Prime
Kimemkuta nini Ahoua?
JEAN Charles Ahoua ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa na mwaka wa kuvutia zaidi kwa Simba msimu uliopita (2024/25), akimaliza akiwa mfungaji bora wa timu kwa kupachika mabao 17 katika mashindano yote.
Mafanikio hayo yalionyesha uwezo wake mkubwa wa kufumania nyavu, kutoa asisti za mabao kwa wenzake, kupiga frii-kiki kali, kupiga penalti nzuri na harakati zake uwanjani akitumia nafasi chache kwa ufanisi. Hata hivyo, msimu huu hali imebadilika kwa kiasi kikubwa, ambapo Ahoua hana nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza, jambo linalozua maswali mengi kwa mashabiki na wachambuzi wa soka.
Swali linabaki: Je, huu ni mwisho au ni kipindi cha mpito kwa Ahoua? Hali hii si ishara ya kushuka kwa kiwango, bali ni sehemu ya mzunguko wa kawaida wa soka la ushindani. Historia inaonyesha kuwa wachezaji wengi wakubwa wanapitia vipindi kama hivi kabla ya kurejea kwa nguvu zaidi, japokuwa si wote hupitia nyakati hizo baada ya mafanikio.
Anayoyapitia Ahoua, ambaye hadi sasa hajahusika kwenye bao hata moja kati ya mabao 11 yaliyofungwa na Simba katika mechi tano walizocheza katika Ligi Kuu (huku wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu), yamewahi kuwakumba nyota wengi ambao baadaye walirejea kwenye mstari.
Mwanaspoti linakuletea uchambuzi kumhusu mchezaji huyo ambaye, licha ya kuwa na msimu bora uliopita, msimu huu ameanza kwa kusuasua kutokana na sababu tano zinazomuondoa kwenye ushindani.
USHINDANI
Ahoua alikuwa chaguo la kwanza chini ya kocha Fadlu Davids, ambaye tayari ametimka ndani ya kikosi hicho. Tangu kuondoka kwake, mambo yamekuwa magumu kwa mchezaji huyo ambaye kwa sasa anapambania nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Sababu mojawapo kubwa ni ongezeko la ushindani ndani ya kikosi cha Simba. Msimu huu timu imeimarishwa kwa kusajili washambuliaji na viungo wa ushambuliaji wenye uwezo mkubwa, hali iliyosababisha kocha kuwa na machaguo mengi zaidi.
Licha ya kiungo huyo kuonyesha ubora msimu uliopita, amepoteza namba mbele ya Morice Abraham, ambaye ni ingizo jipya ndani ya kikosi cha Simba. Wawili hao wamekuwa wakigawana mechi, mmoja akianza na mwingine akitokea benchini.
MABADILIKO YA MBINU/MFUMO
Tofauti na msimu uliopita, Simba msimu huu inaonekana kubadilisha mfumo wa uchezaji, ikiweka mkazo zaidi kwenye kasi, presha ya juu na ushiriki wa washambuliaji katika kujilinda.
Mabadiliko hayo yamekuwa yakimuondoa kiungo huyo mshambuliaji kwenye kikosi cha kwanza, hali iliyomfanya kujikuta akikalia benchi katika baadhi ya mechi, licha ya kuonyesha ubora msimu wake wa kwanza ndani ya Simba.
Ukiondoa hilo, mbinu tofauti za makocha waliopita Simba katika kipindi cha hivi karibuni, mchezaji huyo akiwa kikosini, zimekuwa sababu ya kuanzia benchini na kushindwa kuendana na kasi ya timu, ambayo imecheza mechi tano, ikishinda nne na kupoteza moja.
Ahoua, ambaye nguvu yake kubwa iko kwenye kumalizia mashambulizi, anaweza kuwa hajalingana kikamilifu na mahitaji mapya ya kiufundi na kimkakati, hasa kwa kocha anayehitaji mshambuliaji anayekimbia sana, anayerudi nyuma kusaidia ulinzi na kubadilisha nafasi mara kwa mara.
Pia, kiungo huyo mshambuliaji ambaye alizoea kucheza nafasi ya kiungo mshambuliaji (namba 10), msimu huu ameonekana kubadilishiwa majukumu na hata kupangwa katika nafasi tofauti, ikiwemo kiungo namba nane.
KUJIAMINI KWA REKODI
Huenda Ahoua ameanza msimu kwa kujiamini kutokana na rekodi nzuri aliyokuwa nayo msimu uliopita, akiamini mambo yangekuwa yaleyale, lakini hali imekuwa tofauti kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara kama ilivyokuwa msimu uliopita alipokuwa ni chaguo la kwanza.
Msimu huu Ahoua amekuwa akipata dakika chache, hali inayoweza kuathiri makali yake mbele ya lango. Mfungaji yeyote anapokosa muda wa kucheza, hata uwezo wake wa kisaikolojia hupungua, na kufanya kila nafasi mpe mzigo mkubwa wa kuthibitisha, jambo linaloongeza presha badala ya kumsaidia.
Ahoua huenda pia anapozwa na rekodi nzuri ya msimu uliopita, akiamini ataendelea pale alipoishia. Hata hivyo, hadi sasa katika mechi tano ambazo timu imecheza, hajapata nafasi ya kufunga wala kutengeneza bao.
MATARAJIO MAKUBWA
Hii ni mojawapo ya changamoto kubwa zaidi kwa Ahoua. Baada ya kuwa na msimu bora ndani ya Simba mara baada ya kujiunga na timu, msimu huu amejikuta akitaka kuthibitisha ubora huo huku akikumbana na changamoto mpya.
Badala ya kuingia uwanjani akiwa huru kiakili, mchezaji anaingia na mzigo wa kujihukumu mwenyewe, akiamini kuwa kila mechi ni mtihani wa kuthibitisha kuwa bado anastahili heshima, sifa na nafasi yake.
Baada ya kufunga mabao 17, matarajio kwa Ahoua yaliongezeka maradufu. Aliamini kuwa ndiye mchezaji mkubwa na tegemeo la timu. Hata hivyo, mzigo wa matarajio unamfanya kucheza kwa presha zaidi, tofauti na msimu uliopita ambapo alikuwa na uhuru mkubwa wa kucheza bila lawama nyingi.
Pia, kiungo huyo anapitia wakati mgumu kutokana na presha kutoka kwa mashabiki wanaoanza kumlinganisha na msimu wake wa kwanza. Hofu ya kupoteza namba, ushindani ulioongezeka kwenye nafasi yake, pamoja na presha ya kucheza, humfanya awe na haraka ya kutaka kufunga au kulazimisha pasi zisizo sahihi akitafuta kutengeneza au kufunga bao.
MECHI KUBWA KUMKATAA
Ahoua alipojiunga na Simba, alionekana kama kiungo mshambuliaji mwenye uwezo wa kutoa mchango mkubwa katika nyakati muhimu, hasa kutokana na takwimu zake za ufungaji msimu uliopita. Hata hivyo, hadi sasa amekuwa akikosa alama za moja kwa moja kwenye mechi kubwa iwe ni mabao, pasi za mwisho au mchango unaoamua matokeo dhidi ya wapinzani wakubwa kama Yanga, mechi za hatua za juu za mashindano ya CAF au fainali za michuano ya ndani.
Hali hii imefanya baadhi ya wachambuzi kuanza kuhoji kama Ahoua anaweza kubeba uzito wa mechi zenye presha kubwa. Mechi hizi huambatana na presha ya mashabiki na matarajio makubwa ya klabu. Kwa mchezaji ambaye tayari ana mzigo wa kuthibitisha thamani yake, presha hii huongezeka maradufu na mara nyingi humfanya kucheza kwa tahadhari au kulazimisha badala ya kucheza kwa utulivu.
Hata hivyo, kukosa rekodi kwenye mechi kubwa hakumaanishi Ahoua hana uwezo wa kuamua mechi hizo. Kiungo huyo mshambuliaji anachotakiwa kutulia. Anaweza.
Ni kujiweka katika ubora wake kwenye mechi kubwa kwa kupata tukio moja chanya iwe ni bao, pasi ya mwisho au mchango wa kimbinu unaoleta ushindi ili kuvunja mzigo wa kisaikolojia na kumfungulia ukurasa mpya kama mchezaji wa mechi kubwa ndani ya Simba.