Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kamati ya leseni za klabu yenyewe haina leseni

PUMZI Pict

Muktasari:

  • Hayo yanakuja baada ya mechi ya wenyeji TRA United (zamani Tabora United) dhidi ya Dodoma Jiji, uliofanyika Jumamosi, Septemba 20.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), imetangaza kuufungia kwa muda usiojulikana Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi uliopo mjini Tabora kutokana na kutokidhi vigezo.

Hayo yanakuja baada ya mechi ya wenyeji TRA United (zamani Tabora United) dhidi ya Dodoma Jiji, uliofanyika Jumamosi, Septemba 20.

Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kufanyika uwanjani hapo tangu Mei 14, 2025 wakati Tabora United walipowakaribisha KMC.

Hizo ni jumla ya siku 129  zimepita na hakukuwa na mechi, lakini msimu unaanza tu uwanja unafungiwa.

Unaweza kuwalaumu wenyeji TRA United, unaweza kukilaumu Chama cha Soka Mkoa wa Tabora, Serikali ya au chama tawala - CCM ambao ndio wamiliki wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.

Lakini, mimi nadhani hao hawana makosa hata kidogo. Mwenye kosa hapa ni Kamati ya Leseni za Klabu ya TFF.

PUM 01

Kamati hiyo ndio inayokagua viwanja na kuvithibitisha kwamba vimekidhi vigezo.

Iweje uwanja uliokidhi vigezo hadi Septemba 19 ukawa haujakidhi Septemba 20 na hakukuwa na mechi hapo kwa siku 129?

Hii kamati ya leseni kwanza yenyewe ina leseni kweli? Inatumia vigezo gani kupitisha viwanja na je yenyewe ina vigezo?

Sheria za soka Tanzania kwa sasa zinataka kocha wa kufundisha Ligi Kuu Bara awe na vigezo vya kufundisha Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yaani awe na elimu isiyopungua Diploma A ya CAF.Awe na leseni A.

Kama kocha anatakiwa kuwa na vigezo vya Ligi ya Mabingwa kwanini viwanja visiwe na vigezo hivyo pia?

Yaani kocha mwenye hadhi ya kufundisha Ligi ya Mabingwa anatumiaje viwanja vya ndondo?

PUM 02

Ukiangalia viwanja vyetu asilimia kubwa havina sifa ya kutumika kwenye Ligi ya Mabingwa.

Sasa kwanini tunakuwa na vigezo nusu nusu? Kama tumeamua kuchukua makocha wa hadhi ya juu, basi tuwawekee na mazingira ya hali ya juu pia.

Ligi Kuu Bara ni namba nne kwa ubora Afrika, lakini miundombinu haipo hata katika 10 bora.

Na shida iliyopo kwenye hili ni hii kamati. Inaruhusu viwanja kutumika ilhali hata macho yasiyo ya kitaalamu yanaona kwamba uwanja haufai.

PUM 03

Na hapo sio tu sehemu ya kuchezea, huku kwa mashabiki ndio balaa.

Nenda Uwanja wa Sokoine Mbeya majukwaani hakuna mabadiliko. Michirizi ya maji ya chemchemi ni kawa uwanjani pale.

Vyoo vya mashabiki ndio hatari, na hii ni hadi VIP.

Huwa wanaweka kipande kidogo cha pipa la maji ambayo huisha hata kabla ya mapumziko.

Baada ya hapo hakuna maji uchafu juu ya uchafu.

Halafu mwisho wa mwezi meneja anashinda tuzo ya meneja bora...unashangaa.

Uwanja wa Sokoine sio tu haustahili kutoa meneja bora, bali haustahili kutumika.

PUM 04

Tatizo ni kamati ya leseni. Nadhani kuna kitu zaidi ya uwajibikaji yawezekana kuna kitu nyuma ya pazia katika hili.

TFF inafanya kila kitu kukuza mpira wetu, lakini kuna watu hawawajibiki ipasavyo ikiwemo hii kamati.

Wito kwa rais Wallace Karia pitia upya hii kamati ina shida. Ligi yetu inatiwa doa kubwa na viwanja vyetu.

Timu zinajitahidi kuleta wachezaji bora kutoka nje waje wainue kiwango cha mpira wetu, lakini ubovu wa viwanja vyetu unapunguza ubora wao.

Ligi bora ni pamoja na miundombinu bora. Futa leseni za viwanja vyote vya hovyo vibaki viwanja vichache. Watu wanafanya makusudi kutoimarisha viwanja kwa sababu wanajua vigezo vya kamati ni vya chini sana.

Tuwape sifa zao JKT Tanzania kwa kutoa darasa kwa wamiliki wa viwanja, hasa vya nyasi asilia.

PUM 05

Vile ndivyo uwanja unapaswa kuwa. Kama kamati imeshindwa kutoa somo kwa wamiliki wa viwanja wawaambie tu waende pale Meja Jenerali Isamuhyo wakajifunze. Uwanja wa Tanzanite Kwaraa ulikuwa bora sana msimu uliopita. Bila shaka utakuwa bora tena msimu huu. Na hivi viwanja ni bora kwa sababu ya jitihada za wamiliki wala sio vigezo vya kamati.

Kwa sababu ulinganishaji viwanja hivi na vingine vilivyoruhusiwa kwa vigezo vya kamati ni mbingu na ardhi.

Cha ajabu ni kwamba kuna uwanja unaitwa Black Rhino uko Karatu unamilikiwa na shule tu ni bora kuliko viwanja kibao vinavyotumika kwa Ligi Kuu.

Kwanini mameneja wa viwanja vibovu wasiende kupata somo huko?

Isiwe tu uwanja unafungiwa, hapana. Kuwe na maelekezo kwamba meneja wa uwanja uliofungiwa aende kupata darasa kwa meneja wa uwanja bora kama Meja Jenerali Isamuhyo, Tanzanite Kwaraa au Black Rhino.


TATIZO KUU

Viwanja kama CCM Kirumba - Mwanza, Jamhuri - Dodoma, Sokoine - Mbeya na hata Ali Hassan Mwanyi - Tabora nyasi zake zimezeeka.

Nyasi za viwanja hivi zilipandwa muda mrefu sana na kwa sasa zimemezwa na magugu ambayo sio rafiki kwa mpira.

Kinachotakiwa kufanywa ni kung’oa nyasi zote na uwanja usawazishwe upya na kisha zipandwe nyasi mpya.

Hivi ndivyo ilivyo kwa Uwanja wa Meja Isamuhyo, Tanzanite Kwaraa na hata Black Rhino.Nyasi zake ni mpya.

Nyasi za viwanja vikongwe zimeota kwa mafungu mafungu uwanjani. Hii ni zaidi ya kusababisha mpira kutotulia. Pia husababisha majeraha kwa wachezaji hasa vifundo vya miguu.

Hivyo, kama tunataka kurekebisha viwanja vyetu sio tu tuvifungie kupisha umwagiliaji maji, hapana. Nyasi zing’olewe na kupandwa nyasi mpya.

Fungia viwanja vyote vya hovyo acha ligi ichezwe Azam Complex - Chamazi, KMC Complex - Mwenge, Majaliwa - Ruangwa, Meja Jenerali Isamuhyo, Benjamin Mkapa, Tanzanite Kwaraa na kule New Amaan - Zanzibar.

Badilisha Kamati ya Leseni za Klabu ili kuongeza uwajibikaji kwani ni wazi huenda yenyewe haina leseni.