Dakika 180 zilivyobeba hatma ya Simba, Yanga
Muktasari:
- Timu hizo zinaingia raundi ya pili zikiwa na kumbukumbu ya msimu uliopita ambapo Tanzania ilikuwa na wawakilishi wawili katika Ligi ya Mabingwa na wawili katika Kombe la Shirikisho, wote wakifika hatua ya makundi. Singida na Azam walikuwa sehemu ya timu 16 za Kombe la Shirikisho msimu uliopita huku Simba na Yanga zikifanya yao katika Ligi ya Mabingwa.
BAADA ya kuvuka kiunzi cha kwanza kwa mafanikio, wawakilishi wanne wa Tanzania Bara, Simba, Yanga, Singida Black Stars na Azam FC, sasa wamebakiwa na dakika 180 za vita ya kutafuta tiketi ya hatua ya makundi ya michuano ya CAF msimu wa 2026/27.
Timu hizo zinaingia raundi ya pili zikiwa na kumbukumbu ya msimu uliopita ambapo Tanzania ilikuwa na wawakilishi wawili katika Ligi ya Mabingwa na wawili katika Kombe la Shirikisho, wote wakifika hatua ya makundi. Singida na Azam walikuwa sehemu ya timu 16 za Kombe la Shirikisho msimu uliopita huku Simba na Yanga zikifanya yao katika Ligi ya Mabingwa.
Kwa maana hiyo, raundi hii si tu vita ya kuvuka kiunzi kingine, bali pia ni vita ya kuthibitisha kuwa mafanikio ya msimu uliopita hayakuwa kwa kubahatisha bali ni ishara ya kukua kwa soka la Tanzania. Timu hizo sasa zimebakiwa na kibarua kizito kwa sababu raundi ya pili ndiyo ya mwisho kabla ya kuingia hatua ya makundi. CAF imepanga mechi za kwanza za raundi hiyo kuchezwa kati ya Oktoba 16 na 18 huku marudiano yakichezwa Oktoba 23 hadi 25. Washindi wa jumla wataingia moja kwa moja hatua ya makundi.
Katika raundi ya kwanza, Simba ilionyesha ukubwa wake upande wa Ligi ya Mabingwa, ikiiangusha Mighty Wanderers ya Malawi kwa jumla ya mabao 7-1 huku Yanga ikitumia nguvu ya nyumbani kumaliza kazi dhidi ya Gaborone United ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-2.
Singida Black Stars, kwa upande wake, iliweka rekodi ya ushindi mkubwa zaidi miongoni mwa timu za Tanzania katika raundi hiyo baada ya kuifumua Al-Ghazala Wau ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 10-1 huku Azam ikiwa imepangwa moja kwa moja kuanzia raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kutokana na nafasi yake kwenye viwango vya CAF.
Kwa upande wa Zanzibar, KVZ na KMKM hazikuweza kuendelea na safari hiyo baada ya KVZ kutolewa na Swehly ya Libya kwa jumla ya mabao 4-0 huku KMKM ikipoteza kwa jumla ya mabao 7-0 dhidi ya Al Ahly Tripoli.
Sasa macho yote yanaelekezwa kwenye raundi ya pili, ambako kila timu ya Tanzania ina kibarua chake na kila mpinzani ana sababu yake ya kuamini anaweza kuingia hatua ya makundi.
CFFA VS YANGA ‘SAFARI YA MADAGASCAR
Katika mchezo huu, Yanga itakuwa na kibarua cha kutetea hadhi yake kama mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara na timu ambayo imekuwa ikifika mbali kwenye michuano ya Afrika katika misimu ya hivi karibuni.
Katika raundi ya kwanza, Yanga ilikutana na Gaborone United ya Botswana, ikatoka na sare ya bao 1-1 ugenini kabla ya kushinda 2-1 nyumbani na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2, lakini raundi ya pili itakutana na CFFA ya Madagascar, timu ambayo imeingia msimu huu ikiwa na taji la ubingwa wa nchi hiyo.
CFFA ilitwaa ubingwa wa Madagascar msimu wa 2025/26 baada ya kuifunga Ajesaia 2-1 kwenye fainali, ikiwa ni taji lake la pili baada ya lile la mwaka 2022. Jambo la kuifanya CFFA iwe mpinzani wa kuogopwa ni kwamba haikubeba ubingwa huo kwa bahati. Katika nusu fainali iliiondoa Elgeco Plus, mabingwa wa msimu uliopita, kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kushinda mchezo wa kwanza 2-1 na kutoka sare ya 1-1 katika marudiano.
Kocha Franck Rajaonarisamba alitajwa kuwa kocha bora wa msimu huo, wakati kipa Goly Kely alitwaa tuzo ya kipa bora na kiungo Gregas akitajwa kuwa mchezaji bora wa mash indano. Hii inaonyesha kuwa Yanga haijaangukiwa na timu ambayo ilibahatisha kufika katika michuano hiyo.
CFFA pia ilianza kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa kwa ushindi wa nyumbani wa mabao 2-0 dhidi ya Lijabatho ya Lesotho. Katika marudiano ya ugenini ililazimisha sare ya bao 1-1 na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-1. Hapo ndipo Yanga inapaswa kuwa makini.
CFFA imeonyesha katika raundi hizi mbili kuwa inaweza kucheza kwa nidhamu inapokuwa mbele, lakini pia ina uwezo wa kusimamia matokeo ugenini. Katika mchezo dhidi ya Lijabatho, iliweza kushikilia sare ya 1-1 na kulinda faida iliyotengenezwa Madagascar.
Kwa Yanga, jambo la kwanza litakuwa kuzuia mchezo usigeuke kuwa wa kusubiri dakika za mwisho. Mabingwa hao wa Tanzania wanapaswa kutafuta bao la mapema na kulazimisha CFFA kutoka kwenye mfumo wake wa kusubiri nafasi za kushambulia kwa kushtukiza.
Faida kubwa kwa Yanga ni uzoefu wa wachezaji wake katika mechi za aina hii. Tofauti na CFFA, ambayo bado inajenga jina lake katika michuano ya juu ya CAF, Yanga imekuwa ikicheza mara kwa mara dhidi ya vigogo katika michuano hiyo.
Hata hivyo, safari ya Madagascar inaweza kuwa mtego kama Yanga itaingia kwa dhana kwamba jina na ubora wake pekee vinatosha. CFFA imefika hapa ikiwa bingwa wa nchi na imeshaonyesha kuwa inaweza kushindana katika dakika 180.
15 DE AGOSTO VS SIMBA- MABINGWA WAPYA
Simba bado inasubiri kujua rasmi mpinzani wake wa raundi ya pili baada ya 15 de Agosto ya Equatorial Guinea kuweka mguu mmoja mbele dhidi ya Fomboni FC ya Comoros.
Katika mchezo wa kwanza, 15 de Agosto iliichapa Fomboni 4-0 na kuweka wazi kuwa Simba ina uwezekano mkubwa wa kukutana na mabingwa hao wa Equatorial Guinea.
Lakini 15 de Agosto si timu ya kawaida. Kwanza, ni mabingwa wapya wa Equatorial Guinea. Takwimu za RSSSF zinaonyesha kuwa klabu hiyo ilitwaa ubingwa wa ligi ya nchi hiyo mwaka 2026 baada ya kumaliza Liguilla Nacional ikiwa juu huku ikiwa pia na msimu uliokuwa na mafanikio makubwa kwenye mashindano ya ndani.
Klabu hiyo inatoka Akonibe na imekuwa ikipanda kwa kasi katika soka la Equatorial Guinea. Mwaka 2022/23 ilitwaa ubingwa wa daraja la pili na kupanda daraja, kabla ya kuwa mshindi wa pili kwenye msimu wa 2023/24 na baadaye kuendelea kujenga kikosi kilichoiwezesha kufika kileleni.
Hivyo, Simba haitakuwa inakutana na timu inayocheza michuao ya CAF kwa bahati. 15 de Agosto inaingia katika safari hii ikiwa na ari kubwa baada ya mafanikio ya ndani na muhimu zaidi, imeonyesha makali katika mchezo wake dhidi ya Fomboni.
Ushindi wa 4-0 unaipa nafasi kubwa ya kuingia raundi ya pili, lakini pia umebeba ujumbe kwa Simba kwamba wapinzani hao wanaweza kufunga mabao mengi wanapopata nafasi.
Wekundu wa Msimbazi wameonyesha katika raundi ya kwanza kwamba wanaweza kuumiza mpinzani kwa mashambulizi ya kutosha. Ushindi wa jumla wa 7-1 dhidi ya Mighty Wanderers uliwapa nafasi nzuri ya kuingia raundi ya pili wakiwa na kujiamini.
Lakini Simba haitakiwi kuingia dhidi ya 15 de Agosto kwa hesabu za raundi iliyopita. Mpinzani huyu ni bingwa wa nchi yake, ana ari ya kujithibitisha na anacheza mbele ya mashabiki wake. Simba itahitaji kuwa makini zaidi kwenye mipira ya pili, mipira iliyokufa na mashambulizi ya kustukiza.
Kama 15 de Agosto itafuzu, kibarua cha Simba kitakuwa cha tofauti na kile cha Mighty Wanderers. Hii inaweza kuwa mechi ambayo uzoefu wa Simba kwenye Ligi ya Mabingwa utakuwa silaha kubwa kulingana na nguvu ya wapinzani wao.
TUSKER VS SINGIDA - AFRIKA MASHARIKI
Singida Black Stars ndiyo imeingia raundi ya pili kibabe zaidi baada ya kuichapa Al-Ghazala Wau ya Sudan Kusini mvua ya mabao 10-1.
Lakini safari yake inayofuata imekuwa nzito zaidi kwa sababu itakutana na Tusker ya Kenya, moja ya klabu kongwe na zenye mafanikio makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Hiyo maana yake ni kwamba Singida inaingia kwenye vita dhidi ya timu yenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya ukanda na Afrika. Tusker pia imeonyesha ushindani wake katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho.
Ilikutana na Al Ahli Madani ya Sudan, ikatoka sare ya 2-2 katika mchezo wa kwanza kabla ya kushinda 1-0 katika marudiano ya Nairobi kupitia bao la Chrispine Erambo na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2.
Hapa ndipo Singida itakapohitaji kutumia silaha zake zote ili kutimiza malengo yao ya kutinhga hatua ya makundi kwa mara ya pili mfululizo.
Tusker si timu inayohitaji kushambuliwa kwa papara. Ina uzoefu wa kutosha kusubiri makosa na kutumia mazingira ya nyumbani. Kwa Singida, mchezo wa kwanza ugenini utakuwa kipimo kikubwa cha ukomavu wake wa kimataifa.
ZED VS AZAM - KIBARUA KIKUBWA
Kama kuna mchuano ambao Azam FC itahitaji umakini wa hali ya juu, basi ni huu dhidi ya ZED FC ya Misri. ZED si moja ya majina ya kihistoria kama Al Ahly au Zamalek, lakini ni klabu inayokua kwa kasi na imejenga mfumo wa maendeleo ya wachezaji ambao umevutia hata nje ya Misri.
Klabu hiyo ilianzishwa mwaka 2009 kama FC Masr na baadaye ikabadilishwa jina kuwa ZED FC baada ya kununuliwa na ZED Sports mwaka 2020.
Kinachovutia zaidi ni uwekezaji wake kwenye vijana. Akademi ya ZED imewahi kutwaa tuzo za akademi bora katika Afrika na Mashariki ya Kati huku klabu ikiwa na ushirikiano na Aston Villa, Vitaria ya Ureno na Vissel Kobe ya Japan katika mpango wa maendeleo ya vipaji.
Katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho msimu huu, ZED iliweka msingi mzuri kwa kuifunga ASAS Djibouti Telecom 4-0 nyumbani na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 5-1.
Hapo ndipo changamoto ya Azam inapoonekana. ZED ina uwezo wa kutumia uwanja wa nyumbani kujijengea faida kubwa, lakini Azam pia ina uzoefu wa kutosha katika mashindano ya CAF baada ya kushiriki hatua ya makundi msimu uliopita.
Azam inahitaji kwenda Misri bila kujaribu kushindana na ZED kwa kasi kila dakika. Itahitaji nidhamu ya kiufundi, kulinda maeneo ya hatari na kutumia kila nafasi itakayopata. Bao la ugenini, ingawa kanuni ya bao la ugenini haitumiki tena kama ‘tie-breaker’ linaweza kuwa na thamani kubwa kisaikolojia kwa sababu litabadilisha namna timu zote zitakavyocheza marudiano.