Celine Dion anazeeka na utajiri wake
Muktasari:
- Nyota huyo wa muziki wa pop na ballad, anayefahamika kwa sauti yake ya kipekee, ameendelea kuvuna matunda ya kazi yake ya zaidi ya miongo minne katika muziki.
MONTREAL, CANADA: MWANZONI mwa mwaka huu, jina la mwimbaji nguli wa Canada, Celine Dion, liliendelea kutawala vichwa vya habari za burudani duniani licha ya changamoto za kiafya alizopitia katika miaka ya hivi karibuni.
Nyota huyo wa muziki wa pop na ballad, anayefahamika kwa sauti yake ya kipekee, ameendelea kuvuna matunda ya kazi yake ya zaidi ya miongo minne katika muziki.
Mbali na heshima kubwa aliyoijenga kisanaa, Celine pia anatajwa kuwa miongoni mwa wasanii wanawake matajiri zaidi duniani. Mapato yake yanatokana na mauzo ya albamu, ziara mbalimbali na biashara nyingine.
Hapa tumekusogezea mchanganuo wa kina wa utajiri wake na jinsi anavyovuna pesa.
ANAPIGAJE PESA
Kwa sasa, utajiri wa Celine Dion unakadiriwa kufikia takribani Dola 500 milioni, ambao kwa asilimia kubwa umetokana na mapato aliyokusanya kwa muda mrefu kupitia muziki na uwekezaji wa sehemu mbalimbali.
Ameuza zaidi ya nakala milioni 200 za albamu duniani, jambo linalomweka katika orodha ya wasanii waliouza sana katika historia ya muziki.
Albamu kama Falling Into You, Let’s Talk About Love na A New Day Has Come zimemwingiza zaidi ya Dola 300 milioni.
Amepata pia pesa nyingi kupitia ziara zake za kupiga shoo duniani ambako amepata zaidi ya Dola 200 milioni.
Kwa mjumusho wa shoo zake alizowahi kupiga Marekani na Canada amepata takribani Dola 680 milioni.
Celine amekuwa balozi wa kampuni kubwa kama La Oreal, pamoja na kampuni kadhaa ambazo kwa mwaka zinampa takribani Dola 10 milioni.
Pia ana biashara yake binafsi ya manukato (perfumes) ambayo imeuza mamilioni ya chupa duniani, ana biashara nyingine ya kampuni ya utengenezaji nguo za watoto iitwayo CELINUNUNU.
Kuna wakati alikuwa balozi wa kampuni ya ndege ya Air Canada ambayo ilikuwa ikitumia sauti yake katika matangazo yao.
Kwa mujibu wa jarida la Fobres, staa huyu anaingiza Dola 40 milioni kwa mwaka kupitia biashara zake.
MIJENGO
Ana jumba la kifahari huko Florida, Marekani lenye thamani ya takribani Dola 30 milioni, ambalo ndani yake lina bustani kubwa, bwawa la kuogelea na fukwe binafsi.
Vilevile ana nyumba nyingine ya kifahari maeneo ya Montreal, Canada inayokadiriwa kuwa na thamani ya Dola 15 milioni, ambapo hupendelea sana kukaa na ndiko anakoishi na familia yake.
Pia anamiliki nyumba Las Vegas na Paris ambazo sana huzitumia wakati wa mapumziko.
MSAADA KWA JAMII
Celine Dion ni mmoja wa wasanii wanaosifika kwa kuwa na moyo wa kutoa na kurudisha kwa jamii.
Ameanzisha taasisi yake ya Celine Dion Foundation, inayosaidia watoto wenye magonjwa hatarishi na familia zisizojiweza.
Amechangia mamilioni ya dola katika sekta ya afya, hususani kwenye utafiti wa magonjwa kadhaa na misaada kwa waathirika wa majanga ya asili.
Pia amekuwa mstari wa mbele kusaidia taasisi za afya nchini Canada na duniani kote.
FAMILIA NA MAISHA BINAFSI
Celine Dion aliolewa na Rene Angelil (sasa marehemu) mwaka 1994, ambaye pia alikuwa meneja wake na walidumu hadi Rene alipofariki dunia mwaka 2016.
Wakiwa katika ndoa, walijaliwa kupata watoto watatu: Rene Charles na mapacha Eddy na Nelson.