wa makampuni na kasi ya mahusiano mapya yaliyoundwa,”€  alisema Kamando.

Alisema kwa Vodacom Business, ushiriki huo ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo kuwa mshirika wa biashara zinazokua ndani ya uchumi wa kidijitali wa Tanzania.

“Kwa Vodacom Business, hii ni sehemu ya dhamira yetu ya kubaki mshirika wa kuaminika katika ukuaji wa biashara kwa taasisi zinazokua ndani ya uchumi wa kidijitali wa Tanzania,”  alisema.

Katika kipindi cha mash indano, Vodacom Business pia ilitumia jukwaa hilo kuwaonyesha wateja wake suluhisho mbalimbali za mawasiliano na huduma za kidijitali zinazolenga kukidhi mahitaji ya kampuni na taasisi.


ZAIDI YA KOMBE

Mwenyekiti wa Kamati ya Corporate Masters, Ken Kariuki, alisema ushiriki wa kampuni mbalimbali umeifanya michuano hiyo kuwa zaidi ya tukio la michezo.

“Mwaka huu tumeshuhudia ushindani wa kiwango cha juu uwanjani na ushiriki wenye maana nje ya uwanja. Huo ndio msingi wa Corporate Masters, kuzikutanisha kampuni katika mazingira rafiki yanayoweza kuzalisha fursa halisi za ushirikiano,† alisema Kariuki.

Kauli hiyo inaonyesha picha kubwa ya Corporate Masters, kwani mashindano hayo hayaangalii tu nani amepiga vizuri zaidi, amekusanya pointi nyingi au amebeba kombe.

Pia yanalenga kutumia nguvu ya gofu kujenga mahusiano, kuvutia washiriki wapya na kuufanya mchezo huo ufikie watu wengi zaidi.