Prime
Kazi imeanza, unabisha ulikuwepo?
MSIMU wa 62 wa Ligi Kuu Bara unaanza leo kwa mechi mbili zitakazopigwa katika majiji ya Tanga na Dar es Salaam.
Kupigwa kwa mechi hizo kunaashiria kuanza vita ya karibu miezi tisa ikatayohusisha mechi 240 kupitia klabu 16 kuwania ubingwa wa msimu wa 2025-2026.
Kwa mujibu wa ratiba leo zinapigwa mechi kati ya KMC na Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa KMC Complex kuanzia saa 10:00 jioni kisha saa 1:00 usiku itakuwa zamu ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union kuikaribisha Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Historia inaonyesha kuwa Ligi Kuu Bara ilianza rasmi 1921 Mzizima (sasa Dar es Salaam ikihusisha timu za mkoa huo na Pwani kabla ya kupitia mabadiliko mbalimbali.
Hata hivyo, rekodi za ligi hizo za miaka ya 1920 ni kama hazipo na kilichopo kwa sasa ni historia ya kuanza kwake katika mfumo wa kushirikisha timu za mikoa tofauti mwaka 1965 ikipewa jina la Ligi ya Taifa.
Inaelezwa aliyeasisi Ligi ya Taifa ni kocha wa zamani wa timu ya taifa, Milan Celebic, raia wa Yugoslavia aliyetoa wazo ili kumrahisishia kupata wachezaji 1964 na mwaka mmoja baadaye ligi ikaanza ikishirikisha klabu sita. Klabu hizo zilizoasisi ligi hiyo ni pamoja na Tobacco au Sigara, Young Africans (Yanga), Sunderland (Simba), Coastal Union, TPC Moshi na Manchester United ya Tanga na kwa miaka 62 imeshuhudiwa timu tisa zilizotwaa ubingwa hadi msimu uliopita.
DAR YAFUNIKA
Rekodi zinaonyesha tangu Ligi ya Bara ianze 1965 klabu za Dar es Salaam ndizo zilizotawala kwa kutwaa mataji mengi. Yanga ambayo ndio mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo imetwaa mataji 31, ikifuatiwa na Simba 22, huku Cosmopolitan, Pan Africans na Azam FC zimebeba kila moja mara moja.
Yanga imetwaa ubingwa 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2007-08, 2008-2009, 2010-2011, 2012-2013, 2014-2015, 2015-2016, 2016-2017, 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025.
Simba katika mataji 22 imetwaa 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007 uliokuwa wa Ligi Ndogo), 2009-2010, 2011-2012, 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.
Cosmopolitan ilitwaa 1967, ikafuatiwa na Pan Africans iliyobeba 1982 na Azam ilitwaa msimu wa 2013-2014.
KARIAKO NDO BALAA
Licha ya Dar es Salaam kuonekana kuwa vinara wa kubeba mataji mengi ikiwa imekusanya ubingwa mara 56, lakini kitongoji cha Kariakoo ndicho kimeonekana kuwa balaa zaidi kwa kubeba mara 55, huku sita yakibebwa na klabu tano za Mseto na Mtibwa Sugar za Morogoro, Tukuyu Stars ya Mbeya na Coastal Union ya Tanga.
Mataji 31 ya Yanga yapo mitaa ya Twiga na Jangwani, huku 22 ya Simba yako mitaa ya Msimbazi na Masasi, ilhali mawili ya Cosmopolitan na Pan Africans yapo mitaa ya Sikukuu na Mkunguni (Cosmo) na Swahili kwa Pan.
MOROROGO WAMO
Mkoa wa Morogogo ndio uliokuwa wa kwanza nje ya Dar es Salaam kubeba ubingwa ukifanya hivyo 1975 ukiwa na wachezaji nyota kina Said Gedegela, Charle Boniface Mkwasa, Vincent Mkude, Ramadhan Matola, Aluu Ally, Shiwa Lyambiko, Hassan Shilingi, Omar Hussein, Jumanne Hassan ‘Masimenti’ Miraji Salum, Abdallah Hussein, Hussein Ngulungu, Hemed Mussa, Roma Mapunda, Kassim Mmanga na wengine wakiwa chini ya kocha Mohammed Hussein Hassan ‘Msomali’. Mmoja wa makocha bora waliowahi kutokea nchini. Lakini kulikuwa na mtu aliyeamini Moro ilibahatisha tu kwa klabu ya mkoa kubeba taji la Ligi ya Bara, Mtibwa Sugar ilirejea mafanikio kwa kubeba mara mbili mfululizo 1999 na 2000 ikiwa ndio ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa na kisha kutetea.
Katika ligi ya msimu huu Mtibwa wapo baada ya kurejea tangu waliposhuka 2023-2024 baada ya kudumu katika ligi kwa misimu zaidi ya 20 tangu 1996.
BANYAMBALA
Ukiachana na Mseto na Cosmo zilizozishtua Simba na Yanga kwa kutwaa ubingwa mbele yao, 1986 ulikuwa mwaka wa maajabu wakati Tukuyu Stars ilipopanda daraja na kutikisa enzi za Daraja la Kwanza ikibeba ubingwa.
Tukuyu iliyoundwa na nyota wakali baadaye walisajiliwa na klabu nyingine na kuisababisha ishuke daraja msimu uliofuata na kupambana kurejea kabla ya kushuka kimoja ikiwa imeshaanza kusahaulika masikioni mwa wadau wa soka.
Kikosi hicho cha Tukuyu kilichokuwa chini ya Kocha Athuman Juma kiliundwa na wakali kama Peter Mwakibibi, Mbwana Makatta, Godwin Aswile, Suleiman Mathew, Kelvin Haule, Hussein Zitto, Karabi Mrisho, Ally Kimwaga, Danford Ngessi, Fadhil Hembe, Richard Lumumba.
Wengine walikuwa ni Yusuph Kamba, John Alex, Daniel Chundu, Aston Pardon, Selemani Mwankenja, Taisi Mwalyoga, Daniel Chundu, Wilfred Sangula, Abdallah Shaibu, Mohamed Salehe, Haji Shomari, Augustino Mumbe, Abdalla Madodi, Michael Kidilu, Justin Mtekele, Lawlance Pyukula, Asanga Aswile, Dickson Ntole na Benson Kasambo.
Meneja wa timu hiyo alikuwa Lucas Monyo na mlezi akiwa Ramnick Patel ‘Kaka’
WAGOSI WA KAYA
Coastal Union walifanya yao 1988 ikiwa miaka miwili tu tangu Tukuyu Stars ilipoziduwaza Simba na Yanga kwa kubeba ubingwa.
Msimu huo ulikuwa ni wa aina yake kwa Mkoa wa Tanga kwani, kwani mwaka huo pia watani wa jadi wa Coastal Union yaani African Sports ‘Wana Kimanumanu’ walibeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Muungano.
Wagosi wa Kaya walibeba ubingwa huo wakiwazidi ujanja Yanga waliokuwa wakichuana nao kwa muda mrefu wakiwa na vichwa matata vinavyoendelea kukumbukwa na wadau wa soka nchini.
Nyota walioipa Coastal taji hilo la kwanza la pekee ni Hamisi Makene, Mohammed Mwameja, Saidi Kolongo, Douglas Muhani, Joseph Lazaro, Yassin Abuu Napili, Elisha John, Abdallah Tamim, Ally Maumba, Kassa Mussa, Aboubakar Hassan, Aggrey Chambo na Seifdin Kabange.
Wengine waliounda timu hiyo iliyokuwa chini ya kocha Zakaria Kinanda ‘Arrigo Sacchi’ ni Razak Yusuf ‘Careca’, Juma Mgunda, Hussein Mwakuruzo na Kassim Mwajeki.
AZAM FC
Azam FC ndio waliokuwa mabingwa wa mwisho nje ya Simba na Yanga kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara wakifanya hivyo msimu wa 2013-2014 kwa rekodi ya aina yake bila kupoteza mechi wakiifikia Simba iliyoiweka msimu wa 2009-2010.
Azam iliyoasisiwa mwaka 2004 kwa jina la Mzizima FC na kupanda Ligi Kuu Bara mwaka 2007 na kuichezea msimu wa 2008-2009 ikiwa ni moja ya klabu iliyoleta mapinduzi makubwa katika soka la Tanzania kutokana na kumiliki uwanja binafsi na miundombinu mingine ya kisasa.
Tangu ilipotwaa ubingwa huo, Azam haijawahi tena kubeba licha ya mara kadhaa kumaliza ikiwa nafasi ya pili ikiwamo msimu wa 2023-2024.