KASIGA: Hii ndiyo mikakati ya gofu nchini
Muktasari:
- Ameyazungumza hayo mwenyekiti wa Tanzania Golf Union, Gilman Kasiga alipotembelewa katika ofisi zake zilizopo Kawe jijini Dar es Salaam kubadilishana mawazo na Mkuu wa Idara ya Michezo ya Mwananchi Communications Ltd, Ephrahim Bahemu.
CHAMA cha Gofu Tanzania (TGU), linaendelea na programu ya kuwanoa vijana kuanzia umri wa miaka mitano na kuendelea, lengo ni kuwaandaa wachezaji watakaofanya vizuri kwa kiwango cha kidunia.
Ameyazungumza hayo mwenyekiti wa Tanzania Golf Union, Gilman Kasiga alipotembelewa katika ofisi zake zilizopo Kawe jijini Dar es Salaam kubadilishana mawazo na Mkuu wa Idara ya Michezo ya Mwananchi Communications Ltd, Ephrahim Bahemu.
Wakiwa katika mazungumzo, Kasiga anasema Tanzania ina vipaji vya hali ya juu vinavyopatikana mitaani na mashuleni.
“Ukiachana na watoto wanaoletwa na wazazi wao katika klabu ya Lugalo Golf Club hasa wanaoishi karibu, tumeamua kwenda shuleni ambako tunawapeleka katika viwanja vya mpira, tunawaonyesha jinsi ya kupiga mipira ya gofu, wanaopenda tunawachukua na kuwaingiza katika programu ya vijana,” anasema Kasiga na kuongeza:
“Watoto waliopo katika programu za gofu ni mfano wa kuigwa mitaani kwao, wanafundishwa nidhamu, uchapakazi na umakini, kwani mchezo huo ni wa umakini na kuzingatia. Pia wamekuwa na ufaulu mzuri katika masomo.
“Tukiwaandaa katika misingi sahihi, miaka inayokuja Tanzania itatikisa duniani kwa kuwaibua mastaa wakubwa na matajiri wa kutegemewa na familia zao na jamii inayowazunguka kama ilivyo kwa mastaa wakubwa wa gofu duniani.”
Baadhi ya mastaa na matajiri wanaotajwa katika gofu kidunia ni Cameron Young (Marekani), Matt Fitzpatrick (Uingereza), Scottie Scheffler (Marekani), Jacob Bridgeman (Marekani), Collin Morikawa (Marekani), Akshay Bhatia (Marekani).
Kwa upande wa wanawake wanaotajwa kufanya vizuri zaidi kidunia na waliotwaa mataji mbalimbali makubwa ni Patty Berg ambaye alishinda mara 60 katika Ladies Professional Golf Association (LPGA), pia anatajwa kama mmoja wa waanzilishi na Mwenyekiti wa kwanza wa LPGA. Mwingine ni Mickey Wright anayejulikana kwa kutwaa mataji 13 makubwa (Major Titles), pamoja na Louise Suggs aliyeshinda mataji makubwa 11 yakiwemo Womenâ€Western Open, Titleholders Championship, US Women Open na Women PGA Championship. Hao ni baadhi tu, wapo wengi na ni mfano wa kuigwa. Ukiachana na hao, kwa Afrika baadhi yao ni Warren Abery, Thomas Aiken, Fulton Allem, Hugh Baiocchi, John Bland, Desvonde Botes, Michiel Bothma, Sid Brews, Tienie Britz na Hendrik Buhrmann kutoka Afrika Kusini, huku kutoka Zimbabwe akiwa Marc Cayeux na Tongoona Charamba.
“Tunataka watu wakiingia katika link ya gofu duniani, basi majina ya Watanzania yawe kinara. Ndiyo maana tumekuwa na programu hiyo inayochukua muda mrefu na ndiyo maana viwanja vinaendelea kujengwa ili viwe vingi, ila kwa sasa nchi nzima vinavyotumika ni 11,” anasema.
Mbali na hilo, anasema Juni mwanzoni wachezaji wa gofu wa ridhaa watakwenda kushiriki mashindano ya Zone 4 nchini Mauritius na kambi itapigwa Arusha.
“Viwanja vya Arusha vina green nzuri inayofanana na viwanja vya nje na ndiyo maana wachezaji wengi wanaotoka mkoa huo wanafanya vizuri.”
HESHIMA KWA NGULI MWANYENZA
Anamzungumzia nguli wa gofu, Salum Mwanyenza kuwa Mtanzania pekee aliyeandika rekodi ya kucheza mashindano makubwa ya The Open Championship kwenye viwanja vya Port Rush nchini Northern Ireland 1998.
“Hiyo ni rekodi ya heshima ya kipekee kuwa na Mtanzania ambaye anaheshimika katika rekodi ya vitabu vya gofu duniani,” anasema Kasiga na kuongeza:
“Mbali na hilo, alienda Sweden kwa ajili ya mashindano ya Senior na alitumiwa ujumbe na Balozi wa Tanzania nchini humo kwamba haruhusiwi kushiriki mashindano hayo kutokana na ubaguzi wa rangi kwa madai ya Watanzania hawatakiwi kushiriki mashindano yoyote ya makaburu. Bendera ya Tanzania ilikuwa imepandishwa ikabidi ishushwe na akarejea nchini kipindi cha Rais Hayati Julius Nyerere.
“Ingawa hachezi mashindano ya kiushindani, pia ni mtaalamu wa kuelekeza viwanja vya gofu vijengwaje na mchoraji wa ramani ambapo Lugalo alisaidia kuanzia kiwanja namba 1-9 na anaendelea na ujenzi wa viwanja vingine vya mikoani. Kwa heshima hiyo tumeandaa kitabu kinachohusu historia yake na tunatarajia kuzinduliwa Juni mwaka huu.”