NCBA yafungua milango ya fursa Arusha
Muktasari:
- Hiyo imejitokeza kupitia mfululizo wa NCBA Golf Series 2026, uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Kili Golf ambapo wachezaji, viongozi wa biashara, wateja na wadau mbalimbali walikutana katika mashindano yaliyokuwa na sura zaidi ya ushindani wa kawaida.
MASHINDANO ya Gofu huko Arusha yameendelea kushika kasi huku safari hii si kwa ajili ya kutafuta mshindi pekee, bali yakitumika kama daraja la kuunganisha michezo, elimu na fursa kwa vijana katika jamii.
Hiyo imejitokeza kupitia mfululizo wa NCBA Golf Series 2026, uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Kili Golf ambapo wachezaji, viongozi wa biashara, wateja na wadau mbalimbali walikutana katika mashindano yaliyokuwa na sura zaidi ya ushindani wa kawaida.
Mashindano hayo yalifanyika kwa ushirikiano na Diplomatic Golf Tournament, mpango unaolenga kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia kulipia ada za shule kwa wanafunzi wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini huku mshindi wa jumla akipata fursa ya kudhaminiwa kushiriki NCBA Golf Series.
Kwa hiyo, wakati wachezaji wakisaka ubora wao kwenye mashimo ya Kili Golf, kulikuwa na jambo jingine likiendelea nyuma ya mashindano hayo kutumia mchezo huo kusaidia kufungua milango kwa wanafunzi na pia kuwapa wachezaji nafasi ya kusukuma mbele vipaji vyao.
Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA Bank Tanzania, Alex Mziray, amesema matumizi ya gofu katika shughuli hizo yanaendana na falsafa ya benki hiyo ya ‘Banking on Belief Empowering Ambition’, akisisitiza kuwa mchezo huo unaweza kuunganisha watu na kuzalisha matokeo yanayovuka uwanja.
“Gofu inatupa nafasi ya kuungana na wateja na washirika wetu, lakini zaidi ya hapo, inatupa fursa ya kuleta matokeo yanayoenda mbali zaidi,” amesema Mziray.
Mashindano ya Arusha ni sehemu ya NCBA Golf Series 2026 na yanafuatia awamu iliyofanyika Dar es Salaam Gymkhana huku mfululizo huo ukiendelea katika masoko mbalimbali ambako NCBA Group inaendesha shughuli zake.
Kwa Tanzania, mfululizo huo unatarajiwa kuhitimishwa Dar es Salaam huku wachezaji watakaofuzu wakipewa nafasi ya kushiriki NCBA Group Grand Finale jijini Nairobi mwishoni mwa Novemba, jambo linaloongeza ushindani na thamani ya mashindano hayo.
Lakini Arusha haikuishia kwenye gofu. Siku iliyofuata, NCBA ilihamia Shule ya Msingi Kijenge ambako ilishiriki zoezi la upandaji miti, sehemu ya mpango wa kupanda na kutunza miti 20,000 ifikapo Desemba 2026 katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Dar es Salaam na Zanzibar.
Zoezi hilo lililofanyika kwa ushirikiano na TEEMO pamoja na wadau mbalimbali liliwashirikisha wanafunzi ambao walihamasishwa kutunza miti hiyo na kuwa mabalozi wa mazingira katika shule, familia na jamii zao, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya badilisha simulizi.