Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kigingi kinachomsubiri straika mpya Mashujaa FC

Muktasari:

  • Michael alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar akiwa na KVZ baada ya kufunga mabao 21 katika mechi 29 alizocheza akitumia dakika 2320 kwa msimu wa 2025-2026, huku akitoa pia asisti nane na kumfanya kuhusika kwenye jumla ya mabao 29.

JULAI 20, 2026, uongozi wa maafande wa Mashujaa FC ulimtambulisha mshambuliaji Michael Joseph ili kuongeza nguvu katika kikosi hicho kwa msimu wa 2026-2027 baada ya kuachana na kikosi cha KVZ inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).

Michael alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar akiwa na KVZ baada ya kufunga mabao 21 katika mechi 29 alizocheza akitumia dakika 2320 kwa msimu wa 2025-2026, huku akitoa pia asisti nane na kumfanya kuhusika kwenye jumla ya mabao 29.

Kiwango bora cha nyota huyo kiliiwezesha KVZ kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar, baada ya kumaliza na pointi 67, nyuma ya JKU iliyomaliza ya pili na pointi 64 kwa msimu wa 2025-2026, jambo lililoivutia Mashujaa kuitaka saini yake.

Baada ya nyota huyo kukamilisha usajili wake, kwa sasa ana kazi kubwa ya kufanya ili kuendelea kufanya alichokifanya akiwa Zanzibar, ingawa, rekodi zinaonyesha wengi wao wameshindwa kuwika Bara, kama ambavyo Mwanaspoti linavyowaelezea.


MAABAD MAULID

Mshambuliaji, Maabad Maulid ni nyota mwingine aliyefanya vizuri akitokea Zanzibar na kuwavutia mabosi wa Coastal Union kumsajili, japo licha ya uwezo wake huo mzuri wa kufunga, ila amekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka Ligi Kuu Bara.

Maabad alijiunga na kikosi hicho Julai 11, 2022, akitokea KVZ ya Zanzibar ambapo alikuwa pia mfungaji bora mara mbili mfululizo, akianza na msimu wa 2020-2021, alipofunga mabao 17, kisha na msimu uliofuata wa 2021-2022, akafunga mabao 21.

Licha ya rekodi hiyo bora kwake, ila tangu amejiunga na Coastal Union hajawahi kufikisha hata mabao 15 ya Ligi Kuu Bara, kwani msimu wake wa kwanza yaani wa 2022-2023, alifunga mabao manne, huku msimu wa 2023-2024, akifunga mabao matatu tu. Msimu wa 2024-2025, nyota huyo alifunga mabao matano, huku bao la mwisho kufunga lilikuwa ni la ushindi wa kikosi hicho wa 2-1, dhidi ya maafande wa JKT Tanzania, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, Februari 7, 2025.

Kwa msimu wake bora hadi sasa ni uliopita wa 2025-2026, ambapo mshambuliaji huyo alifunga mabao 10, ya Ligi Kuu Bara na kuonyesha kiwango cha kuvutia, huku msimu huu wa 2026-2027, amefunga matatu na kusubiriwa ikiwa ataendeleza makali yake.


ABDALLAH IDD ‘PINA’

Abdallah Idd ‘Pina’ sio jina geni kwa mashabiki wa Ligi Kuu, kwani nyota huyo alijiunga na Pamba Jiji ya Mwanza, Agosti 7, 2025, akitokea Mlandege ya Zanzibar alipoonyesha kiwango cha kuvutia na kusaini mkataba wa miaka miwili kikosini.

Nyota huyo aliyejiunga na Pamba msimu wa 2025-2026, akitokea Mlandege ya Zanzibar alitabiriwa kufanya makubwa kutokana na alichofanya msimu wa 2024-2025, akiwa na kikosi hicho, ingawa licha ya matarajio hayo ila mambo yalikuwa ni tofauti.

Msimu wa 2024-2025, katika Ligi Kuu Zanzibar, Pina aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21, kwenye mechi 22, alizozicheza, huku akichangia pia mengine 12 (asisti), ingawa tangu aichezee Pamba Jiji hajafunga bao hadi alipoondoka.

Mshambuliaji huyo alishindwa kuonyesha makali yake yaliyotarajiwa na timu hiyo na katika dirisha dogo la Januari 2026, alijiunga na Muembe Makumbi City kwa mkopo wa miezi sita, japo msimu wa 2026-2027, amejiunga na KVZ zote za Zanzibar.

Pina aliyeianza safari ya soka mwaka 2015 amezichezea pia timu za, Magomeni, Gulioni, Jang’ombe Boys, Polisi Tanzania, Kipanga, Kundemba, Mlandege na Muembe Makumbi City, huku za nje ni za Alzakhir ya Dubai na Chaux Sport ya DR Congo.


MUDRIK ABDI SHEHE ‘GONDA’

Baada ya kuondoka Seleman Mwalimu ‘Gomez’ katika kikosi cha Fountain Gate, mabosi wa timu hiyo walimsajili, Mudrik Abdi Shehe ‘Gonda’ kutoka JKU ya Zanzibar kwenye dirisha dogo la Januari 2025, kufuatia kufunga mabao manane ya kikosi hicho.

Usajili wa nyota huyo, ulikuwa wa kuziba nafasi ya Gomez, aliyejiunga na Wydad Casablanca ya Morocco kisha kutolewa kwa mkopo Simba na sasa Yanga, ingawa ujio wa Gonda ulimshuhudia akimaliza msimu wa 2024-2025, bila bao lolote la Ligi Kuu.

Msimu wa 2025-2026, nyota huyo alitoa gundu baada ya kufunga bao moja la Ligi Kuu, katika ushindi wa Fountain Gate wa 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji mechi iliyopigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, Oktoba 17, 2025. Licha ya kutabiriwa makubwa na kikosi hicho cha Fountain Gate, ila mshambuliaji huyo alishindwa kuwashawishi mabosi pia na msimu huu wa 2026-2027, akapewa mkono wa kwaheri na kujiunga na KVZ inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar.


IBRAHIM HAMAD HILIKA

Hilika ni miongoni mwa washambuliaji bora waliofanya makubwa katika Ligi ya Zanzibar, japo kwa upande wa Ligi Kuu Bara, nyota huyo ameshindwa kuonyesha makali yake, licha ya kuzichezea timu za, Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar na TRA United.

Mshambuliaji huyo, alijizoelea umaarufu mkubwa wakati akiichezea Zimamoto ya visiwani Zanzibar, ambapo alikuwa mfungaji bora mara mbili, akianza msimu wa 2016-2017 alipofunga jumla ya mabao 33, kuanzia Ligi ya Kanda hadi hatua ya nane bora.

Katika Kanda ya Unguja, Hilika alifunga mabao 19 msimu huo, huku kwenye hatua ya nane bora nyota huyo alifunga jumla ya mabao 14, hivyo kuhitimisha msimu kibabe kwa kufunga 33, hali iliyovutia timu mbalimbali zilizohitaji kupata saini yake.

Msimu mwingine wa 2019-2020, nyota huyo akaendeleza balaa akiwa na kikosi hicho cha Zimamoto, ambapo alifunga jumla ya mabao 20, akimpita bao moja tu mshambuliaji wa kikosi cha JKU, Shehuu Magaji Buwa aliyehitimisha msimu huo na mabao 19.

Kabla ya Hilika kuibuka mfungaji bora, msimu uliopita wa 2018-2019, nyota wa Zimamoto, Abubakar Khamis Sufiani ‘Kabela Kanu’ na Mussa Ali Mbarouk wa KMKM, wote walikuwa wafungaji bora wa Ligi hiyo baada ya kufunga mabao 23, kila mmoja wao. Licha ya rekodi tamu kwa Hilika, lakini nyota huyo alishindwa kuonyesha makali yake kutokana na ufinyu wa nafasi zaidi ya kucheza, jambo lililochangia kwa msimu wa 2026-2027, TRA United kufikia makubaliano ya pande mbili ya kuachana naye.


YASSIN MGAZA

Nyota mwingine ni Yassin Mgaza ambaye pia alikuwa mfungaji bora katika Ligi ya Zanzibar akiwa na kikosi cha KMKM msimu wa 2022-2023, ambapo alichangia mabao 25, baada ya kufunga 17 na kuasisti manane kwenye mechi 25 kati ya 30 alizocheza.

Mgaza alijiunga na KMKM akitokea Mbuni ya Arusha ambayo kwa sasa inashiriki Ligi ya Championship, ingawa kwa msimu huo ilikuwa Ligi Daraja la Pili, First League, ambapo alionyesha kiwango kizuri kilichoishawishi KMKM kuihitaji saini yake.

Akiwa na Mbuni, Mgaza alihusika katika jumla ya mabao 22 kwa msimu mzima kwenye mechi 16, alizocheza, baada ya kufunga mabao 16 na kuasisti mengine sita, ingawa kiwango hicho bora kwake alikiendeleza hadi alipojiunga na kikosi cha KMKM.

Baada ya hapo, mabosi wa Dodoma Jiji wakamsajili kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji kwa msimu wa 2023-2024 na kubeba matarajio makubwa ndani ya kikosi hicho, ingawa aliangukia pua baada ya kufunga mabao matatu kwa msimu mzima.

Kwa msimu wa 2024-2025, Mgaza alifunga bao moja lililokuwa la kichapo ilichokipata Dodoma Jiji cha mabao 2-1, dhidi ya Singida Black Stars, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Liti Singida, Desemba 12, 2024.

Mwenendo wa nyota huyo sio wa kuridhisha tofauti na mambo makubwa aliyoyafanya akiwa Ligi Kuu Zanzibar, kwani msimu wa 2025-2026 alifunga mabao matatu, huku msimu huu wa 2026-2027 hadi sasa amefunga bao lake moja tu.


MICHAEL JOSEPH

Baada ya kufanya vizuri na kuibuka mfungaji bora akiwa na KVZ kwa kufunga mabao 21 katika mechi 29, alizocheza kwa msimu wa 2025-2026, huku akitoa pia asisti nane na kuhusika kwenye jumla ya mabao yake 29 kwa sasa ana kazi ya kufanya. Bado mshambuliaji huyo hajafunga bao lolote hadi sasa katika Ligi Kuu Bara, huku akikabiliwa na ushindani wa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kinachoongozwa na mfungaji bora wa msimu wa 2021-2026, George Mpole aliyesajiliwa msimu huu.

Mpole aliyefunga mabao 17 kwa msimu wa 2021-2022 akiwa na kikosi cha Geita Gold na kuibuka mfungaji bora amejiunga na Mashujaa FC msimu huu akitokea Tanzania Prisons, jambo linaloongeza ushindani na mshambuliaji mwenzake, Michael Joseph.