Katwila anavyoipambania Geita Gold kurudi Ligi Kuu
Muktasari:
- Katwila amejiunga na Geita Gold kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuachana na Bigman aliyoiongoza msimu wa 2024-2025 kufuatia dili lake la kujiunga na Coastal Union ya mjini Tanga iliyomuhitaji mwanzoni mwa msimu huu kukwama.
UNAPOTAJA miongoni mwa makocha bora Tanzania ambao tunajivunia hutoacha kulitaja jina la kocha Zubery Katwila ambaye kwa sasa anaifundisha Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship akiipambania kuirejesha tena katika Ligi Kuu Bara.
Katwila amejiunga na Geita Gold kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuachana na Bigman aliyoiongoza msimu wa 2024-2025 kufuatia dili lake la kujiunga na Coastal Union ya mjini Tanga iliyomuhitaji mwanzoni mwa msimu huu kukwama.
Kocha huyo mzoefu aliyetamba na timu mbalimbali zikiwemo Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na Mtibwa Sugar alijiunga na Bigman akichukua nafasi ya Fredy Felix ‘Minziro’ aliyejiunga na Pamba ambayo kwa sasa ameachana nayo pia.
Kwa msimu wa 2024-2025 Katwila aliiwezesha Bigman kumaliza ikiwa nafasi ya nane katika Ligi ya Championship na pointi 47 baada ya kushinda mechi 12, sare 11 na kupoteza saba ikifunga mabao 29 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 21.
Ujio wa Katwila ndani ya kikosi hicho cha Geita ni ishara tosha kuwa mabosi wa timu hiyo wanataka kuirejesha tena Ligi Kuu msimu ujao baada ya msimu wa 2024-2025 chini ya kocha Mohamed Muya anayefundisha kwa sasa Coastal Union kukwama.
MTEGO WA PLAY-OFF
Moja ya jambo kubwa analopambana nalo Katwila katika kikosi hicho ni kuhakikisha timu hiyo inamaliza nafasi mbili za juu kwenye Ligi ya Championship ili kuukwepa mtego wa mechi za mchujo (play-off) kama ilivyotokea kwa msimu wa 2024-2025.
Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024 msimu wa 2024-2025 wa Championship ilimaliza ikiwa nafasi ya nne na pointi 56 chini ya aliyekuwa kocha mkuu Mohamed Muya na kushindwa kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kufeli mechi za play-off.
Timu hiyo ilicheza play-off kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya sare ya 2-2 nyumbani kisha kuchapwa ugenini 2-0.
Kwa msimu huu wa 2025-2026 Katwila ameiongoza timu hiyo katika mechi 21 ikiwa kileleni mwa msimamo na pointi 52 ikifuatiwa na Kagera Sugar inayoshika nafasi ya pili baada ya kukusanya pointi 49.
REKODI YA KIPEKEE
Geita ndiyo timu iliyopoteza mechi chache msimu huu ambapo kikosi hicho kimechapwa mara moja tu kati ya mechi 21 ikiwa ni kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi Februari 20, 2026.
Timu nyingine inayofuatia ni Kagera Sugar iliyochapwa mara mbili tu msimu huu huku Geita ikiwa pia ndiyo timu iliyoshinda mechi nyingi baada ya kushinda 16 kati ya 21 huku mechi nne zikienda sare.
Geita inashika pia nafasi ya pili kwa timu zenye safu kali ya ushambuliaji msimu huu ambapo imefunga mabao 38 ikizidiwa bao moja na Kagera Sugar iliyofunga 39 huku zote zikiruhusu nyavu zao kutikiswa mara 12.
MSIMU WA KUKUMBUKWA
Katika msimu bora na wa kukumbukwa kwa Geita Gold na wadau wa soka ni ule wa 2021-2022 ambao timu hiyo ilishika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara jambo lililoiwezesha kukata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Geita ilimaliza ya nne na pointi 46 baada ya kushinda mechi 12, sare 10 na kupoteza nane nyuma ya Azam FC iliyokuwa ya tatu na pointi 49, Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 61 na mabingwa Yanga waliokusanya pointi 74.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya Geita iliposhiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu wa 2022-2023 ilitolewa raundi ya kwanza kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Hilal Alsahil ya Sudan.
Mechi ya kwanza iliyopigwa Sudan Geita ilichapwa bao 1-0 na ziliporudiana jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Azam Complex kikosi hicho kilishinda mabao 2-1, hivyo kuwafanya Wasudani kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.
REKODI MSIMU WA MWISHO
Timu hiyo haikuwa na rekodi nzuri katika msimu wake wa mwisho wa Ligi Kuu ambao ni wa 2023-2024 jambo lililochangia kushuka daraja ingawa kwa msimu huu wa Championship Katwila ameiboresha na kuleta ushindani.
Msimu wa 2023-2024 Geita ilimaliza nafasi ya 15 na pointi 25 baada ya kushinda mechi tano, sare 10 na kupoteza 15 huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 18 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 38.
Kwa msimu huo Geita ilishuka daraja pamoja na Mtibwa Sugar iliyomaliza mkiani na pointi 21 baada ya kushinda mechi tano, sare sita na kupoteza 19 ingawa imerejea tena Ligi Kuu kufuatia kutwaa ubingwa wa Championship msimu wa 2024-2025.
MSIKIE KATWILA
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa Geita Gold, Zubery Katwila anasema licha ya mwenendo mzuri wa timu hiyo bado ana kazi kubwa ya kufanya katika mechi zilizobakia ili kufikia malengo ya kurejea Ligi Kuu.
“Ushindani kutoka kwa wapinzani wetu unatuongezea chachu ya kuendelea kupambana katika kila mechi ugumu uliopo kwa sasa ni gepu dogo la pointi lililopo kati yetu hivyo tunacheza kwa tahadhari ili kuyatimiza malengo yetu,” anasema Katwila.