Tony Rashid afunguka safari yake ya ngumi, ndoto ya Las Vegas
Muktasari:
- Rashid maarufu AK 47 Bad Belle ni miongoni mwa mabondia wa Tanzania ambao wamejijengea heshima kwa kupigana ndani na nje ya nchi.
'KAZI KAZI' ndivyo unavyoweza kumwita bondia, Tony Rashid ambaye amekuwa na wakati mzuri tangu alipoanza kupigana mwaka 2017.
Rashid maarufu AK 47 Bad Belle ni miongoni mwa mabondia wa Tanzania ambao wamejijengea heshima kwa kupigana ndani na nje ya nchi.
Bondia huyo mwenye miaka 32, mzaliwa wa Mbeya anasema safari yake imekuwa na milima na mabonde, lakini amebaki kuwa mmoja wa mabondia wanaoamini mafanikio yanatokana na kazi, nidhamu na kutokata tamaa.
“Mimi napiga kazi kweli hata wapinzani wangu nikipigana nao wanajipanga haswa kwa sababu ili unipige basi lazima uhakikishe umeshiba vizuri,” anasema Rashid kwa msisitizo.
Safari ya bondia huyo kwenye ngumi ilianza mwaka 2017, kutokana na mapenzi makubwa kwenye mchezo huo.
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Rashid alisema mafanikio aliyoyapata kwenye mchezo huo hayajatokea kwa bahati mbaya, bali yametokana na kujituma tangu alipoamua kuufanya mchezo huo kuwa sehemu ya maisha yake.
Bondia huyo kutoka Mbeya alisema kila pambano analocheza huingia akiwa amejiandaa kushinda, jambo ambalo limemfanya kuendelea kuwa miongoni mwa mabondia wanaoheshimika nchini.
Kwa mujibu wa rekodi zake Boxrec, Rashid amecheza mapambano 24 ya kulipwa tangu alipoanza mwaka 2017, akishinda 17, kupoteza manne na kutoka sare mara tatu, huku ushindi mara 11 ukiwa kwa njia ya KO. Rekodi hiyo inaonyesha amepambana na mabondia mbalimbali kutoka Tanzania na Afrika Kusini, jambo lililompa uzoefu mkubwa wa kupambana katika viwango tofauti.
PAMBANO LIJALO
Rashid kwenye pambano lijalo la Dar Boxing litakalofanyika Julai 24 dhidi ya Juma Choki, anasema maandalizi yake yanaendelea vizuri na hana wasiwasi kwa sababu amekuwa na kambi nzuri Afrika Kusini.
Anaeleza muda wote aliokuwa kambini umetumika kuboresha uwezo wake wa kiufundi na kuongeza uimara wa mwili, huku akibadilishana uzoefu na mabondia mbalimbali kabla ya kurejea Tanzania kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya mwisho.
"Nimejiandaa vizuri sana. Hakuna kilichoharibika kwenye maandalizi yangu. Nilikuwa kambini Afrika Kusini na nimepata mazoezi mazuri pamoja na kubadilishana uzoefu na mabondia wengine, naamini mashabiki wataona Tony Rashid tofauti siku ya pambano," anasema.
HILI LILIMUUMA
Bondia huyo anasema mechi ambayo hataisahu ni dhidi ya Bongani Mahlangu wa Afrika Kusini mwaka 2021 akiitaja kuwa moja ya mapambano yaliyomuumiza zaidi katika maisha yake ya ngumi.
Rashid anasema alikuwa anaongoza kwa pointi lakini akapoteza umakini katika raundi za mwisho na kuondoka akiwa amepoteza pambano ambalo anaamini lilikuwa mikononi mwake.
"Nilikuwa naongoza vizuri, lakini mwisho wa pambano mambo yakabadilika. Liliniuma sana kwa sababu niliamini ushindi ulikuwa karibu kwangu. Hilo ndilo pambano ambalo limenifundisha ngumi zinaisha pale kengele ya mwisho inapolia," anasema Rashid na kuongeza.
“Natamani hata leo nirudiane naye ili nimaliza kisasi changu, naamini wakati huu sitazembea kama ilivyokuwa awali.”
HILI BORA
Pamoja na maumivu hayo, Rashid anasema yapo mapambano ambayo hayatasahaulika kirahisi kutokana na kiwango alichoonyesha.
Alilitaja pambano dhidi ya Oscar Richard ni miongoni mwa mapambano bora kabisa aliyowahi kucheza. Kwa mujibu wake, aliamua kubadili mbinu tofauti na zile alizokuwa akitumia mara nyingi, jambo lililomsaidia kutawala pambano hilo lililoandaliwa na Peak Time Media na kuwavutia wengi waliolifuatilia.
"Nilicheza kwa staili tofauti kabisa. Watu wengi waliona uwezo mwingine ambao sikuwa nimeuwahi kuuonyesha kabla hilo ni pambano ambalo huwa nalikumbuka mara nyingi," anasema.
NDOTO YAKE
Mbali na mafanikio ya ndani ya nchi, Rashid amesema ndoto yake kubwa ni kupanda kwenye majukwaa makubwa ya dunia. Ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo anaamini atakuwa akipigana Las Vegas, Marekani, mahali ambapo mabondia wengi wakubwa duniani wameandika historia zao.
Anaamini uwezo alionao, pamoja na maandalizi anayofanya sasa, vinaweza kumfikisha kwenye ndoto hiyo ikiwa ataendelea kupata mapambano ya kimataifa na usimamizi mzuri.
"Ninajiona Las Vegas ndani ya miaka mitano hivi ama 10. Nataka niwe mmoja wa mabondia wanaotambulika duniani hiyo ndiyo ndoto yangu kubwa na ninaifanyia kazi kila siku," anasema.
Anasema mapambano aliyopigana nje ya Tanzania yamechangia kwa kiasi kikubwa kumjenga kiufundi na kimawazo. Anaamini kushinda mataji ya ukanda wa Afrika ya Central Zone kutafungua milango ya kupigana katika nchi nyingine zenye ushindani mkubwa zaidi.
NGUMI NCHINI
Akizungumzia hali ya ngumi nchini, bondia huyo anawapongeza viongozi wanaosimamia mchezo huo kwa juhudi wanazozifanya kuendeleza ngumi za kulipwa.
Hata hivyo, anawataka kuhakikisha wanadhibiti mapambano yasiyo na ushindani wa kweli na kuhakikisha mabondia wanapangwa kucheza kwa haki ili kukuza hadhi ya mchezo huo.
"Usimamizi wa ngumi unaendelea kuwa mzuri, lakini ni muhimu kuhakikisha hakuna mapambano ya magumashi. Mabondia wapewe nafasi ya kupigana kwa haki kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kukuza mchezo wetu," anasema.
Alipoulizwa bondia anayemvutia zaidi duniani, Rashid alimtaja jina la Shushu wa Marekani, amekuwa akifuatilia namna anavyopigana na kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwake.
Aidha anasema katika maisha yake ya ngumi amewashinda mabondia wengi kwa uwezo wake halali, akimtaja Sabelo Ngebinyana kuwa mmoja wa wapinzani waliompa ushindani mkubwa lakini akaonyesha uwezo wake ulingoni.
NGUMI ZIMEMLIPA
Anasema ingawa hajafika anapohitaji lakini kwa kiasi fulani ngumi zimemlipa kwani sasa hivi anaishi maisha yake kutokana na mchezo huo.
"Alhamdulillah siyo haba lakini ngumi kusema ukweli hadi sasa zimenifanyia mengi lakini naamini njia zitafunguka kwa uwezo wa Mungu."
ALIKUWA DANSA
Kabla ya ngumi Rashid anasema alishawahi kuwa dansa lakini baada ya kushuhudia mazoezi ya marafiki zake waliokuwa mabondia akatokea kuupenda mchezo huo.
"Mimi nilikuwa dansa ingawa sikuwa najulikana lakini ndiyo kitu nilikuwa napenda kukifanya, nakumbuka kuna siku tulitoka na marafiki zangu kuangalia mazoezi yao ya ngumi basi na mimi nikabadili mawazo tangu hapo ndio watu wananifahamu hadi sasa," anasema.
Anasema mbali na kuwa dansa alishawahi kuuza chipsi kabla ya kuamua kuvaa glavu na kuingia ulingoni.
VIKWAZO
"Vikwazo kwenye mchezo wa ngumi vipo vingi sana mwanzoni wakati naanza nilipitia wakati mgumu sana kuna muda unafanya mazoezi bila ukiwa na njaa lakini kocha anakuambia pambana."
"Mimi nilifika hatua hadi ya kutaka kuacha kabisa ngumi lakini mzee wangu akanisihi sana na kuniambia usiache ngumi ila fanya kwa muda aliamini ngumi ingenifikisha mahali fulani."