Jamil Mchaulu ‘Baloteli’; Vituko, mabao na maisha ya mtaani
Muktasari:
- Kama ilivyokuwa kwa Mario Balotelli wa Italia ambaye aliwahi kutawala vichwa vya habari kwa matukio yake ya ndani na nje ya uwanja, Baloteli wa Tanzania naye ana historia yake ya matukio yanayochekesha, kushangaza na wakati mwingine kumweka kwenye matatizo.
JAMIL Mchaulu, maarufu kwa jina la Baloteli, ni mmoja wa wachezaji waliotengeneza jina kubwa kwenye soka la mtaani kwa kipaji, mabao na vituko ya nje ya uwanja ‘utukutu’ vilivyomfanya kuwa gumzo.
Kama ilivyokuwa kwa Mario Balotelli wa Italia ambaye aliwahi kutawala vichwa vya habari kwa matukio yake ya ndani na nje ya uwanja, Baloteli wa Tanzania naye ana historia yake ya matukio yanayochekesha, kushangaza na wakati mwingine kumweka kwenye matatizo.
Kuanzia kukataa kufanya majaribio ndani ya Tanzania, kufungiwa chumbani kabla ya mchezo, mpaka kumpiga chenga kipa wa timu ya taifa na kisha kujipigia makofi mwenyewe huku akigoma kufunga, Jamil anaamini hayo yote ni sehemu ya tabia iliyomfanya kuwa yeye.
Lakini nyuma ya jina hilo lenye utata, kuna maisha marefu ya mpira yaliyopita kwenye akademi ya Azam, Simba B, Mbeya City, Mashujaa na hata safari ya kucheza nje ya nchi. Pia kuna simulizi nzito ya miaka minne aliyotumia kumhudumia mama yake aliyepooza na kupoteza uwezo wa kuona, kipindi ambacho anasema maisha yake ya soka yalikwama na watu wengi wakamsahau.
“Mi naitwa Jamil. Baloteli ni jina ambalo watu wamenipa. Lakini hata kabla ya kuitwa Baloteli, nilikuwa Jamil Go. Kila sehemu niliyokwenda kucheza nilikuwa nafunga, ndiyo maana watu wakaanza kuniita Jamil Go,” anasema Jamil.
Anasema jina hilo lilikuwepo muda mrefu kabla hata ya msh ambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samatta, kuanza kupata umaarufu mkubwa na baad aye kuitwa Samagoal na mashabiki.
Nilikuwa natumia jina la Jamil Go hata kwenye Instagram miaka ya nyuma. Kwa hiyo niliposikia Samatta anaitwa Samagoal sikushangaa. Ni vizuri kwa sababu naye anafanya kazi hiyo uwanjani. Huwezi kuitwa ‘Go’ bila sababu,” anasema.
AZAM NA KIZAZI CHA FEISAL
Safari yake ya mpira ilipitia akademi ya Azam, kipindi ambacho alikutana na baadhi ya wachezaji ambao leo ni majina makubwa katika soka la Tanzania. Miongoni mwao ni Feisal Salum, ambaye wakati huo alikuwa bado kijana anayepigania nafasi kwenye kikosi.
Jamil anakumbuka jinsi ushindani ulivyokuwa mkubwa ndani ya akademi hiyo, akieleza kuwa kila mwisho wa mwezi baadhi ya wachezaji walikuwa wakiachwa.
“Azam ilikuwa na ushindani mkubwa. Mazoezi yalikuwa mazuri, chakula kilikuwa kizuri, kila kitu kilikuwa sawa. Changamoto ilikuwa kila mwezi wanaacha baadhi ya wachezaji. Ulikuwa ukiona watu kama Feisal, Mudathir wa Yanga na wengine, wote wanataka nafasi,” anasema.
Anaamini mfumo wa Azam ulimsaidia sana kwa sababu walikuwa wakisoma na kucheza mpira kwa wakati mmoja.
“Azam ilikuwa klabu nzuri. Tulikuwa tunasoma hadi mpira darasani. Ndiyo maana watu wengi waliotoka pale walikuwa na kiwango kizuri. Mimi nilikuwa mmoja wa wachezaji waliokuwa na mashabiki wengi. Nikitoka kupasha nilikuwa nasikia watu wananiimba,”.
“SIKAI BENCHI”
Jamil anajielezea kama mshambuliaji mwenye kujiamini kupita kawaida. Anasema moja ya sheria zake kwenye soka ni kutokubali kukaa benchi.
“Kocha aliyenifundisha mimi na kuniweka benchi yupo wapi Tanzania? Nimecheza klabu nyingi. Mimi nikirudi kwenye timu sitaki kukaa benchi,” anasema kwa kujiamini.
Anasema hata mazoezi yake binafsi anayapanga kwa ratiba kali. Anaweza kukimbia kutoka Gongo la Mboto hadi Tazara na kurudi, kufanya push-up 100, kupumzika, kisha kwenda kukimbia mchangani kwa dakika 60.
“Jumatatu mpaka Ijumaa nina ratiba yangu. Naweza kuamka asubuhi nikakimbia, nikafanya push-up, nikapumzika, baadaye nikakimbia mchangani kwa dakika 60. Jioni naenda kucheza mpira wa mtaani. Mimi nikitaka kurudi kucheza lazima nijue nimejiandaa,”.
KISA CHA KUKATAA ‘TRIAL’
Moja ya visa vinavyomtofautisha Baloteli ni kile cha kukataa kufanya majaribio ndani ya Tanzania. Anasimulia kwamba aliwahi kwenda kwenye mchezo wa kirafiki akiwa na mpango wa kusaini mkataba Mbeya City ambayo ilikuwa ikinolewa na Juma Mwambusi, lakini mambo yakabadilika na kuambiwa afanye majaribio.
“Nilifika pale nakumbuka vizuri ilikuwa Morogoro na wakati huo walikuwa wakicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar nikaambiwa nivae jezi niingie nikafanye majaribio. Nikasema, ‘Teacher, mimi Tanzania sifanyi trial.’ Hilo nilimwambia kweli,” anasema.
Baadaye alikutana tena na kocha huyo katika mazingira tofauti wakati akiitwa kuanza mazoezi na Yanga. Badala ya kuingia uwanjani, Jamil anasema aliona mazingira yale hayakuwa yake na akaondoka.
“Nilipomuona tu nikajua hapa hakuna kitu. Nikavua hata viatu nikasema hapa hakuna jambo,” anasimulia huku akicheka.
KUFUNGIWA CHUMBANI
Lakini tukio lingine analolikumbuka zaidi ni la mchezo kati ya Azam na timu ya taifa ya vijana. Anasema kabla ya mchezo alianza akiwa amefungiwa chumbani, wakati wenzake wakiwa wanapanga kikosi.
“Nilikuwa nimefungiwa. Nilitoka kwenda chooni, nikarudi nikakuta nimefungiwa. Wenzangu wakaenda kwenye kikao cha kupanga kikosi, mimi sipo,” .
Azam ilianza mchezo na baadaye ikafungwa mabao mawili. Jamil anasema ilimbidi kupiga kelele ikitokea mtu mmoja alikuwa akipita eneo hilo ndipo alipopata msaada na kufunguliwa na mlango. Baada ya kuingia uwanjani, alifanya kile alichokizoea.
“Nilipata pasi ya Mudathir, nikafunga. Baadaye nikafunga tena kwa kichwa. Ikawa mbili mbili,” anasema.
Lakini tukio lililofuata ndilo lililobaki kwenye kumbukumbu za watu. Jamil anasema aliwalamba chenga mabeki na kipa wao, kisha badala ya kufunga akatoa mpira nje na kujipigia makofi. “Nilimtoa kipa mpaka nje ya 18. Nikawaangalia mashabiki, nikatoa mpira nje nikajipigia makofi. Mzungu (kocha wa Azam) akanitoa palepale,” anasema.
KUJITOSA
Kwa Jamil, mpira wa mtaani haukuwa burudani pekee pia ilikuwa sehemu ya kujenga jina lake.
Anasema ndondo zilimpa nafasi ya kucheza kwa uhuru baada ya mazoezi mazito ya programu ndani ya timu.
“Azam walikuwa wanatufanyisha mazoezi ya programu. Ukimaliza hayo, ukija kwenye ndondo unakuwa unaenda kumaliza hasira zako. Ndondo kwangu ilikuwa sehemu yangu,”
“Ukiniangalia kwenye ndondo, mimi naondoka na mabeki wawili, watatu au wanne. Yani kabla ya mechi yoyote nilikuwa nikipiga mikwara mabeki na kweli nilikuwa nikihakikisha nafunga,” anasema.
MAISHA YALIMVUTA NYUMA
Licha ya kujiamini kwake uwanjani, maisha nje ya uwanja yalikuja kumpiga Jamil pigo kubwa. Mama yake alipata matatizo makubwa ya kiafya, akapooza na kupoteza uwezo wa kuona.
Wakati huo Jamil alikuwa akicheza nje ya nchi, lakini aliamua kusimama na kurudi kumhudumia mama yake.
“Nilimlea mama yangu kwa karibu miaka minne. Alikuwa amepooza na amepoteza uwezo wa kuona. Akihitaji maji unampa, akitaka kula unamlisha, akitaka kuoga unamsaidia. Kulikuwa na mambo mengi.” Miaka hiyo ilimfanya aweke soka pembeni. Anasema alijua kwamba kukaa nje ya mpira kwa muda mrefu kungemfanya asahaulike.
“Ukikaa miaka minne nje mpira watu wanakusahu. Wengine wanakuja, wengine wanachukua nafasi. Ndiyo maana sasa nimepata nafasi hii ya kujitambulisha tena,”.
Baada ya mama yake kufariki, Jamil anasema alibaki na changamoto nyingine ya kuanza maisha upya.
“Maisha yalikuwa magumu. Kuna wakati mfukoni una Sh100, Sh200 au Sh1,000. Huna kazi, unategemea ndugu. Lakini nilikuwa najua lazima nirudi,”.
POMBE NA MAISHA
Anakiri kwamba kipindi cha changamoto kilimfanya aanze kunywa pombe, akieleza kuwa wakati mwingine alitafuta njia ya kusahau matatizo yaliyokuwa yakimkabili.
“Nilianza kunywa kipindi ambacho nilikuwa na changamoto nyingi. Ukiwa na mambo mengi kichwani, unatafuta kitu cha kukusahaulisha,” anasema.
Hata hivyo, anasema kwa sasa amebadilika na ameacha pombe. Anakanusha pia madai ya matumizi ya dawa za kulevya yaliyowahi kuhusishwa na jina lake.
“Skendo hizo nilipewa. Lakini mimi nimejiuliza, nikitumia dawa za kulevya nani atanisaidia? Nimekaa miaka minne bila timu, bado sijamuona mtu aliyenitetea. Sasa nitumie unga kwa nini?” anauliza.
AMCHAMBUA DOUMBIA
Jamil pia anajiona kama mtu anayependa kuchambua soka kwa jicho lake mwenyewe. Anaamini wachezaji wengi wanaotambulishwa Tanzania wanapewa sifa kabla ya kuangaliwa kwa undani. Anatoa mfano wa wachezaji wanaokuja Simba na Yanga na kupewa majina makubwa kutokana na idadi ya mabao waliyofunga.
“Watu wa Tanzania wanatakiwa wajue mchezaji anacheza aina gani ya mpira. Usisikie tu ana mabao 10 au 15 ukasema ni hatari. Mwangalie anavyocheza.”
DIAMOND NA WASAFI
Mbali na soka, Baloteli amewahi pia kuonekana kwenye mazingira ya burudani, hasa akiwa karibu na wasanii maarufu.
Anakumbuka safari yake ya kushiriki shughuli za Wasafi Festival, ambako alikutana na watu wa karibu na Diamond Platnumz.
“Nilipigiwa simu nikaambiwa tufanye Wasafi Festival. Nikakubali. Nilikwenda mpaka Mtwara,”.
Kutoka hapo, anasema alianza pia kupata nafasi ya kuonekana kwenye matukio mbalimbali na kujenga jina lake kwenye mitandao ya kijamii.
“Wakati ule interviews hazikuwa nyingi kama sasa. Mimi nilitoka kwenye shida, nikawa najitafuta. Hata video nilizokuwa nikifanya na watu kwenye magari zilianza hivyo hivyo. Nilikuwa napigisha watu stori, tunakwenda nao kwenye show.
BADO SIJAFA
Pamoja na misukosuko yote, Jamil anaamini bado ana nafasi ya kurudi kwenye soka na kujenga maisha yake upya.
Anasema kipindi cha kukaa nje ya soka kilikuwa kama kuzimia, lakini hajafa.
“Mimi sijafa. Nimezimia tu. Ukizimia kuna siku unazinduka, lakini ukifa huwezi kuzinduka. Kwa hiyo naamini bado nina nafasi,”.
Kwa sasa anasema anafanya mazoezi na watu mbalimbali, akiwamo Ibrahim Ajibu ambaye anamtaja kama mmoja wa watu anaowaamini sana.
Anasema Ajibu amebadilika na sasa amekuwa mtu wa mazoezi na anayejitolea kuwafundisha vijana.
“Watanzania wasimchukulie tofauti. Ibra ni mtu makini. Mimi naamini ukinitoa mimi, sioni kama kuna mtu hatari kama Ibra,”.
Jamil anasema anaendelea kutafuta timu huku akitumia mitandao ya kijamii kujitangaza tena.