Kimbia marathoni uishi maisha marefu
Muktasari:
- Kwa upande wa wanawake, mwanariadha wa Tanzania, Magdalena Shauri aliongoza katika mbio za kilomita 21, akifuatiwa na Doreen Kibet Chetzop kutoka Kenya. Mafanikio ya wanariadha hawa yanatokana pia na kufanya mazoezi kwa juhudi binafsi, kuwa na ukakamavu na ustahimilivu uliojengwa kupitia mazoezi yanayozingatia weledi.
JUMAMOSI, Juni 27, 2026, mji wa Dodoma ulisimama kutokana na mbio maarufu za NBC Marathon 2026 zilizokusanya maelfu ya wakimbiaji kutoka ndani na nje ya Tanzania. Katika mbio hizo, mwanariadha wa Tanzania, Gabriel Geay, aliibuka mshindi wa mbio za kilomita 21 kwa upande wa wanaume akifuatiwa na Simon Kelenzyoke kutoka Kenya.
Kwa upande wa wanawake, mwanariadha wa Tanzania, Magdalena Shauri aliongoza katika mbio za kilomita 21, akifuatiwa na Doreen Kibet Chetzop kutoka Kenya. Mafanikio ya wanariadha hawa yanatokana pia na kufanya mazoezi kwa juhudi binafsi, kuwa na ukakamavu na ustahimilivu uliojengwa kupitia mazoezi yanayozingatia weledi.
Vilevile, huzingatia lishe bora, mapumziko ya kutosha na muda wa kulala, pamoja na kuwa na mwenendo na mtindo mzuri wa maisha unaojumuisha ulaji sahihi, kutovuta tumbaku na bidhaa zake, na kutotumia vilevi kupita kiasi.
Siri kubwa ya kutekeleza yote hayo ni kuwa na nidhamu ya hali ya juu. Hiyo ndiyo humwezesha mtu kutekeleza yote hayo bila kulazimishwa.
Mafanikio yao yanatukumbusha kuwa maisha ya mwanariadha, hususan wakimbiaji wa mbio ndefu, huchangia kuishi maisha marefu kutokana na faida nyingi za kiafya zinazotokana na ukimbiaji.
Kukimbia mara kwa mara huchangia kuwa na afya bora ya moyo na mzunguko wa damu, huku pia kukisaidia kudhibiti uzito wa mwili.
Ndiyo maana wanariadha wa mbio ndefu na wakimbiaji wa kawaida kutoka ukanda wa Afrika Mashariki wameendelea kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali, huku wengi wao wakiishi maisha marefu bila magonjwa yasiyoambukiza.
Ingawa kwa baadhi ya washiriki, marathon za aina hii huwa ni sehemu ya kujiburudisha. Mtakumbuka kuwa siku hiyo kulikuwa pia na burudani mbalimbali baada ya mbio hizo, ikiwamo maonesho ya ma-DJ maarufu.
Kwa mpenda burudani, hilo ni burudisho la akili ambalo lina faida kwa afya ya akili, mradi tu burudani hiyo ifanyike kwa kuzingatia kanuni za afya. Hata hivyo, katika makusanyiko makubwa hapakosekani matukio hatarishi, ikiwamo baadhi ya washiriki kujiingiza katika unywaji wa vilevi kupita kiasi na kujihusisha na mahusiano yanayoweza kusababisha ngono zembe.
USHAHIDI WA KITAFITI UNASEMAJE?
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani, wakimbiaji wa kawaida huishi kwa wastani wa miaka mitatu zaidi kuliko wasio wakimbiaji.
Utafiti uliochapishwa 2017 uliowahusisha watu zaidi ya 55,000 waliokuwa wakifuatiliwa kwa zaidi ya miaka 15 uligundua kuwa kukimbia kulihusishwa na kupungua kwa hatari ya mshtuko wa moyo na kiharusi kwa asilimia 45.
Ilionekana kuwa hata kukimbia kwa dakika tano hadi 10 kwa siku, kwa mwendo wa polepole wa takribani maili sita kwa saa, kunaweza kuleta matokeo chanya ya kiafya na kuongeza muda wa kuishi. Watafiti walizingatia umri, jinsia, uzito na vigezo vingine vya hatari ya kiafya, ikiwamo shinikizo la damu, kisukari, uvutaji sigara na matumizi ya pombe.
Matokeo hayo yalikuwa na uzito mkubwa kwa kuwa tafiti nyingine pia zimeonyesha kuwa, mbali na kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na mishipa, kukimbia hupunguza uwezekano wa kupata saratani na magonjwa ya mfumo wa fahamu kama vile ugonjwa wa kusahau na kutetemeka bila hiari.
Hali hiyo pia inawapa matumaini wakimbiaji wa mbio ndefu wa kiwango cha juu, akiwamo Simbu, kuwa na maisha marefu yenye afya njema.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo vya mapema duniani.
Faida kubwa wanazopata wanariadha wa mbio ndefu pamoja na wakimbiaji wa kawaida ni kuwa na afya bora ya moyo na kuepuka unene uliopitiliza. Hali hiyo huwasaidia kujiepusha si tu na magonjwa ya moyo, bali pia na magonjwa mengine yasiyoambukiza kama kisukari, ugonjwa sugu wa figo na kiharusi.
Hata hivyo, nchi nyingi za Afrika, hususan zile zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara na zenye uchumi mdogo, bado zinakabiliwa na magonjwa ya kuambukiza kama malaria, UKIMWI na kifua kikuu. Ndiyo maana wale wanaoshiriki marathon kwa ajili ya burudani wanashauriwa kuchukua tahadhari na kuepuka mahusiano ya chapu chapu yanayoweza kusababisha ngono zembe. Jambo hilo linaweza kuwaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU na magonjwa mengine yanayoenezwa kwa njia ya kujamiiana.
UKIMBIAJI HUSABABISHAJE MAISHA MAREFU?
Kwa ujumla, wakimbiaji wa mbio ndefu huishughulisha misuli na viungo vingi zaidi vya mwili kuliko mazoezi mengine kama kuogelea au kucheza muziki.
Mazoezi ya kukimbia yanatajwa kuwa miongoni mwa njia bora za kuujenga mwili, jambo linalochangia wanariadha wengi kuishi maisha marefu wakiwa na afya imara.
Kukimbia huongeza uwezo wa moyo kusukuma damu, hupunguza ugumu wa mishipa ya ateri na hupunguza hatari ya kupata kiharusi au mshtuko wa moyo kwa hadi asilimia 45. Kukimbia kwa uthabiti pia husaidia kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu na kuboresha mfumo wa kimetaboliki, hivyo kupunguza hatari ya kisukari cha aina ya pili.
Uchunguzi wa kijenetiki unaonyesha kuwa angalau dakika 75 za kukimbia kwa wiki zinaweza kusaidia kulinda seli dhidi ya kuzeeka, hivyo kuwafanya wakimbiaji kuonekana wachanga kibaiolojia kuliko umri wao halisi. Wakimbiaji wa kawaida wanakabiliwa na hatari ndogo kwa asilimia 40 ya kufa mapema, huku kila saa moja ya kukimbia ikikadiriwa kuongeza saa saba za maisha.
YUPI ANAWEZA KUISHI MUDA MREFU?
Ingawa wakimbiaji wa mbio ndefu wa kiwango cha juu huishi kwa muda mrefu, faida kubwa zaidi huonekana kwa watu wanaokimbia kwa kiwango cha wastani na kwa uthabiti.
Kukimbia kunaweza kupunguza umri wa mishipa ya ateri kwa takribani miaka minne, hivyo kuufanya mfumo wa moyo na mishipa kuwa na uwezo mzuri zaidi wa kusafirisha damu.
Kuboreka kwa afya ya mishipa ya damu husaidia kupunguza hatari ya magonjwa kama shinikizo la damu, shambulio la moyo na kusimama ghafla kwa moyo.
Mambo mengine yanayochangia tofauti hizo ni pamoja na mwenendo na mitindo mibaya ya maisha kwa baadhi ya wakimbiaji. Kwa mfano, ni vigumu kwa mkimbiaji kuishi maisha marefu ikiwa anakula kiholela, hapumziki, halali saa nane hadi 10 kwa siku, anatumia tumbaku na bidhaa zake, ikiwamo shisha, au anakunywa pombe kupita kiasi.