Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JABULANI; Maisha ya pili ya mpira uliobezwa kwa ubaya

JABULANI Pict

Muktasari:

  • Ingawa kwa wengi footgolf siyo maarufu hapa nchini, katika nchi zilizoendelea ni aina ya mchezo wa kifahari unaochezwa na watu wachache mara nyingi kwa ajili ya kujifurahisha, lakini katika siku za karibuni watu wengi wanaucheza na tayari umeanzisha shirikisho lake maarufu kama Federation for International FootGolf (FIFG).

LONDON, ENGLAND: FAINALI za Kombe la Dunia 2010 zilizopigwa Afrika Kusini zilikuja na kuondoka na mpira wake uliokuwa maarufu kwa jina la Jabulani ambao ulijizolea umaarufu wa aina yake.

Miaka zaidi ya 15 baada ya fainali hizo, gozi hilo la ng’ombe limerejea, lakini safari hii likitumika katika mchezo tofauti na soka; footgolf (mchezo wa gofu ya mpira wa miguu ambapo mchezaji hutumia mpira wa soka kuupeleka kwa teke hadi kwenye shimo maalumu lililo ardhini. Lengo ni kuufikisha mpira kwenye shimo kwa idadi ndogo zaidi ya mipigo, kama ilivyo kwenye gofu).

Ingawa kwa wengi footgolf siyo maarufu hapa nchini, katika nchi zilizoendelea ni aina ya mchezo wa kifahari unaochezwa na watu wachache mara nyingi kwa ajili ya kujifurahisha, lakini katika siku za karibuni watu wengi wanaucheza na tayari umeanzisha shirikisho lake maarufu kama Federation for International FootGolf (FIFG).

Achana na hilo, lakini katika mchezo huo Jabulani ndiyo habari ya mjini kwa sasa ikiuzwa takriban Pauni 500 (zaidi ya Sh1.7 milioni) na unaonekana kupapatikiwa na matajiri wengi Ulaya wanaocheza footgolf na miongoni mwao ni supastaa wa kimataifa wa England, Ben Clarke ambaye ni nyota wa kulipwa wa mchezo huo.

JABU 01

Clarke bingwa wa FootGolf World Tour mara nne, na amekuwa akishika nafasi miongoni mwa wachezaji watatu bora duniani tangu 2020, takribani mara moja kwa mwezi, amekuwa akitembea na boli hilo kwenye mkusanyiko wake wa mipira ya Adidas Jabulani inayotumiwa sana kwa sasa.

Kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa kiwango cha juu, Clarke ana mkusanyiko mkubwa wa mipira, ambayo yote inahitaji kujazwa hewa mara kwa mara ili kuzuia kuharibika, hata ile iliyohifadhiwa ikiwa mipya ndani ya boksi lake la awali, bila hata kuguswa na kiatu.

Mipira ya miguu ni mali muhimu katika mchezo huo wa kipekee ambao unawataka wachezaji kuipiga kwa mguu kuizungusha kwenye uwanja na kuiingiza kwenye mashimo 18 makubwa kuliko yale ya kawaida (ya gofu), kwa idadi ndogo zaidi ya mipigo iwezekanavyo. Usahihi ndiyo kila kitu katika mchezo huo.

Kwa hiyo, inaonekana kama jambo la kushangaza kwamba mpira unaopewa nafasi ya heshima zaidi katika mkusanyiko wa Clarke ni Jabulani maarufu, ambao wakati mmoja kocha Fabio Capello katika fainali za Kombe la Dunia 2010 aliuelezea kuwa “mpira mbaya zaidi ambao nimewahi kuuona katika maisha yangu.”

JABU 02

Kocha huyo wa zamani wa England hakuwa peke yake katika kuukosoa, kwani pia kipa wa zamani wa England, David James, aliuita “wa kutisha”, huku mwenzake wa Brazil, Julio Cesar akisema ulikuwa “kama ile mipira unayonunua supermarket”, wakati mshambuliaji wa Brazil, Robinho, alidai kuwa “mtu aliyebuni mpira huo hajawahi kucheza soka.”

Ni mipira michache iliyowahi kubezwa kwa kiwango kikubwa kama ule uliotengenezwa kwa ajili ya Kombe la Dunia 2010, ambako mwenendo wake usiotabirika ulifanya ulalamikiwe kuwa hauwezi kudhibitiwa, hasa kunapotokea kuwapo kwa upepo.

Hata hivyo, miaka 16 baadaye, mahitaji ya wachezaji bora wa footgolf duniani yana maana kwamba mtu yeyote anayemiliki Jabulani sasa amekaa kwenye mgodi wa dhahabu, huku mipira iliyohifadhiwa ndani ya maboksi ikiuzwa kwa zaidi ya Pauni 500 na thamani yake ikiendelea kupanda.

“Ni jambo la kushangaza kidogo,” anasema Clarke, anayeishi Hertfordshire, England na ambaye aliwahi kuongoza viwango vya dunia vya footgolf mara tano.  “Hakuna mtu aliyekuwa na uwezo wa kuudhibiti mpira huo kwenye Kombe la Dunia 2010, lakini hapa tulipo sasa tunautumia katika mchezo unaohitaji usahihi. Sote tunauamini na kuutegemea. Ni jambo la ajabu sana.”


JABU 03

HII HAPA SABABU

Sababu yake iko kwenye kasoro maalumu ya kihandisi ya Jabulani, ambayo iliwakwaza sana wachezaji wa soka kwenye fainali za Kombe la Dunia 2010.

 Jabulani ulitengenezwa kwa paneli nane zilizounganishwa kwa joto ikiwa ni pungufu kutoka 14 zilizotumika kwenye Adidas Teamgeist, mpira wa Kombe la Dunia 2006, jambo lililopunguza sana mishono na kuufanya kuwa mpira laini na wa mv iringo zaidi kuwahi kutengenezwa.

Unapopigwa kwa mzunguko mdogo kwa kasi kubwa ambayo wanasoka wa kiwango cha juu hutumia wanapopiga mashuti au krosi, ulisababisha kuwa na mwelekeo usiotabirika, ukibadilisha ghafla mwelekeo au mzunguko ama kushuka chini ilhali ulipaswa, kulingana na mpigaji, upae juu.

Kinyume chake, kwa wachezaji wa footgolf, ambao hupiga mpira kwa kutumia sehemu ya ndani ya mguu ili kuupa mzunguko unaotabirika, mishono michache ya Jabulani husaidia mpira kwenda mbali zaidi kuliko mpira mwingine wowote. Mipira ya Adidas ya kipindi hicho ndiyo pekee inayokaribia kiwango hicho ikiwamo Teamgeist, Terrapass, Speedcell na Torfabrik ya awali.

Kwa kuwa hakuna aina yoyote kati ya hiyo ambayo imekuwa ikitengenezwa kwa karibu miaka 15, mahitaji makubwa kutoka footgolf ya kiwango cha juu yakichanganyika na uhaba wa mipira hiyo, yamesababisha bei ya Jabulani kupanda sana.

“Inazidi kuwa adimu na ghali zaidi,”  anasema Clarke, ambaye ana Jabulani tatu zilizohifadhiwa ndani ya maboksi, pamoja na mipira mingine mingi ya Adidas ya kipindi hicho.

JABU 04

“Sijanunua mmoja kwa miaka kadhaa, kwa sababu tu ya jinsi bei zilivyokuwa ghali. Kwa kawaida unapata kutoka kwa wachezaji wen-gine wa footgolf au wakusanyaji wanaouza kwa sababu wamegundua soko la footgolf. Wa mwisho nilioupata ulikuwa karibu Pauni 250 (zaidi ya Sh87 ,000) takribani miaka mitatu iliyopita, lakini sasa ni pauni 500 au zaidi. Inaweza kuwa kosa la gharama kubwa ukimpiga kwenye mti na ukapasuka.”

Kuna makubaliano ndani ya mchezo huo kwamba hali hii haiwezi kuendelea kwa muda mrefu, kwani Sean Rontree, mmoja wa wakurugenzi wa chombo kinachosimamia footgolf nchini England, ana Jabulani tatu na Speedcell tatu katika mkusanyiko wake binafsi.  “Itakuja siku ambapo hakutakuwa na (mpira kama huo) mwingine sokoni,”  anasema Rontree nakuongeza:

“Adidas hawatakubali kutengeneza mingine. Tumewahi kufanya mazungumzo nao, lakini idadi ambayo wangetakiwa kutengeneza ili iwe na faida karibu mipira 10,000 ni kubwa kuliko uwezo wetu.”