Iwobi kwenye kisa cha kubebWa na Okocha, Ronaldinho utotoni

Muktasari:
- Kuna hili la Alex Iwobi. Usichokijua, staa huyo wa Kinigeria utotoni alibebwa na mafundi wa mpira, Jay-Jay Okocha na Mbrazili Ronaldinho.
LAGOS, NIGERIA: LAMINE Yamal amekuwa moto mkali uwanjani kwa sasa, akicheza soka lake la uhakika Barcelona na timu ya taifa ya Hispania. Na wakati akifanya hilo, kuna stori kwamba aliogeshwa na supastaa wa soka, Lionel Messi wakati alipokuwa mtoto.
Ameambukizwa makali ya Muargentina huyo? Achana na hilo la Yamal na Messi.
Kuna hili la Alex Iwobi. Usichokijua, staa huyo wa Kinigeria utotoni alibebwa na mafundi wa mpira, Jay-Jay Okocha na Mbrazili Ronaldinho.
Na sasa, Iwobi amebainisha dhamira yake ya kufikia soka la viwango bora kabisa kama magwiji hao waliombeba wakati akiwa mtoto. Kuhusu Okocha, huyo ni mjomba wa Iwobi na wote ni Wanigeria.
Kuhusu Ronaldinho kwenye mataji hakuwa mnyonge, alishinda Copa America mwaka 1999 na Kombe la Dunia 2002 akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya Brazil.

Okocha na Ronaldinho waliwahi kucheza kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain na wawili hao ni mafundi wa chenga za maudhi. Wakati Ronaldinho na Okocha wakiwa pamoja PSG, kikosi hicho kilikuwa na wakali wengine pia kama Mikel Arteta, Mauricio Pochettino, Nicolas Anelka na Gabriel Heinze.
Ronaldinho na Okocha walipokuwa pamoja kwa msimu mmoja huko Ufaransa, kabla ya mmoja wao, fundi wa Kinigeria kwenda kujiunga na Bolton mwaka 2002.

Lakini, kwa upande wa Iwobi - aliyezaliwa Mei 1996 - amefahamu kwamba, alipokuwa mtoto, alipata nafasi ya kubebwa na masupastaa wakubwa sana kwenye soka, ambao walikuwa wakicheza soka la ufundi na kuburudisha mashabiki.
Winga huyo wa Fulham mwenye umri wa miaka 29 kwa sasa aliiambia SunSport: “Kitu kilichovutia ni kwamba nilikuwa Barcelona na kumwona Ronaldinho.
“Nilirudi kumwambia mama yangu, ‘Nimemwona Ronaldinho.’
“Na mama yangu, alisema, ‘Unajua alikubeba wakati ulipokuwa mdogo kipindi alipokuwa akicheza PSG na mjomba wako?’
“Alinionyesha hadi picha.”

Okocha alipata umaarufu mkubwa kwenye Ligi Kuu England kwa kipindi chake cha miaka minne aliyokuwa katika kikosi cha Bolton, ambapo Iwobi alipata nafasi ya kuangalia mafanikio hayo na kuhamasika kufuata nyayo za mjomba wake huyo.
Iwobi na Okocha wamekuwa na uhusiano wa karibu sana, lakini mjomba mtu amejizuia kumpa ushauri wa kuhusu soka mpwa wake. Lakini, bila shaka Iwobi atamgeukia Okocha katika kuelekea fainali za Afcon wakati akipambana kuwa mtu wa pili kwenye familia hiyo kunyakua taji hilo la ubingwa wa Afrika akiwa na kikosi cha Super Eagles.
Okocha wakati akiwa kwenye kikosi cha Nigeria walitokea nyuma dhidi ya Zambia mwaka 1994 na kunyakua taji la Afcon ikiwa ni moja ya mataji yaliyobebwa na kikosi hicho.

Iwobi na wenzake walikumbana na pigo mwaka jana, wakati walipochapwa na Ivory Coast kwenye mechi ya fainali, wapinzani ambao waliwafunga wakati walipokutana kwenye hatua ya makundi.
Na sasa Iwobi anajiandaa kwenda kufikia nyayo za mjomba wake kwa kuwa mtu wa pili kwenye familia yao kubeba ubingwa wa taji la Afcon katika fainali itakayofanyika Morocco, Januari 18, 2026. Fainali hizo za Afcon 2025, zitaanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.
Iwobi kwa wakati huu yupo kwenye majukumu kucheza mechi za hisani zinazofanywa na asasi zake za kiraia, alisema: “Mwaka jana, tulikaribia kushinda. Kilichouma zaidi, tulifungwa na wenyeji ambao tuliwafunga kwenye hatua ya makundi na kuongoza kundi letu.

“Natumaini mwaka huu utakuwa wetu. Kuna majina makubwa sana, nchi kubwa kwenye michuano. “Tunaamini tuna wachezaji wenye uwezo wa kufanya hivyo. Mjomba alijipambanua mwenyewe akicheza akiwa na tabasamu usoni.”