Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kikosi cha matajiri Kombe la Dunia 2026

MATAJIRI Pict

Muktasari:

  • Kikosi kinachoundwa na mastaa 11 kutoka mataifa mbalimbali kina utajiri unaokadiriwa kuzidi dola 3.2 bilioni (zaidi ya Sh trilioni 8.3), fedha zilizotokana na mishahara mikubwa, mikataba ya matangazo na biashara binafsi walizowekeza nje ya uwanja.

NEW YORK, MAREKANI: KOMBE la Dunia 2026 halitakuwa mkusanyiko wa wachezaji bora zaidi duniani, bali pia wa baadhi ya wanamichezo matajiri zaidi katika historia ya soka.

Kikosi kinachoundwa na mastaa 11 kutoka mataifa mbalimbali kina utajiri unaokadiriwa kuzidi dola 3.2 bilioni (zaidi ya Sh trilioni 8.3), fedha zilizotokana na mishahara mikubwa, mikataba ya matangazo na biashara binafsi walizowekeza nje ya uwanja.

Kinara wa orodha hiyo ni Cristiano Ronaldo wa Ureno ambaye utajiri wake unakadiriwa kufikia dola 1.3 bilioni (zaidi ya Sh 3.3 trilioni).

Mbali na mshahara mkubwa anaopata Al Nassr, Ronaldo amejijengea himaya ya biashara inayojumuisha hoteli za CR7, bidhaa za mavazi, manukato, vituo vya mazoezi, uwekezaji wa mali na mikataba mikubwa ya matangazo na kampuni kama Nike, Binance na Herbalife.

Anayemfuatia ni Lionel Messi wa Argentina mwenye utajiri unaokadiriwa kufikia dola milioni 900 (zaidi ya Sh trilioni 2.3). Nahodha huyo wa Argentina amevuna fedha nyingi kupitia mishahara ya Barcelona, PSG na Inter Miami huku mikataba yake na Adidas, Apple, Pepsi, Mastercard na uwekezaji katika sekta ya mali ikiongeza thamani ya utajiri wake kila mwaka.

MATAJ 04

Mshambuliaji wa Brazil, Neymar, anashika nafasi ya tatu akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia dola 400milioni (zaidi ya Sh  1.0 trilioni).

Chanzo kikubwa cha fedha zake ni mkwanja aliovuna Barcelona, PSG na Saudi Arabia pamoja na mikataba ya Puma, Red Bull, PokerStars na matangazo mengine ya kibiashara.

Nyota wa Ufaransa, Kylian Mbappe, tayari amejiweka miongoni mwa wanasoka matajiri zaidi duniani akiwa na utajiri wa takribani dola 250 milioni (zaidi ya Sh 650 bilioni).

MATAJ 05

Mshahara wake mkubwa, bonasi za mikataba na ushirikiano wa kibiashara na Nike, Hublot, Oakley na EA Sports vimemfanya kuwa moja ya sura muhimu zaidi katika biashara ya soka la kisasa.

Kiungo wa Ubelgiji, Kevin De Bruyne, anatajwa kuwa na utajiri wa karibu dola 100milioni (zaidi ya Sh 260 bilioni). Fedha hizo zimetokana na mikataba yake ya muda mrefu katika Ligi Kuu England, bonasi za mashindano, matangazo na uwekezaji katika biashara mbalimbali.

Luka Modric wa Croatia ana utajiri unaokadiriwa kufikia dola 80 milioni (zaidi ya Sh 208 bilioni). Nahodha huyo wa Croatia amejikusanyia fedha hizo kupitia mafanikio ya muda mrefu akiwa Real Madrid, matangazo ya kibiashara, uwekezaji wa mali na hisa katika kampuni mbalimbali.

MATAJ 06

Katika nafasi ya kiungo mkabaji, Casemiro wa Brazil anakadiriwa kuwa na utajiri wa dola 70 milioni (zaidi ya Sh 182 bilioni). Mchezaji huyo amefaidika na mikataba mikubwa aliyosaini Ulaya pamoja na matangazo ya kampuni mbalimbali za kimataifa.

Safu ya ulinzi nayo imejaa mamilionea. Virgil van Dijk wa Uholanzi ana utajiri unaokadiriwa kufikia dola 50 milioni  (zaidi ya Sh 130 bilioni).

Sehemu kubwa ya fedha hizo imetokana na mishahara ya Liverpool, bonasi za mafanikio na mikataba ya udhamini wa kampuni za vifaa vya michezo.

Kalidou Koulibaly wa Senegal anakadiriwa kuwa na utajiri wa dola 40 milioni (zaidi ya Sh 104 bilioni). Uhamisho wake kwenda Saudi Arabia ulimfanya kuwa miongoni mwa mabeki wanaolipwa mishahara mikubwa zaidi duniani huku mikataba ya matangazo nayo ikichangia mapato yake.

MATAJ 02

Marquinhos wa Brazil ana utajiri wa karibu dola 35milioni (zaidi ya Sh 91 bilioni). Nahodha huyo wa PSG amefaidika na mishahara mikubwa ya klabu yake, bonasi za mashindano na mikataba ya kibiashara.

Lango la kikosi hiki linalindwa na Manuel Neuer wa Ujerumani ambaye utajiri wake unakadiriwa kufikia dola 50milioni  (zaidi ya Sh 130 bilioni).

Mbali na mshahara alioupata Bayern Munich kwa miaka mingi, Neuer amewekeza katika biashara mbalimbali huku akiwa balozi wa kampuni kadhaa za kimataifa ikiwemo Adidas.

Kama kuna jambo linalowaunganisha mastaa hawa, basi ni uwezo wao wa kubadili mafanikio ya uwanjani kuwa utajiri mkubwa nje ya uwanja. Wengine wamewekeza katika hoteli, mali isiyohamishika, bidhaa za mavazi, teknolojia na biashara nyingine zinazowaingizia mamilioni ya dola kila mwaka.

MATAJ 01

Kombe la Dunia 2026 linaweza kuwa safari ya mwisho kwa baadhi ya nyota hawa katika mashindano makubwa zaidi ya soka duniani, lakini hata watakapostaafu, majina yao yataendelea kuishi si kwa sababu ya mabao na makombe pekee, bali pia kutokana na himaya za kifedha walizojenga kupitia mchezo huo.

Iwapo kikosi hiki kingeunganishwa katika timu moja, kingekuwa si tu miongoni mwa timu zenye vipaji vikubwa zaidi duniani, bali pia timu yenye utajiri mkubwa zaidi kuwahi kuonekana katika historia ya Kombe la Dunia.