Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nje ya ulingo haya ndo maisha yao

NGUMI Pict

Muktasari:

  • Tofauti na ilivyo kwa baadhi ya wanasoka wenye mishahara ya kila mwezi au posho baadhi ya mabondia Tanzania hawategemei moja kwa moja kazi hiyo, wengine hujishughulisha na fani zingine na baadhi huwa wanafanya kazi ili kujiiingizia kipato cha kila siku.

MASHABIKI huwafahamu kwa ngumi kali, KO na mikanda wanayobeba, lakini wachache wanajua maisha yao yanapoisha kelele za ulingoni. Wakati wengine wakidhani mabondia husubiri pambano linalofuata, ukweli ni kwamba wengi wao wamejenga vyanzo vingine vya mapato ili kuendesha maisha yao.

Tofauti na ilivyo kwa baadhi ya wanasoka wenye mishahara ya kila mwezi au posho baadhi ya mabondia Tanzania hawategemei moja kwa moja kazi hiyo, wengine hujishughulisha na fani zingine na baadhi huwa wanafanya kazi ili kujiiingizia kipato cha kila siku.

Ndiyo maana baadhi yao wakipata mapambano yenye pesa ndefu huamua kuwekeza kwenye kilimo, biashara, muziki, ucheshi na hata kufundisha mazoezi ili kujiingizia kipato.

Mwanaspoti limekuchambulia baadhi ya mabondia ambao wamewekeza pesa zao nje ya ngumi au wengine wamejiajiri na kuajiriwa kupitia fani mbalimbali.

NGUM 04

MWAKINYO

Akiwa na rekodi ya mapambano 28 ya kulipwa, ushindi 25 ukiwemo 18 wa KO na kupoteza mara tatu pekee, Hassan Mwakinyo ni miongoni mwa mabondia wenye rekodi bora zaidi kuwahi kutokea Tanzania, huku umaarufu wake ukitokana na ushindi wa kihistoria dhidi ya Sam Eggington nchini England

Mwakinyo ni miongoni mwa mabondia wanaoamini katika uwekezaji wa vitu mbalimbali.

Katika mahojiano mbalimbali, Mwakinyo amekuwa akieleza kuwa nje ya ngumi ameamua kuwekeza kwenye kilimo na ufugaji nyumbani kwao Tanga. Kwake, kilimo ni uwekezaji wa maisha baada ya ulingo.

Hilo linaonyesha kuwa hata mabondia wanaofanya  makubwa wanaelewa kuwa maisha ya mwanamichezo yana mwisho, hivyo ni muhimu kuwa na chanzo kingine cha kipato.

NGUM 03

KIDUKU

Kwa upande wa Twaha Kiduku, simulizi yake iko tofauti kidogo.Kabla hajawa bondia maarufu nchini, Kiduku alikuwa akiigiza, kupiga ngoma za asili, kuwa DJ na hata kufanya muziki wa Singeli kipindi cha Msagasumu.

Anasema bado hajafunga mlango wa sanaa kwani akipata nafasi anaweza kushiriki kazi mbalimbali za muziki na maonyesho.

“Mimi nilianza kuigiza kabla ya kuanza kupigana. Mbali na kuigiza pia nilikuwa mpiga ngoma za asili, Dj, msanii wa muziki wa singeli kipindi cha Msagasumu. Wakitokea waandaaji wakitaka nishiriki nipo tayari na naendelea kufanya hivyo. Hivi karibuni kuna msanii alinifuata nifanye naye kazi, nilifanya hivyo (ngoma) ipo YouTube inaonyeshwa huko,” anasema.

Kwa mujibu wa BoxRec, Twaha Kiduku ana rekodi ya mapambano 37 ya kulipwa, akishinda 26 kati yake huku 10 ikiwa ni kwa KO. Amepoteza mara 10 na ni pambano moja pekee alidundwa kwa KO, huku akiwa na sare moja, takwimu zinazomweka miongoni mwa mabondia wenye uzoefu mkubwa nchini.

NGUM 08

MKALI WENU

Licha ya kujizolea umaarufu kupitia vichekesho na mitandao ya kijamii, Mkali Wenu ameanza kutengeneza jina pia kwenye ngumi za kulipwa. Kwa mujibu wa BoxRec, tayari amepigana mapambano manne na kushinda yote, mawili kati ya hayo kwa KO/TKO na mawili kwa uamuzi wa majaji, rekodi inayomfanya kuwa mmoja wa mabondia wanaokuwa kwa kasi akiwa hajapoteza pambano lolote katika taaluma yake ya ngumi za kulipwa tangu aanze kupigana mwaka 2024.

Mbali na ndondi ambazo ameanza miaka miwili nyuma lakini Mkali wenu ana kipaji kingine cha kuwaandikia wasanii nyimbo miongoni mwa mastaa aliowaandikia ni Marioo, Juma Jux, Billnas na wengineo.

"Sina maana nimeacha uchekeshaji, nafanya vyote ila katika uchekeshaji unaweza ukawa unapata Sh200,000 kwa mfano kila siku, hiyo haitoshi pekee napaswa kupambana, Nagawa muda wangu kwa kuamka saa 11:00 alfajiri kila siku nafanya mazoezi hadi saa 3:00 asubuhi, napata muda wa kupumzika kisha naanza kushuti, kuediti na kuzipandisha video zangu."

NGUM 07

JESCA MFINANGA

Bondia huyo ambaye ni binti wa mwamuzi, Pendo Njau anasema mbali na ngumi anafanya biashara ndogondogo pamoja na kuwafanyisha mazoezi wazungu na wahindi.

“Napenda kujitegemea. Sitaki kutegemea ngumi pekee. Nafanya biashara ndogondogo na pia nafundisha watu mazoezi ya kupunguza uzito na vitambi,” anasema na kuongeza kuwa, wanawake wengi humtafuta kwa ajili ya mazoezi ya kupunguza uzito, kuondoa nyama uzembe na kujenga maumbo yao.

Jesca mwenye umri wa miaka 26, anayepigana uzani wa super flyweight (kilo 52), anasema bondia anapaswa kujiwekeza kwenye kazi zingine kwa sababu kazi yao haina pesa ya kutosha ya kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

NGUM 02

MWENGA

Bondia chipukizi kutoka Cholila Boxing Gym, Abdulrazack Mwenga anasema anacheza ngumi kwa sababu ni kitu alichokuwa anakipenda kufanya tangu utoto ingawa hategemei pesa ya mchezo huo kwani huwa wanapigana mara tatu hadi nne kwa mwaka.

Bondia huyo, ambaye kwa sasa anatumikia adhabu ya kutoshiriki ngumi kwa mwaka mmoja baada ya kufanya vurugu ulingoni, amekuwa akifanya kazi ya gereji kama sehemu ya kujipatia kipato.

“Mfano unaweza kulipwa 120,000 pambano moja hilo hapo hapo ugawane pesa na kocha wako kwa hiyo kiufupi huwezi kutegemea ngumi labda uwe bondia mkubwa ambaye ukipigana mapambano makubwa matatu tu unakaa mwaka mzima hufanyi kazi ila kwa sisi ni ngumu ndio maana tunapambana na fani nyingine.”

Mwenga ni bondia wa kulipwa nchini Tanzania mwenye rekodi ya mapambano 13, ingawa ni 10 pekee yaliyopo kwenye rekodi rasmi za BoxRec. Katika rekodi hizo 10, ameshinda mapambano matatu (mawili kwa KO), amepoteza manne, na ametoa sare mara tatu.

Kwa nchini Tanzania, anashika nafasi ya 23 kati ya mabondia 1,115, huku duniani akijitafuta katika nafasi ya 812 jambo ambalo anaamini kama atarudi kwenye ubora alioanza nao anaweza kuzivunja na kuandika rekodi kubwa.

NGUM 05

DEBORA MWENDA

Debora Mwenda ni miongoni mwa mabondia wa kike wanaojitengenezea jina nchini kutokana na kipaji chake kikubwa cha kupigana na muonekano wake ambao umekuwa ukiwavutia mashabiki mbalimbali nchini.

Mrembo huyo anasema nje ya ngumi amejiwekeza kwenye biashara ya nguo hususani zile za michezo “Huwa nauza nguo za michezo za aina tofauti kuanzia soka na vinginevyo.”

Kwa sasa, Debora anashika nafasi ya pili nchini katika uzani wa kilo 57.15 (57.2 kg) na nafasi ya 91 duniani kulingana na rekodi za BoxRec. Tangu alipoingia katika ngumi za kulipwa mwaka 2022, tayari amepigana mapambano sita, akishinda matatu, kutoka sare moja na kupoteza mawili.

NGUM 01

JAPHET KASEBA

Aliyekuwa bingwa wa dunia wa Kick Boxing na sasa Mwenyekiti wa Chama cha Mabondia wa Kulipwa Tanzania (TPBA), Japhet Kaseba ni miongoni mwa mastaa walijiwekeza kwenye vitu mbalimbali nje ya ngumi .

Kaseba anamiliki gym yake yenye vijana tofauti anaowasimamia, nje ya gym mkali huyo anawafundisha mazoezi ya kupunguza mwili na kujenga afya viongozi na wafanyabiashara kwa kuwafuata majumbani mwao.

“Huwa tunaelewana bei kwa hiyo kila mmoja namfundisha mazoezi kwa kuelewana bei huwa sifanyi bei moja,” anasema Kaseba ambaye hivi karibuni alisema anatamani  kuwa mhubiri mkubwa, kuhakikisha anawafikia wana michezo ili waweze kumjua Mungu.

Uzoefu alioupata akiwa bondia umegeuka kuwa taaluma inayomwingizia kipato hata nje ya mashindano.

Hili  linaonyesha kuwa ngumi peke yake haziwezi kuwa tegemeo la maisha ya muda mrefu. Mabondia wengi wamegundua umuhimu wa kuwa na shughuli nyingine zinazowaingizia kipato.