Prime
Jonathan Sowah hakufika Simba kwa bahati mbaya
UNAMRUSHIA paka juu ya banda la kuku. Analinusa kisha anaachana nalo. Lazima kuna jambo. Haiwezi kuwa kawaida. Namna ambavyo Yanga waliamua kuachana na mpango wa kumsajili mshambuliaji Jonathan Sowah wakati akiwa na Singida Black Stars ilimshangaza kila mtu.
Kuna ile mechi ambayo Sowah alionekana akiwa amesimama katikati ya uwanja na rais wa Yanga, Hersi Said wakipiga stori baada ya pambano baina ya timu zao kumalizika. Baadaye Sowah akakaririwa akidai kwamba Hersi alikuwa kama baba yake na amekuwa naye karibu kwa muda mrefu. Na ni kweli.
Yanga walimtaka Sowah akiwa na Meneama ya Ghana. Mchezaji akaamua kwenda Libya ambako hakudumu kwa muda mrefu akajikuta akiangukia Singida Black Stars ambako ujio wake ulileta joto jipya nchini. Namna ambavyo alionekana kuwa mtambo wa mabao. Katika dunia hii yenye uhaba wa wafungaji Sowah alitutisha. Wote tukaamini kwamba ataenda kuishia Yanga.
Hakuna shaka kuhusu uhusiano wa Yanga na Singida Black Stars katika mambo haya. Wote tukajua kwamba Sowah angeweza kuwa Fiston Mayele mpya katika jezi ya Yanga baada ya Prince Dube kuanza maisha yake Yanga kwa kusuasua. Ilikuwaje Yanga wakaachana na mpango wa kumchukua Sowah? Haikuwa kwa bahati mbaya. Yanga walijua kitu.
Watu wengi walidhani kwamba Yanga waliachana na mpango wa kumsajili Sowah baada ya kugombana na kina Ibrahim Bacca katika fainali za Kombe la FA pale Unguja. Sio kweli. Ule ulikuwa ugomvi wa kawaida tu wa uwanjani. Yanga waliambiwa kuhusu tabia za Sowah mapema tu. Ndani na nje ya uwanja. Badala yake wakawa tayari hata kumchukua kwa mkopo, Andy Boyeli.
Akili ya kawaida ingekuwa rahisi tu. Kumchukua mchezaji ambaye amethibitisha ubora wake katika ligi yetu kuliko kumchukua mchezaji ambaye alikuwa anatua nchini kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, Hersi na genge lake waliamua kuchukua uamuzi tofauti na sisi tulivyofikiri. Inadaiwa kwamba hata Sowah mwenyewe alikuwa amejiandaa kutua Yanga na alichukizwa na uamuzi wa Yanga kutoendelea na mpango wa kumchukua.
Na kinachoendelea pale Simba kuhusu Sowah inaonekana kama vile kina Hersi walikuwa sahihi. Ushahidi wa mazingira katika miezi michache ya kwanza ya maisha yake Msimbazi unaonyesha kwamba Yanga walikuwa sahihi kuachana na mpango wa kumchukua staa huyo wa kimataifa wa Ghana. Kumbe lilikuwa ni bomu linalosubiri kulipuka.
Kwa sasa Simba wanahangaika na Sowah. Anashinda katika kamati za maadili ya nidhamu Msimbazi. Ni suala la utovu wa nidhamu ndani ya klabu. Kabla ya hapo alishafungiwa mechi nyingi kwa kumpiga kiwiko Himid Mao katika pambano ambalo siku hizi linaitwa Dabi ya Mzizima. Simba dhidi ya Azam katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Sowah hakufika nchini kwa bahati mbaya. Wala hakufika Simba kwa bahati mbaya. Tuna wachezaji kadhaa mahiri wa kigeni ambao wapo nchini na hawakufika kwa bahati mbaya. Wachache sana ambao tuliwapata kwa sababu tulichimba mifuko. Wengi tuliwapata kwa sababu mbalimbali. Kuna wavivu, kuna wasio na nidhamu, kuna ambao umri umesogea. Sowah mguu wake una mabao yanayohitajika popote duniani. Angeweza kuwa kwingineko lakini yupo kwetu labda kwa sababu ya tabia zake.
Kuna mchezaji naambiwa alikuwa kinda Hispania, lakini akaishia kucheza nchini. Kipaji kipo lakini ni mvivu. Hata aina yake ya mchezo ni ya kivivu ingawa kwetu aling’ara kwa sababu ya mashuti na matukio ya hapa na pale. Mchezo wake kiujumla unajua ni kwanini asingeweza kutamba katika mpira wa Ulaya. Mpira wa Ulaya una mahitaji makubwa kuliko uvivu wake. Hakufika nchini kwa bahati mbaya.
Haishangazi kuona kuna mastaa wetu wengi wa kigeni wakienda timu zilizo ‘serious’ huwa wanafeli na wanarudi nchini kuishi maisha rahisi ya soka letu. Hawapo hapa kwa bahati mbaya. Wachezaji wachache walikuwepo hapa nchini kwa bahati mbaya kama kina Nonda Shaban na Fiston Mayele.
Na sasa kuna huyu Sowah anaigharimu timu yake. Wakati huu Simba wakiwa wanaijenga upya timu huku wakiwa wamesajili wachezaji bora hasa katika maeneo ya pembeni mwa uwanja eneo la ushambuliaji walimhitaji Sowah na mabao yake. Walihitaji yale mabao yake ya Singida ayahamishie Msimbazi. Ni jambo ambalo limeshindikana mpaka sasa.
Naambiwa kwamba ana matatizo ya nidhamu nje ya uwanja kiasi kwamba wakubwa wa Msimbazi wanaona kama vile anatumika na watani wao kuwahujumu. Yupo kiongozi wa Msimbazi ambaye aliwahi kuniambia kwamba Sowah anavujisha hata siri zao kwenda kwa watani kwa sababu ana urafiki nao. Hata hivyo, sina cha kuwalaumu Simba ingawa walikuwa wanatoa tabia za kuudhi wakati wanamchukua.
Kwamba walijua kuwa hana nidhamu, lakini angekuwa anatumia nidhamu za kina Shomari Kapombe katika maisha yake ya Msimbazi. Sina cha kuwalaumu sana kwa sababu kuna wakati unatamani kitu fulani kutoka kwa mchezaji licha ya tabia zake mbaya. Kwamba hata Roberto Mancini alikuwa anajua Mario Balotelli alikuwa na tabia mbovu, lakini bado alimchukua Manchester City akiamini kwamba alihitaji sana mabao yake pengine kuliko nidhamu yake.
Sijui nini kitatokea kati ya Sowah na Simba, lakini ukweli ni kwamba amewaangusha mapema. Kabla ya nusu msimu tayari ameshaharibu. Huu ndio wakati wa kuchukua uamuzi mgumu. Simba wameshawahi kufanya hivyo huko nyuma na hata wakifanya tena sasa hivi hakuna atakayewalaumu. Tuachane na zile zama za kuwalinda wachezaji wasio na nidhamu ambao kiukweli wanalipwa pesa nyingi.
Lakini pia kuna kitu kingine cha kuweka sawa. Je ni kweli wachezaji kutoka Ghana wana shida? Watu wanamkumbuka Bernard Morrison. Alikuwa na shida hizihizi ndani na nje ya uwanja. Na sasa hivi Sowah anakwenda kwa mwendo uleule. Hili jambo linanishangaza kwa sababu mbili. Kwanza kabisa niliwahi kusafiri kwenda Ghana nikakaa kule wiki mbili. Waghana ni watu wenye upendo. Sio wakorofi. Hawa kina Sowah na Morrison sijui ni aina gani ya Waghana.
Lakini sio mbaya sana tukijikumbusha tabia za wachezaji mbalimbali maarufu wa Ghana. Wote hawana tabia hizi za kina Sowah na Morrison. Kina Michael Essien, Ally Sulley Muntari, Andre Ayew na Jordan Ayew pamoja na mastaa wengine wa Ghana. Wote hatujawahi kusikia wakiwa na matatizo ya nidhamu ndani na nje ya uwanja.
Rafiki yetu Muntari alikuwa anaonekana katika misikiti ya Milan akiwa anaswali na kufagia misikiti. Hii ni katika kipindi alichokuwa katika ubora wake wakati akicheza Inter Milan. Hapa ndio huwa najiuliza, hawa kina Sowah na Morrison ni Waghana wa wapi?
Kwa tabia zao ndio maana walifika nchini. Vipaji vyao ni vikubwa na wangeweza kwenda mbali kama wangefuata mienendo ya kina Muntari. Hawakufuata na ndio maana wameishia nchini na sio Inter Milan. Huyu Sowah naye hakufika Simba kwa bahati mbaya. Fikiria kwamba hata Yanga walishtuka licha ya kwamba alionekana kuwa na kila sababu ya kwenda Jangwani.