Prime
Chanzo cha majeraha, vifo vya mabondia chafichuka -1
Muktasari:
- Miongoni mwa hiyo ni katika familia ya nyota wa zamani wa ngumi, Rashid Matumla ‘Snakeboy’. Licha ya jina kubwa alilonalo ndani na nje ya nchi, anasema hana furaha kwa anayopitia maishani yaliyotokana na mchezo wa ngumi.
IPO mikasa inayoonyesha athari kubwa ya mabondia kushindwa gharama za vipimo kama MRI/CT Scan, ilivyoleta hatari kwa baadhi yao; wapo waliopata ulemavu, ugonjwa wa kudumu na miongoni mwao vifo.
Miongoni mwa hiyo ni katika familia ya nyota wa zamani wa ngumi, Rashid Matumla ‘Snakeboy’. Licha ya jina kubwa alilonalo ndani na nje ya nchi, anasema hana furaha kwa anayopitia maishani yaliyotokana na mchezo wa ngumi.
Katika mahojiano na Mwananchi, Matumla anasimulia kilichomkuta kijana wake wa kwanza, Mohammed Matumla ‘Snakeboy Jr’ aliyepata ulemavu wa kudumu kichwani uliozima ndoto zake za kuwa bondia mashuhuri.
Hayo yakibainishwa, Kanuni za Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) za mwaka 2024, zinasisitiza umuhimu wa kila bondia kupima kabla na baada ya pambano, lakini hakuna ulazima wa kipimo cha MRI/CT Scan.
Kanuni 4.1.2 inasema siku 14 kabla ya kushiriki pambano lolote la ngumi za kulipwa bondia atawajibika kupimwa afya yake na daktari mwenye leseni ya kamisheni na anayetambulika na Chama cha Madaktari wa tiba za michezo (TASMA).
Kutokana na majibu ya vipimo daktari atashauri iwapo bondia husika anaweza au hawezi kushiriki pambano.
Kanuni za kimataifa za ngumi zinahitaji mabondia kufanyiwa uchunguzi wa afya, huku MRI au CT Scan ya ubongo ikihitajika katika mazingira maalumu au kwa vipindi vinavyowekwa na shirikisho au mamlaka husika; si lazima kabla ya kila pambano.
Mfano, Shirikisho la Kimataifa la Ngumi (IBA), lililokuwa likijulikana awali kama AIBA katika kanuni zake zilizoboreshwa MRI/CT Scan inapendekezwa kabla ya kushiriki mashindano makubwa kama mashindano ya dunia. Pia bondia akipigwa KO au TKO vipimo hivyo vitahitajika.
SIMULIZI YA MATUMLA
Kwa sauti yenye kuashiria uchungu anasema: “Sina furaha ya maisha, niliwekeza nguvu kwa kijana wangu ili aje kuwa bondia atakayechukua mataji ndani na nje ya nchi, kama ilivyo kwa wanasoka mfano marehemu Ally Pazi Samatta, kijana wake Mbwana Samatta bado analiendeleza jina la mzee wake kwa kufanya makubwa katika soka.”
Anasimulia: “Mwaka 2017 kabla ya pambano la kijana wangu Mohamed na Mfaume Mfaume alikuwa kama amechizika, baada ya kufuatilia niliambiwa alipigwa rungu la kichwa na askari mmoja, akatumia dawa akawa anaendelea vizuri, tukaanza mazoezi ya maandalizi ya pambano lake.”
“Kabla ya pambano alipima vipimo vya kawaida kama HIV, macho, malaria na vingine isipokuwa MRI au CT Scan. Siku ya pambano alipanda ulingoni, akapigana raundi kadha kisha akadondoka chini, damu zilikuwa zinamtoka puani akapelekwa hospitali na kuwekwa ICU, baadaye walipomfanyia kipimo cha CT Scan kilionyesha alikuwa na jeraha nyuma ya kichwa, hivyo alipopigwa panchi ni kama alitonesha kidonda,” anasimulia na kuongeza:
“Tatizo lililogundulika ni kuwa, damu ilikuwa inavujia kwenye ubongo, hivyo akafanyiwa upasuaji wa kichwa. Kutokana na changamoto hiyo madaktari walituambia atameza dawa maisha yake yote na asicheze ngumi tena.”
Matumla anasema: “Hana bima na dawa zake anazichukulia Hospitali ya Taifa Muhimbili, kwa mwezi inagharimu siyo chini ya Sh50,000. Anapozikosa kuna changamoto anapitia, kwani madaktari walisisitiza uimara wa afya yake ya kichwa ni dawa kila siku.”
Si kijana wake pekee, anasema yeye anatakiwa kutumia dawa maisha yake yote kutokana na kusumbuliwa na mgongo, huku akitamani kupata mdhamini ili akapime kichwa kwani huhisi maumivu kila mara.
“Kuna mtu alinikatia bima ya mwaka mmoja iliyoisha muda wake 2025, iligharimu Sh1.5 milioni. Dawa zangu kwa mwezi siyo chini ya Sh50,000. Akitokea mtu akatukatia bima mimi na kijana wangu atakuwa ametusaidia pakubwa,” anasema na kuongeza:
“Mabondia wengi wa zamani tuna changamoto ya mikono, vichwa, mabega na migongo zilizotokana na kufanya mazoezi makali.”
Hata hivyo, anasema uwazi wake haumaanishi kuwakatisha tamaa vijana kuingia katika mchezo wa ngumi, bali anaonyesha hali halisi ya changamoto zilizopo, ambazo iwapo Serikali ikiweka mkono wake zitapungua.
Vilevile, amewataka mameneja wa mabondia kuhakikisha wanasimamia vipimo ili kuokoa maisha yao.
“Wakati kijana wangu amepata changamoto, meneja wake alisimama na sisi bega kwa bega hadi alipotoka hospitali. Mimi pia ni kocha wa mabondia, huwa nawasisitiza kuhusu afya maana ndiyo mtaji mkubwa wa maisha yao ili yaliyomtokea kijana wangu yasitokee kwao,” anasema.
GHARAMA KUBWA
Katibu wa Chama cha Mabondia wa Kulipwa Tanzania (TPBA), Salum Mgeni ambaye pia ni bondia anayepigana uzani wa kilo 63-66 anakiri ni miongoni mwa wasiopima vipimo hivyo, akitaja changamoto ni gharama kubwa.
“Japokuwa kuna kanuni inayosimamia afya za mabondia, mara nyingi kwa mapambano ya hapa nchini inategemea ni ya aina gani, ingawa vipimo vinavyopimwa mara kwa mara ni HIV, sukari, malaria, macho, ini na mimba kwa wanawake,” anasema na kuongeza:
“Wapo baadhi ya mabondia wanaojiweza kupima MRI/CT Scan, ingawa na wenyewe ni kwa mapambano maalumu. Mfano bondia anapigana na mtu kutoka nje au anakwenda kupigana nje, lazima atafanya vipimo hivyo.”
Kutokana na umuhimu wa vipimo hivyo, anasema waliomba bima za afya kwa ajili ya mabondia TPBRC. Hata hivyo, anasema bado halijafanyiwa kazi na anatambua hata wakipata itakuwa ngumu bima kumudu vipimo hivyo, isipokuwa itasaidia magonjwa ya kawaida.
“Tunaiomba Serikali itusaidie hospitali itakayotoa dhamana ya kutupunguzia gharama ya vipimo hivyo, angalau iwe Sh250,000 kwani madhara yapo, kuna mabondia wenzetu ambao wamepoteza maisha, wengine wamepata ulemavu wa kudumu,” anasema Mgeni na kuongeza:
“Kuna bondia ilibidi tujichange kama chama akapima CT Scan, ingawa aligundulika ana shida ya mgongo, wengine wamestaafishwa, huku baadhi wakiendelea na matibabu kwa kuhudhuria kliniki kama wanavyoambiwa na madaktari.”
Anawataja mabondia waliopoteza maisha ni Hassan Mgaya aliyefariki Desemba 29, 2024 katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam baada ya kupigwa TKO na mpinzani wake Paulo Elias.
Aprili 23, 2023, Ibrahim Najim baada ya kumaliza pambano la raundi nne alidondoka na kuwahishwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na akafariki dunia. Kipimo kilionyesha alikuwa na jeraha la muda mrefu kichwani.
Mbali ya hao, Abbasi Mselem alipopigwa Novemba 30, 2024 alipoteza fahamu ulingoni, kisha akafariki dunia Desemba 1, 2024.
“Siyo kila kifo cha bondia kinatokana na kipigo cha KO, wengine wanashindwa kwa pointi lakini bado wanadondoka ulingoni, hivyo siyo kila anayepata changamoto inatokana na panchi kali, isipokuwa wanakuwa na majeraha ya nyuma na kwa kuwa hawakupima akipigwa ni kama wanatonesha,” anasema.
Bondia wa zamani wa ngumi na mateke ‘Kick boxing’ Japhet Kaseba ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Mabondia wa Kulipwa Tanzania (TPBA), anakiri kuwapo tatizo la baadhi ya mabondia kupigana kiholela bila kuzingatia baadhi ya vipimo, jambo analosisitiza ni hatari kwa usalama wa maisha yao.
“Siwezi kulaumu moja kwa moja viongozi kushindwa kusimamia kanuni za afya za mabondia, kwani wapo wanaofeki vyeti vya vipimo kwa tamaa za pesa ndogo na kugharimu maisha yao,” anasema.
“Nitoe mfano wa pambano langu la mwisho kupigana ulingoni ingawa sikumbuki mwaka kwa sababu ni muda mrefu umepita. Lilikuwa la raundi 10 dhidi ya Master Yusufu Mzaire Bingwa wa Congo, japokuwa nilishinda lakini nilizimia ulingoni, nilihisi kufa, ndiyo ulikuwa mwisho na kuachana na ngumi za ushindani na kutokana na tukio hilo nikaokoka,” anasema.
Kaseba anasema: “Baada ya kupima CT Scan madaktari waligundua nilipunguza kilo nyingi kutoka 88 hadi 68, hivyo mwili wangu ulikuwa haujajengeka vizuri, ningepigana na Mmarekani ningefia ulingoni. Mbali na hilo nina changamoto nyingine ya kusahausahau vitu inayotokana na ngumi nilizopigana kwa muda mrefu.”
Anaiomba Serikali iwasaidie mabondia kupata bima za afya na iwapunguzie gharama za vipimo vikubwa jambo analoamini litaongeza chachu ya kupenda kupima afya zao mara kwa mara.
SHUHUDA ZA MABONDIA
Bondia wa kike, Jesca Mfinanga anayepigana uzani wa kilo 50 hadi 52 kwa zaidi ya miaka mitano, anakiri hajawahi kupima MRI au CT Scan kutokana na gharama.
“Majeraha kwa bondia anaweza akapata wakati wa mazoezi yanayofanyika kwa miezi mitatu kabla ya pambano, bila kujua ukubwa wa jeraha iwe kichwani, mgongoni au mabegani na akaendelea kumeza dawa za maumivu, akija kukutana na panchi inaweza ikamsababishia ulemavu au kifo,” anasema na kuongeza:
“Siyo kila bondia anayeanguka ulingoni amekutana na panchi kali wakati wa pambano, wengine inakuwa ni kutonesha jeraha la muda mrefu na ni kitu kibaya kuishi kwa mazoea kwa kumwangalia mtu usoni na kumuona yupo sawa, ukweli vipimo hivyo ni muhimu tunaomba udhamini ili kuokoa afya zetu.
Bondia Miraji Supakila ‘Mkali Wenu’ anayepigana uzani wa kilo 66 hadi 69, anakiri suala la mabondia kupima vipimo hivyo ni gumu kutokana na gharama kuwa juu.
“Kuna haja mabondia kupewa elimu ya mara kwa mara ya afya za miili yao, kitendo cha kupigwa akameza panadol na kuendelea na shughuli nyingine ni hatari, mfano mtu akipata Sh3 milioni anaona bora akanunue kiwanja asije akafa hana nyumba, hiyo yote ni kwa sababu ya umaskini,” anasema.
Bondia maarufu nchini, Ibrahim Class anasema ni muhimu mabondia kupima vipimo hivyo ila changamoto ni gharama hasa kwa wale ambao wana kipato cha chini cha kutafuta pesa ya chakula na kodi.
“Nimepata udhamini wa Hospitali ya Royal Polyclinic hivyo napima mara kwa mara, kwani najali afya yangu kwa sababu mchezo wa ngumi ni hatari, bila uchunguzi wa afya mtu anaweza akapoteza maisha,” anasema.
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Mfaume Mfaume anasema mara ya mwisho kupima MRI ni Januari 2025 na ilibainika kuwa ana changamoto ya bega akafanyiwa upasuaji.
“Binafsi nazingatia kupima kwani ngumi ni mchezo hatari, niliona bega langu linafyatuka mara kwa mara, nikaanza na kipimo cha x-ray kisha MRI baada ya upasuaji nikazingatia muda nilioambiwa na daktari nipumzike. Baada ya kupona, Julai nilicheza pambano na Mmalawi nikashinda kwa pointi, ingawa nilikuwa na wasiwasi kabla ya kupanda ulingoni,” anasema.
“Mwaka 2017 nilimpiga kwa KO Mohamed ‘Snakeboy Jr’, lilikuwa ni pambano la raundi nane, panchi niliyompiga akapasuka kichwa na kuwahishwa hospitali akawekwa ICU baadaye akafanyiwa upasuaji wa kichwa, baada ya vipimo madaktari walimstaafisha, siyo kwamba naona ni kitu kizuri, bali najaribu kuonyesha ukubwa wa tatizo na hali halisi ilivyo,” anasema na kuongeza:
“Tukio lingine nililowahi kulishuhudia lilikuwa la mdogo wangu Mgaya alidondoka wakati anapigana katika ukumbi wa Manyara uliopo Manzese, kisha akafia hospitali ya Mwananyamala, iliniuma sana, matukio yapo mengi ni vile watu wamenyamaza, laiti kungekuwa na nafuu ya vipimo ingeokoa maisha ya wengi.”
Bondia wa kulipwa nchini, Twaha Kassim ‘Kiduku’ anasema japokuwa ana kawaida ya kupima vipimo vikubwa, haiondoi ukweli wa mabondia wengine kushindwa kumudu gharama.
“MRI na CT Scan ni vipimo muhimu lakini tatizo ni hali halisi ya kiuchumi. Bondia hajui ale nini, hajui atalipaje kodi, wakati mwingine ana familia anajitosa kupigana ili familia yake ipate chochote kitu,” anasema.
Bondia kutoka Tanga, Said Mundi ‘Kiboko ya Wabishi’ anayepigana uzani wa kilo 69, anasema tangu aanze kucheza ngumi za kulipwa mwaka 2011 amepima MRI mara tatu, ya kwanza ni mwaka 2016 wakati anakwenda Uingereza.
MTINDO WA MAISHA
Bondia mwingine mwanamume aliyeficha jina lake, anaeleza historia tofauti ya maisha yao kabla hawajaingia katika ngumi inachangia baadhi yao kuanguka ulingoni, kupoteza maisha na kupata ulemavu.
Anasema baadhi walikuwa wakijihusisha na uhalifu na huko walipata vipigo, hivyo wanapoingia kwenye ngumi pasipo kufanya vipimo wanapopata madhara baadaye hubainika kuwa na majeraha ya nyuma.
Vilevile anazungumzia ulingo wa ngumi, akieleza ipo ambayo haikidhi viwango na inapotokea bondia kaangukia kichwa ni rahisi kupata majeraha kichwani.
Pia, anasema baadhi yao huamini ushirikina hawafanyi mazoezi inavyotakiwa, hivyo akipigwa panchi ya nguvu ni rahisi kupata jeraha la kichwa.
MTAZAMO WA MAKOCHA, PROMOTA
Kocha Said Jeba kutoka Tanga, anasema bondia anapaswa kupima kabla ya kwenda kunolewa, tofauti na hapo ni hatari.
Kocha wa gym ya Kaseba Champion, Kanda Kabongo ambaye pia ni bondia, anakiri kuwapo kwa changamoto zinazotokana na mabondia kutokupima vipimo hivyo. “Mimi nimepata athari ya macho, ninapata shida kuandika ujumbe katika simu, nasikia maumivu kuanzia kiunoni hadi mguuni, pia goti la mguu wa kushoto lilipata changamoto na niliyajua hayo baada ya kupima,” anasema.
Promota na meneja wa mabondia kutoka kampuni ya Fayheroes Sports Promotion, Abdul Salum, anasema vipimo ni muhimu hata hivyo, anaeleza kuwa changamoto ni gharama ambazo baadhi ya mabondia hawazimudu.