Kaseba: Mabondia wasitumike
Muktasari:
- Mkongwe huyo ni miongoni mwa mabondia wanaoishi vizuri, akisisitiza ndiyo sababu anayotamani wengi wanufaike
BONDIA mkongwe wa ngumi na mateke ‘Kick boxing’ nchini Japhet Kaseba “Champion” hatamani mchezo huo utafsiriwe kama uhuni, badala yake, anatamani kuona wanachofanya wahusika ulingoni kitafsiriwe kwenye maisha yao halisi.
Katika mahojiano baina yake na Mwanaspoti, Kaseba anatamani kuona maisha ya mabondia yanakuwa kama ilivyo kwa wanamichezo wengine na jamii itambue ngumi ni ulingoni na siyo ubabe.
Mkongwe huyo ni miongoni mwa mabondia wanaoishi vizuri, akisisitiza ndiyo sababu anayotamani wengi wanufaike
“Siwezi kusema maisha yangu ni mabaya nitakuwa nakufuru, uwekezaji wangu mkubwa ni kwa familia kwa maana ya watoto wangu kusoma vizuri na mke wangu, kumuwekea mazingira ya kujitegemea hata nikiondoka leo duniani, najua hawatayumba, ndicho ninachokitamani kifanyike kwa mabondia wengine,” anasema.
ANAKULA MATUNDA YA NGUMI
Anasema wakati anacheza alikuwa anajiandaa na maisha nje ya ulingoni, jambo linalomsaidia kwa sasa kulia kivulini na kuepukana na msongo wa mawazo unaowatesa mabondia wengi baada ya kustaafu.
Anasema alistaafu mwaka 2008, baada ya kupiga zaidi ya miaka 10, kwa sasa anawafundisha watu mbalimbali mazoezi kama familia ya Mohammed Dewji, wakati mwingine Simba Queens na mabondia:”Ni kocha wa mazoezi kuanzia watoto wadogo hadi watu wazima, wengine ni mazoezi ya afya, wengine mashindano kama mabondia na wachezaji mpira, hivyo ni miongoni mwa vitu ambavyo vinaniingizia kipato.
Anaongeza: “Ngumi kwangu zilikuwa ajira, sikuchukulia kama ubabe ili nikipita mtaani watu wawe wananiogopa, umaarufu haukunifanya iwe sehemu ya kufanya starehe za kila aina, isipokuwa ulinitengenezea koneksheni ya watu wengi ninaofanya nao kazi kwa kipindi hiki.”
Anasema ingawa alistaafu akiwa na umri wa kuendelea kucheza, akitaja sababu alikosa ushindani wa kweli, alihakikisha anaacha legasi kwa wengine kuuendeleza ngumi za mateke.
“Meneja wangu alikuwa Mjapan, alinisaidia kuhakikisha maisha yangu ya sasa yanakuwa imara zaidi, hata baada ya kustaafu alitamani niishi nchini kwao, ilishindikana kutokana na familia ilikuwa Tanzania sikuona sababu ya kuendelea kukaa nchi hiyo,” anasema na kuongeza:
“Ndani ya miaka miwili niliyokaa Japan, nilikuwa nacheza mapambano mbalimbali makubwa duniani, yalinisaidia kunikutanisha na watu tofauti na nilipata elimu kubwa ya kimaisha.”
VIONGOZI WA SASA
Anawaomba viongozi wa ngumi, kuwasaidia mabondia ili kuelewa ni namna gani wanaweza wakanufaika na vipaji vyao, ili watakapostaafu ama wakakumbana na changamoto, maisha yao yasiishie kwenye majuto.
“Mabondia wengi waliostaafu wanaishi na msongo wa mawazo, vichwa vimekuwa vya moto maana vimepigwa muda mwingi, mbaya zaidi hawana pesa, hicho ndicho sipendi kije kiwatokee mabondia ambao wanacheza, ili baadaye waje kuishi vizuri,” anasema Kaseba na kuongeza:
“Kabla sijastaafu uenyekiti wa Chama cha Mabondia wa Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBA), nilikuwa natumia pesa zangu binafsi kuendesha vikao vya mabondia, ili kuhakikisha tunapanga mikakati ya wao kunufaika na vipaji vyao.
“Sipendi mabondia wafe wakiwa maskini, wapitie changamoto ya magonjwa mfano kiharusi, wasitumike ili wengine wafanikiwe, sitamani wadhulumiwe, bali wajitambue na kuweka sawa maisha yao ya baadaye,” anasema Kaseba.
ALAMA ALIZOZIACHA
Anasema kipindi anapigana ngumi za mateke zilikuwa juu, alifanikiwa kuchukua mikanda mikubwa miwili duniani wa World Kickboxing League (WKL) na World Kickboxing Circuit (WKC).
“Mikanda ambayo ilinisaidia kuwavutia mashabiki hadi viongozi wa serikali, kwani kupitia ubingwa huo nilitangaza Tanzania, kila nchi niliyokwenda ilitajwa Tanzania na bendera yake ilikuwa inapepea” anasema Kaseba na kuongeza:
“Aina yangu ya upiganaji wa kuwavunja miguu wapinzani wangu hasa wa kutoka Ulaya, India, Philippines na nchi nyingine nyingi duniani ulikuwa unawavutia mashabiki wangu kuja kunitazama pindi nilipokuwa na pambano.
“Haikuwaishia hivyo kuna nchi zilikuwa zinanialika kwenda kuwapandisha viwango mabondia wao kama Kenya mmojawapo alikuwa Alphonce Kakaa na Uganda ni Golola Moses, nisingeweza kupewa fursa hiyo endapo ningekuwa nacheza chini ya kiwango,” anasema bondia huyo.
Kaseba muasisi wa mchezo huo anasema kwa hapa Tanzania amewatengeneza “Captain Kabongo na Pendo Njau, Jesca Mfinanga, Feriche Mashauri, Boyka, Imani, Mohamed Alkaida, Kanda Kabongo, Emanuel Shija, Mrisho Dame.
Anaongeza: “Ingawa wengine sikuwafundisha moja kwa moja bondia kama Hassan Mwakinyo nilikuwa namshauri, timu ya taifa ya ngumi ilikuwa inakuja gym yangu kufanya mazoezi na nilikuwa najitoa kuwafundisha mabondia, ukiacha hivyo hadi sasa nakwenda gym mbalimbali kutoa sapoti.”
SABABU YA KUOKOKA
“Tukio la kuzimia ulingoni baada ya kumaliza pambano langu la roundi 10 baada ya kumshinda mpinzani wangu Master Yusufu Mzaire Bingwa wa Congo, sitakuja kulisahau kwenye maisha yangu yote na lilisababisha nimrudie Mungu wangu;
“Huo kwangu ni ushuhuda mkubwa sana, nilijihisi kifo, kilichosababisha nilizoea kupigana raundi moja hadi tatu, lakini pambano lile lilikuwa la raundi 10, kwanza nilikuwa na mwili mnene hivyo upepo ulijaa kifuani.”
Anasema tangu kipindi hicho akaamua kuokoka na anasali kanisa la Akuzamu na kwamba isingekuwa mchezo huo angekuwa mtumishi wa Mungu kwa kuhubiri injili.
“Ningekuwa mhubiri wa neno la Mungu kwani ndiyo kitu nilichokuwa nakipenda zaidi, huku kwenye ngumi niliingia kutafuta maisha, ila tukio la kuzimia likanirusha rasmi kwa Mungu, maana maisha yetu ni mafupi sana,” anasema.
Anasema kwenye michezo kuna wakati mwingine watu wanawekeana roho mbaya ili mradi tu kupigania vitu ambavyo kila mmoja ataviacha duniani na vinapita. “Kila mtu ana kipaji chake ambacho Mungu amempatia, hakuna haja ya kuweana roho mbaya na siyo vyema kufurahia mateso ya mtu huo ni udhaifu.”
NINI KIFANYIKE
Kasema anaseshauri kwamba, “ngumi kwa sasa zimekosa msisimko ni duniani kote, tofauti na zamani nadhani inatokana na mifumo hasa ya kirekodi, wengi wao wanaokuwa wanashinda kuna namna wanakuwa wanatengenezewa mazingira, tofauti na kipindi chetu, vipaji vilikuwa ni halisi.
“Kwa Tanzania tunawahitaji wawekezaji wa kweli, ambao watakuwa na moyo wa kuupenda mchezo huo, hapo mabondia watapiga hatua ya kimaisha pia wanaowasimamia mabondia wasitangulize maslahi yao, wakiwafanyia vibaya watoto wa wengine na wao pia watakutana na mtihani huo kwa watoto wao, ndiyo maana sipendi dhuluma.”