Kaze anatakiwa akaze kule Kagera Sugar
Muktasari:
- Kule anatakiwa akomae vilivyo na aiongoze timu ipate matokeo mazuri ambayo yatamfanya abakie timu hiyo kwa muda mrefu na sio akae muda mfupi kama picha au video ya vyuuwansi kwenye Whatsapp.
KIJIWE leo hakitaki kupepesa maneno kwa Kocha Cedric Kaze baada ya kupewa kibarua cha kuifundisha Kagera Sugar.
Kule anatakiwa akomae vilivyo na aiongoze timu ipate matokeo mazuri ambayo yatamfanya abakie timu hiyo kwa muda mrefu na sio akae muda mfupi kama picha au video ya vyuuwansi kwenye Whatsapp.
Kitakachomfanya asiwe na presha kule Kagera Sugar ni timu hiyo kufanya vizuri na kuondoa mkosi ambao wamekutana nao wa kutoshinda mechi hadi sasa katika Ligi Kuu hadi wakawa nafasi mbaya.
Vinginevyo kinyume na hapo basi jamaa yetu hatoweza kudumu kule. Hapa Tanzania soka letu linavyoenda tunajuana. Mambo ya kuvumiliana sasa hivi hayapo tena kama zamani.
Ukiondoa kuifufua na kuinusuru Kagera Sugar kutoka nafasi mbaya ambayo ipo sasa katika Ligi, Kaze anatakiwa akaze ili asafishe sivii yake baada ya kushindwa kutamba kule Afrika Kusini alikokuwa anafundisha kabla hajaja Kagera Sugar.
Lakini hata hapa Bongo, Kaze buana hajawahi kutuonyesha makali ya huo ukocha wake akiwa katika nafasi ya Kocha Mkuu mara mbili alizowahi kuwa katika nafasi hiyo hapo nyuma.
Hakufanya vizuri alipokuwa Kocha Mkuu Yanga hadi akavunjiana mkataba na klabu hiyo na baadaye alishindwa kuonyesha umwamba alipokuwa Namungo FC hadi alipoachana nayo.
Sasa huu ni wakati muafaka kwake kutuonyesha kwamba yeye ni mtaalam hasa katika masuala ya ukocha na kilichotokea hapo nyuma kilikuwa bahati mbaya tu na upepo mzuri haukuvuma kuelekea upande wake.
Akishindwa kutoboa ndani ya Kagera Sugar, ajue wazi kuwa atawapa watu cha kusema na atajiweka kwenye wakati mgumu sana mbele ya macho ya timu za bongo.