Kikosi ghali kwenye Ligi Kuu England hiki hapa

LONDON, ENGLAND: NDO hivyo, Ligi Kuu England sasa inakaribia kutengeneza kikosi cha kwanza chenye thamani ya Pauni 1 bilioni baada ya kiungo mshambuliaji Florian Wirtz kumpoka namba staa wa zamani wa Manchester United kwenye kikosi kinachoundwa na wachezaji waliosajiliwa kwa pesa nyingi ligi hiyo ya kibabe.
Unakijua kikosi chenyewe kilivyo? Nani anaunda timu hiyo?
Kipa: Kepa Arrizabalaga
(Athletic Bilbao - Chelsea, Pauni 71.6milioni)
Gianluigi Buffon alikuwa kipa ghali zaidi kwa siku 5,820. Ederson alishika hadhi hiyo kwa miezi 13. Alisson alidumu kwenye cheo cha kuwa kipa ghali kwa wiki tatu. Na baada ya hapo, taji hilo lilitua kwa Kepa, ambaye hadi sasa ndiye kipa ghali zaidi kuwahi kusajiliwa kwenye Ligi Kuu England, aliponaswa na Chelsea akitokea Bilbao kwa ada ya Pauni 71.6 milioni. Atakuwa golini kwenye kikosi hiki.

Beki wa kati: Harry Maguire
(Leicester City - Man United, Pauni 80milioni)
Manchester United ilipokuwa chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer ilimfanya beki wa kati, Harry Maguire kupata hadhi ya kuwa beki ghali zaidi duniani wakati ilipomsajili kwa Pauni 80 milioni kutoka Leicester City. Maguire alipita kwenye nyakati ngumu kwenye kikosi hicho cha Old Trafford kabla ya kuja kukubalika na kocha mpya, Ruben Amorim, ambaye amekuwa akimpa nafasi.
Beki wa kati: Josko Gvardiol
(Leipzig - Man City, Pauni 77milioni)
Ligi Kuu England siku zote imekuwa ikimtafuta Gvardiol. Leeds ilikaribia kumsajili staa huyo wa Croatia katika msimu baada ya kupanda daraja, huku beki huyo wa kati aliweka hadharani ndoto za kwenda kucheza Liverpool. Chelsea ilijaribu na kushindwa kunasa saini yake, kabla ya Manchester City kushinda vita hiyo kwa kunasa huduma yake kwa kulipa Pauni 77.4 milioni.

Beki wa kati: Virgil van Dijk
(Southampton - Liverpool, Pauni 75milioni)
Kabla ya Liverpool kumsajili Van Dijk kwenye Siku ya Mwaka Mpya 2018, beki wa kati ghali zaidi alikuwa David Luiz (Pauni 50milioni), ambapo Mbrazili huyo alimpangua Mbrazili mwenzako Thiago Silva (Pauni 32milioni) kwenye nafasi hiyo mwaka 2014. Baada ya usajili wa Van Dijk, Mdachi huyo alishikilia nafasi ya kuwa beki ghali duniani aliponaswa kwa Pauni 75 milioni hadi hapo Maguire aliposajiliwa.
Winga wa kulia: Antony
(Ajax - Man United, Pauni 82milioni)
Wasiwasi uliibuka mapema kabisa kabla ya Manchester United kukamilisha dili la kumnasa Mbrazili hiyo kwa Pauni 82 milioni na kwenda kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wao ghali kabisa kikosini. Kocha, Erik ten Hag ndiye aliyekamilisha usajili huo akimnasa Antony kutoka Ajax. Hata hivyo, mambo hayakuwa mazuri na kujikuta akitolewa kwa mkopo baada ya ujio wa kocha Amorim.

Kiungo wa kati: Moises Caicedo
(Brighton - Chelsea, Pauni 115milioni)
Brighton ililipa Pauni 4.5 milioni tu kunasa huduma ya kiungo wa kati, Caicedo kutokea Independiente del Valle kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili mwaka 2021. Baada ya miaka miwili na nusu kwenye timu hiyo na kucheza mechi 53, kiungo huyo alipata dili lililovunja rekodi ya uhamisho Uingereza, wakati aliponyakuliwa na Chelsea kwa ada ya Pauni 115 milioni na kupata namba kikosi hiki.
Kiungo wa kati: Declan Rice
(West Ham - Arsenal, Pauni 105milioni)
Baada ya ofa mbili kukataliwa, Arsenal ilivamia mawindo ya Manchester City kwenye vita ya kumsajili kiungo wa kati, Declan Rice kutoka West Ham United na kufanikiwa kunasa saini ya mchezaji huyo kwa ada ya Pauni 105 milioni. Jambo hilo limemfanya staa huyo Mwingereza, anayeripotiwa kuwa na akili kubwa ya mpira kupata nafasi katika kikosi hiki cha mastaa ghali England.
Kiungo wa kati: Enzo Fernandez
(Benfica - Chelsea, Pauni 106.8milioni)
Baada ya zama za Roman Abramovich kumalizika kwenye kikosi cha Chelsea na kuja mwekezaji Mmarekani Todd Boehly, ilifanya dili kadhaa za pesa nyingi, ikiwamo kunasa huduma ya kiungo wa Kiargentina, Enzo Fernandez kwa ada ya Pauni 106.8 milioni akitokea Benfica kwenye dirisha la Januari. Kwa ada aliyosajiliwa Enzo, ndicho kitu kinachomfanya apate nafasi kwenye kikosi hiki ghali England.
Winga wa kushoto: Jack Grealish
(Aston Villa - Man City, Pauni 100milioni)
Mwaka mmoja ni mkubwa sana kwenye soka. Kuna nyakati, Grealish alikuwa habari nzito kwenye Ligi Kuu England kabla ya mambo kubadilika kwenye kikosi cha Manchester City na kujikuta akikosa nafasi na sasa anaripotiwa kuwa na mpango wa kuachana na timu hiyo ya Emirates. Man City ilimsajili Grealish kwa Pauni 100 milioni akitokea Aston Villa na kupata nafasi kwenye kikosi ghali.

Kiungo mshambuliaji: Florian Wirtz
(Bayer Leverkusen - Liverpool, Pauni 116.5milioni)
Dili hili limefanyika kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya Liverpool kukubali kunasa huduma ya Florian Wirtz kwa ada ya Pauni 116.5 milioni akitokea Bayer Leverkusen, ambapo miamba hiyo ya Anfield, itatanguliza Pauni 100 milioni kwanza na kisha italipa Pauni 16 milioni kama pesa ya ziada itakayotakana na huduma bora atakayoonyesha staa huyo uwanjani.
Straika: Romelu Lukaku
(Inter Milan -
Chelsea, Pauni 97.5milioni)
Kuna kitu kilikuwa hakijakamilika kwa straika Romelu Lukaku wakati mara ya kwanza alipojiunga na Chelsea akiwa kinda, ambapo aliachana na timu hiyo kwenda Everton, kisha Manchester United, halafu Inter Milan na kurudi Chelsea, ambako alisajiliwa kwa pesa nyingi sana, Pauni 97.5 milioni na hivyo kuingia kwenye kikosi hiki cha mastaa ghali waliosajiliwa kwenye Ligi Kuu England.