Katwila alivyobeba matumaini mapya ya geita gold 2026-2027
Muktasari:
- Huu ni msimu wa tatu kwa Geita Gold kucheza Ligi Kuu Bara tangu ilipopanda rasmi daraja msimu wa 2021-2022, ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Fredy Felix ‘Minziro’ na kucheza hadi msimu wa 2022-2023, kisha kushuka 2023-2024 na kurejea 2025-2026.
BAADA ya kusota katika Ligi ya Championship kwa misimu miwili mfululizo, hatimaye Klabu ya Geita Gold tutaishuhudia tena ikicheza mechi za Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027, ikiwa ni timu iliyobeba matumaini makubwa kutokea Kanda ya Ziwa.
Huu ni msimu wa tatu kwa Geita Gold kucheza Ligi Kuu Bara tangu ilipopanda rasmi daraja msimu wa 2021-2022, ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Fredy Felix ‘Minziro’ na kucheza hadi msimu wa 2022-2023, kisha kushuka 2023-2024 na kurejea 2025-2026.
Geita Gold ndio mabingwa wa Ligi ya Championship kwa msimu wa 2025-2026, baada ya kumaliza kinara na pointi 77, kufuatia kushinda mechi 24, sare tano na kupoteza moja tu kati ya 30, iliyocheza, huku ikifunga jumla ya mabao 68 na kuruhusu 17.
Timu hiyo inayofundishwa kwa sasa na Kocha, Zubery Katwila aliyeipandisha daraja kutoka Championship hadi Ligi Kuu Bara, msimu wa 2025-2026, iliandika rekodi za kipekee, japo kwa msimu huu wa 2026-2027, itakabiliwa zaidi na ushindani mkubwa.
REKODI BORA
Rekodi bora ya Geita Gold ni ya kutopoteza mechi yoyote ya nyumbani kwa msimu wa 2025-2026, kwani timu hiyo ilicheza 15 na kati ya hizo ilishinda 12 na kutoka sare tatu, huku ikifunga mabao 42 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa pia mara tisa.
Kwa upande wa mechi za ugenini, timu hiyo ilicheza pia 15, ambapo kati ya hizo ilishinda 12, sare mbili na kupoteza moja tu, ikifunga mabao 26 na kuruhusu nane, ikikusanya pointi 38, ambazo ni moja pungufu ya nyumbani iliyokusanya pointi 39.
Geita ndio timu iliyopoteza mechi chache msimu wa 2025-2026, ambapo kikosi hicho kilichapwa mara moja, kati ya 30, ikiwa ni kichapo cha mabao 2-0, dhidi ya Polisi Tanzania, mechi iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi, Februari 20, 2026.
MSIMU WA KUKUMBUKWA
Katika msimu bora na wa kukumbukwa kwa Geita Gold na wadau wa soka, ni ule wa 2021-2022, ambao timu hiyo ilishika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, jambo lililoiwezesha kukata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Geita ilimaliza ya nne na pointi 46, baada ya kushinda mechi 12, sare 10 na kupoteza minane, nyuma ya Azam FC iliyokuwa ya tatu na pointi 49, Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 61 na mabingwa kwa msimu huo, Yanga, iliyokusanya pointi 74.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya, Geita iliposhiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu wa 2022-2023, ilitolewa raundi ya kwanza kwa faida ya bao la ugenini, baada ya sare ya kufungana mabao 2-2, dhidi ya kikosi cha Hilal Alsahil ya Sudan.
Mechi ya kwanza iliyopigwa Sudan, Geita Gold ilichapwa bao 1-0, japo, ziliporudiana jijini, Dar es Salaam, kwenye Uwanja wa Azam Complex, kikosi hicho kilishinda mabao 2-1, hivyo, kuwafanya Wasudan kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.
MSIMU WA MWISHO
Timu hiyo haikuwa na rekodi nzuri katika msimu wake wa mwisho wa Ligi Kuu ambao ni wa 2023-2024, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa kushuka daraja.
USAJILI TISHIO
Miongoni mwa vitu ambavyo mabosi wa Geita Gold wameonyesha hawataki kurudia tena makosa yaliyojitokeza msimu wa mwisho ilipocheza Ligi Kuu Bara, ni kuhakikisha inaongeza wachezaji wengine wapya wazoefu ili kuendana na ushindani uliokuwepo.
Timu hiyo imehakikisha inafanya maboresho katika kila eneo kutokana na ushindani wa Ligi Kuu Bara, ili kuendana vizuri na mahitaji yanayohitajika, ikiwemo kumsajili mfungaji bora wa Championship msimu wa 2025-2026, Mzambia Obrey Chirwa.
Chirwa aliyetamba na timu mbalimbali hapa nchini zikiwemo za, Yanga, Azam FC, Namungo FC, Ihefu iliyobadilishwa jina na kuitwa Singida Black Stars kisha KenGold, msimu wa 2025-2026, aliifungia Kagera Sugar mabao 18 na kuipandisha Ligi Kuu.
Licha ya Mzambia huyo kuipandisha Kagera Sugar daraja kutoka Championship hadi Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, ila ilishindwa kufikia makubaliano ya kumuongezea mkataba mpya, jambo lililoipa Geita nafasi ya kumsajili kuongezea nguvu.
Chirwa ameenda kuungana na mshambuliaji mwenzake, Maulid Shaban wa Geita Gold aliyefunga pia idadi sawa ya mabao 18, kwa msimu wa 2025-2026, wakienda kuunda safu tishio ya ushambuliaji, kutokana na rekodi bora walizoweka wakiwa timu tofauti.
Sajili nyingine bora kwa Geita ni kumuongeza kipa, Mnigeria Kayode Bankole Iyanu, aliyejiunga na kikosi hicho kwa msimu wa 2026-2027 wa mashindano mbalimbali, baada ya kuachana na TS Galaxy FC ya Afrika Kusini aliyocheza msimu wa 2025-2026.
Pia, imemuongeza beki wa kati anayeweza kucheza beki wa kushoto, Mganda Christopher Tebandeke aliyeachana na TRA United msimu wa 2025-2026, akiungana na mchezaji, Franck Olivier Nya Tenke aliyetokea Les Astres FC De Douala ya kwao Cameroon.
Katika eneo la kiungo, timu hiyo imefanya maboresho pia makubwa ya kumuongeza kikosini, Abdallah Kulandana aliyeachana na Mbeya City, ikionyesha kikosi hicho kimejipanga maeneo yote, ili kuhakikisha kinaleta ushindani msimu wa 2026-2027.
MSIKIE KATWILA
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Geita Gold, Zubery Katwila anasema mahitaji ya Championship ni tofauti na Ligi Kuu Bara kutokana na ushindani mkubwa uliopo, jambo lililowasukuma kuingia sokoni kusajili wachezaji wakubwa na wazoefu.
“Jambo tulilofanikiwa la kwanza ni kuhakikisha wachezaji wetu wazuri walioipandisha timu daraja tunawaongeza mikataba na baada ya hapo tukaongeza wengine wazoefu, hii imetusaidia kuwaunganisha na kutengeneza kikosi imara,” anasema Katwila.
Katwila anasema usajili uliofanyika unatokana na viongozi kutambua mahitaji yake aliyoyapendekeza, kwani malengo yao kwa sasa ni kuona timu hiyo inaendelea kufanya vizuri, baada ya kutokuwa na mwenendo bora inaposhiriki katika Ligi Kuu Bara.