Kikosi bora cha nusu fainali Kombe la Dunia
Muktasari:
- Katika pambano la kwanza, Hispania iliendelea kuonyesha ubora wake baada ya kuichapa Ufaransa mabao 2-0. Kikosi hicho kilitawala umiliki wa mpira, kikaongoza mchezo kwa utulivu na kuwadhibiti washambuliaji hatari wa Ufaransa kwa nidhamu kubwa ya kiuchezaji.
ATLANTA, MAREKANI: NUSU fainali za Kombe la Dunia ziliandika simulizi mbili za kusisimua huku Hispania, Ufaransa, Argentina na England zikipigania tiketi ya kucheza mechi ya mwisho ya michuano hiyo.
Katika pambano la kwanza, Hispania iliendelea kuonyesha ubora wake baada ya kuichapa Ufaransa mabao 2-0. Kikosi hicho kilitawala umiliki wa mpira, kikaongoza mchezo kwa utulivu na kuwadhibiti washambuliaji hatari wa Ufaransa kwa nidhamu kubwa ya kiuchezaji.
Ushindi huo uliweka wazi uimara wa kikosi cha kocha Luis de la Fuente, kilichochanganya ubora wa kushambulia na uimara wa safu ya ulinzi.
Nusu fainali ya pili ilikuwa ya kusisimua zaidi ambapo England ilianza kwa kasi na kupata bao kupitia Anthony Gordon, jambo lililoonekana kuwakaribisha kwenye fainali yao ya kwanza tangu mwaka 1966.
Hata hivyo, uzoefu wa Argentina ulizungumza mwishoni mwa mchezo. Enzo Fernández aliisawazishia timu hiyo kabla ya Lautaro Martínez kufunga bao la ushindi dakika za mwisho akimalizia pasi ya nahodha Lionel Messi. Ushindi huo uliipeleka Argentina kwenye fainali nyingine ya Kombe la Dunia huku ukiizima ndoto ya England.
Sasa Hispania na Argentina zitakutana kwenye fainali inayotarajiwa kuwa kali, ikipeleka uso kwa uso falsafa ya umiliki wa mpira ya Hispania dhidi ya uzoefu, uthabiti na ubora wa kushambulia wa Argentina.
Kikosi Bora cha Nusu Fainali
Kipa: Unai Simón (Hispania) – 7.0
Aliendelea kuwa mwamba langoni kwa kuonyesha utulivu mkubwa dhidi ya Ufaransa. Ingawa hakukabiliwa na mashambulizi mengi, aliokoa mipira muhimu, alitawala vyema mipira ya juu na kusaidia ujenzi wa mashambulizi kutoka nyuma. Clean sheet nyingine ilithibitisha ubora wake.
Beki wa Kulia: Pedro Porro (Hispania) – 8.1
Alikuwa miongoni mwa nyota wa mchezo. Aliwadhibiti washambuliaji wa pembeni wa Ufaransa huku akitoa mchango mkubwa mbele. Alifunga bao na kuonyesha uwezo mkubwa wa kushambulia na kulinda kwa kiwango cha juu.
Beki wa Kati: Pau Cubarsí (Hispania) – 7.4
Kijana huyo aliendelea kuwavutia wengi kwa ukomavu wake licha ya kucheza dhidi ya safu kali ya ushambuliaji ya Ufaransa. Alifanya kuokoa hatari nyingi, akashinda mipambano muhimu na kuanzisha mashambulizi kupitia pasi zake safi.
Beki wa Kati: Aymeric Laporte (Hispania) – 7.2
Uzoefu wake ulionekana wazi. Aliiongoza safu ya ulinzi kwa utulivu, akiondoa hatari, kushinda mipira ya juu na kuzuia washambuliaji wa Ufaransa kupata nafasi za wazi.
Beki wa Kushoto: Marc Cucurella (Hispania) – 7.1
Alifanya kazi kubwa pande zote mbili za uwanja. Aliwadhibiti wachezaji wa pembeni wa Ufaransa na mara kwa mara aliongeza nguvu kwenye mashambulizi kupitia mbio zake za kupanda mbele.
Kiungo: Leandro Paredes (Argentina) – 7.3
Alikuwa mhimili wa kiungo cha Argentina kwa kuvunja mashambulizi ya England na kulinda safu ya ulinzi. Pia alitumia uzoefu wake kutuliza kasi ya mchezo pale ilipohitajika.
Kiungo: Elliot Anderson (England) – 7.3
Licha ya England kuondolewa, Anderson alipambana kwa nguvu katikati ya uwanja. Alikimbia sana, akapress kwa ufanisi na kuwapa wakati mgumu viungo wa Argentina.
Kiungo: Rodri (Hispania) – 7.5
Aliendelea kuthibitisha kwa nini ni mmoja wa viungo bora duniani. Alitawala tempo ya mchezo, akirejesha umiliki wa mpira mara kwa mara na kuiongoza Hispania kucheza kwa utulivu mkubwa.
Kiungo Mshambuliaji: Enzo Fernández (Argentina) – 7.5
Alikuwa moyo wa Argentina. Mbali na kazi kubwa ya kukaba, alifunga bao muhimu la kusawazisha lililobadili mwelekeo wa mchezo na kuipa timu yake nguvu mpya.
Mshambuliaji: Lautaro Martínez (Argentina) – 7.3
Aliingia dakika za mwisho lakini akabadilisha mchezo. Harakati zake ziliisumbua England kabla ya kufunga bao la ushindi lililoivusha Argentina kwenda fainali.
Mshambuliaji: Lionel Messi (Argentina) – 8.1
Nahodha huyo aliendelea kuonyesha ubora wake katika mechi kubwa. Aliongoza kwa mfano, akatengeneza nafasi nyingi na kutoa pasi ya bao la ushindi kwa Lautaro Martínez. Uwezo wake wa kubadili matokeo katika nyakati muhimu uliendelea kuwa silaha kubwa ya Argentina.